1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Serikali, Waasi watia saini makubaliano ya amani-Ivory Coast

Nchini Ivory Coast, Serikali na waasi nchini humo wametia saini mkataba wa amani ikiwa ni juhudi za kurejesha hali ya utulivu katika taifa hilo la Afrika ya magharibi.

Pande mbili hizo mbili zilikubaliana kuunda serikali ya mseto ndani ya wiki tano na vile vile kuunda jeshi la pamoja.

Mkataba huo ulisainiwa hapo jana mjini Ouagadogou,nchini Burkina Faso ,mbele ya Rais Laurent Bagbo na kiongozi wa waasi Guillame Soro.

Lengo kubwa la makubaliano hayo ni kuiunganisha nchi hiyo ,iliyokuwa imegawanyika sehemu mbili ilhali eneo la kaskazini likimilikiwa na waasi toka mwaka 2002.

Mkataba huo wa amani umekuja baada ya mwezi mmoja wa mazungumzo kati ya pande mbili hizo.

Lakini mpaka hivi sasa bado haijajulikana ni nani atakuwa waziri mkuu wa serikali mpya ya muungano ingawa kuna habari kuwa huenda nafasi hiyo akapewa kiongozi wa waasi Guillame Soro.

Vile vile katika mkataba huo imeamuliwa kuundwa kwa jeshi la pamoja ndani ya wiki mbili zijazo kati ya waasi na wafuasi wa Rais Bagbo.

Kipengele kingine katika mkataba huo kinajumuisha ratiba ya usalimishaji wa silaha kwa waasi na utayarishwaji wa vitambulisho kama zoezi la kuwatambua mamilioni ya raia wa nchi hiyo.

Inakadiriwa kuwa uchaguzi ambao umeahirishwa mara mbili hivi sasa, utafanyika baada ya miezi 10 ijayo .

Katibu mtendaji wa umoja wa kiuchumi wa nchi za magharibi mwa Afrika , ECOWAS Bwana Mohamed Chambas, amesema makubaliano hayo ya mjini Ouagadogou ni tofauti na awali , ambapo sasa pande zote mbili zimekubaliana.

Amesema utiaji saini wa mkataba huo utapelekea maendeleo zaidi ya kiuchumi katika eneo la Afrika ya magharibi na kuwa mfano kwa wengine.

Kwa upande wake Ufaransa , nchi ambayo iliitawala Ivory Coat imesema imefurahishwa na hatua iliyofikiwa na pande hizo mbili, kwani itamaliza mzozo wa muda mrefu nchini humo.

Vita ya wenyewe kwa wenyewe iliibuka nchini humo mwaka 2002 kufuatia jaribio lililoshindwa la kumuondoa madarakani Rais Laurent Bagbo.

Mfululizo wa mikataba ya amani ilifuatia toka mwaka 2003, lakini ilishindwa kuzaa matunda baada ya waasi kutokubali kuweka silaha chini,. wakidai marekebisho katika baadhi ya vipengele .

Mojawapo ya kipengele ambacho kilitakiwa kufanyiwa marekebisho ni utoaji wa vitambulisho na usalimishaji wa silaha.

Waasi hao kutoka kaskazini ya Ivory Coast , sehemu ambayo hukaliwa na jamii ya wafuasi wengi wa dini ya kiislam , wanadai kubaguliwa na serikali ya Rais Laurent Bagbo.

 • Tarehe 05.03.2007
 • Mwandishi Charles Mwebeya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHIw
 • Tarehe 05.03.2007
 • Mwandishi Charles Mwebeya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHIw

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com