1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali kuu ya Ujerumani yarefusha muda wa harakati za jeshi la Ujerumani nchini Sudan

Hamidou, Oumilkher13 Agosti 2008

Wanajeshi wa Ujerumani watasalia hadi Agosti 15 mwakani nchini Sudan.

https://p.dw.com/p/EwUv
Vikosi vya Umoja wa mataifa vya UNAMID nchini SudanPicha: AP



Serikali ya Ujerumani imeamua kurefusha muda wa kuwepo vikosi vya jeshi la Shirikisho-Bundeswehr,katika jimbo la machafuko la Darfour na katika eneo la kusini la nchi hiyo.Vikosi vya jeshi la shirikisho vinatumikia harakati za amani zinazosimamiwa kwa pamoja na umoja wa mataifa na umoja wa Afrika.


Muda wa kutumikia harakati za kulinda amani zinazongozwa na Umoja wa mataifa na Umoja wa Afrika UNAMID huko Darfour na juhudi nyengine kama hizo kusini mwa Sudan -UNMIS umerefushwa kwa mwaka mmoja na utamalizika Agosti 15 mwakani.


Uamuzi wa baraza la mawaziri la serikali kuu ya Ujerumani utabidi kwanza uidhinishwe na bunge la shirikisho Bundestag.


Jeshi la shirikisho limepangiwa zaidi kujishughulisha na kuwasafirisha wanajeshi kwa njia ya angani,kusimamia mahitaji ya tume hiyo ya amani ya UNAMID na kutoa mafunzo.Jumla ya wanajeshi 26 elfu wamepangiwa kutumikia shughuli za kulinda amani za UNAMID.Hadi sasa lakini ni thuluthi moja tuu ya wanajeshi waliofika Darfour.


Wanajeshi hadi 250 pamoja pia na Polisi wa Ujerumani wanaruhusiwa kushiriki katika mpango huo.

Baadhi ya wanasiasa wanahofia mpango huo wa amani usije ukashindwa kwasababu ya kushindwa wafadhili kutekeleza ahadi zao kwa upande wa kuchangia wanajeshi na vifaa pia.


Mtaalam wa masuala ya Afrika wa kutoka kundi la CDU/CSU katika bunge la Shirikisho-Bundestag,Hartwig Fischer akiulizwa kama usalama umeimarika mwaka mmoja tangu tume hiyo ya UNAMID ilipoanzishwa anasema:


"Hasha,hali si salama.Makundi ya waasi yanaendelea kupigana yenyewe kwa yenyewe.Serikali inawapiga vita raia zake wenyewe huko Darfur na wanajeshi wa kimataifa hawatoshi ,sawa na visivyotosha vifaa vya kijeshi kuweza kuzuwia mauwaji,mitindo ya watu kutimuliwa makwao na ubakaji."


Wakati huo huo jeshi la Sudan limeanzisha opereshini kubwa kwa lengo la kufyeka vituo vya waasi katika ncha ya kaskazini ya Darfour.


Wanajeshi wa serikali waliosheheni ndani ya magari 200 wamehujumu eneo la Ouadi Atron,karibu na mpaka wa Sudan na Libya na kudhibiti maeneo yaliyokua yakidhibitiwa na waasi wanaodai utawala mkubwa wa ndani.


"Wamekuja wakiwa ndani ya magari 200 ya kijeshi na wamewauwa watu sabaa."Amesema hayo kamanda Souleiman Marajane wa jeshi la waasi wanaopigania Ukombozi wa Sudan-SLA.


Mwenyenzake wa kundi lililojitenga la SLA,Al Sayyid Cherif amethibitisha jeshi la serikali ya Sudan limehujumu vituo vyao huko Ouadi Atron.


 "Tunaangalia hujuma hizi kua ni sawa na tangazo jipya la vita" amesema.


Msemaji wa jeshi la Sudan hakutaka kusema chochote kuhusu ripoti hizo.


Duru za kijeshi zimethibitisha hujuma zinaendelea,lakini hazikufafanua pia.


Kwa mujibu wa kamanda Souleiman Marajane,serikali ya Sudan imetuma wataalam wa kichina katika maeneo hayo yanayohujumiwa kwa lengo la kutafuta mafuta.


Eneo la kaskazini la Darfour ni sehemu ya zoni iliyopewa jina la "Bloc 12A" ambako shughuli za kuchimba mafuta zimekabidhiwa kampuni la  Al Kahtani la Saud Arabia.


Makampuni ya China yanadhibiti sekta ya mafuta nchini Sudan inayochimba mapipa laki tano kwa siku.