1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sera ya pamoja kuhusu uhamiaji yajadiliwa Kampala

Admin.WagnerD15 Mei 2017

Wajumbe kutoka serikali na mamlaka za Afrika wameanzisha mchakato wa kuunda sera ya pamoja kuhusu uhamiaji kufikia mwaka 2018 katika kongamano linalofanyika mjini Kampala, Uganda.

https://p.dw.com/p/2d06q
Uganda Panafrikanisches Forum zu Migration in Kampala
Picha: DW/L. Emmanuel

Wajumbe kutoka serikali na mamlaka za Afrika wameanzisha mchakato wa kuunda sera ya pamoja kuhusu saula la uhamiaji kufikia mwaka 2018. Katika Kongamano ambalo linaratibiwa na Umoja wa Afrika kwa ushirikiano na mashirika ya kimataifa yanayoshughulikia uhamiaji, wajumbe hao wanatarajiwa kujadili masuala kuhusiana na sababu, athari na fursa zilizoko kuhusu uhamiaji wa hiari na pia ule wa lazima.

Katika kongamano la siku tatu lililoanza siku ya Jumapili (14.05.2017) wajumbe kutoka zaidi ya mataifa 40 ya Afrika, mataifa ya mashariki ya kati na pia Ulaya ambapo wahamiaji wengi kuwasili baada ya kufanya safari za hatari wanalenga kukubaliana juu ya sera muafaka itakayozingatiwa na mataifa yote ya afrika na baadaye kuwasilishwa kwa mataifa mengine.Wajumbe hao kwa sasa wanauchukulia uhamiaji kama janga la kimataifa kutokana na tofauti za kisera miongoni mwa mataifa wanakotoka wahamiaji, wanakopitia na wanakoelekea.Charles Obila ni afisa wa uhamiaji kutoka jumuiya ya ushirikiano wa kimaendeleo IGAD.

Kulingana na takwimu za umoja mataifa, mtu mmoja kati ya saba duniani amehamia nchi nyingine.Huku zaidi ya wafanyakazi zaidi milioni 150 wakielezwa kuwa wahamiaji, hadi watu milioni 16 ni wakimbizi katika mataifa mengine.Uganda ndiyo nchi iliyo na wakimbizi wengi barani afrika wapatao milioni moja laki mbili.Waafrika milioni 50 wameyahama mataifa yao kutokana na sababu moja au nyingine. Isitoshe hadi aslimia 48 ya wahamiaji ni wanawake. 

Uganda Panafrikanisches Forum zu Migration in Kampala
Laura Thompson, Naibu Mkurugenzi wa shirika la kimataifa la Uhamiaji, IOM, akihutubia kongamano la mjini Kampala (15.05.2017)Picha: DW/L. Emmanuel

Wimbi la wahamiaji wa Kiafrika

Wimbi la uhamiaji kutoka Afrika limeshuhudiwa hasa katika maitaifa ya Afrika Magharibi, kaskazini na maitaifa ya pembe la Afrika ya mashariki. Idadi kubwa ya wahusika ni wahamiaji haramu wasio na hati za kusafiria ambao hufanya safari za hatari kutafuta kile wanachokitaja kuwa maisha bora barani Ulaya na katika mataifa ya mashariki ya kati.

Washiriki katika mkutano huo wana imani kuwa suala hilo linaweza kutatuliwa iwapo Afrika itatumia fursa bora zilizoko za rasilimali yake kubuni nafasi za kazi hasa kwa vijana wake. Wwaziri mkuu wa Uganda Dr. Ruhakana Rugunda ndiye aliyelifungua rasmi kongamano hilo.

Miongoni mwa hatua wanazozingatia wajumbe ni kurahisisha uhamiaji miongoni mwa mataifa ya afrika ili nguvukazi na maarifa wanazohamisha waafrika viwe vya manufaa kwa bara lenyewe. Hii itakuwa mojawapo ya njia ya kupunguza umasikini na pia kujenga uchumi wa afrika bila kutegemea misaada kutoka nje.Hata hivyo chuki dhidi ya wageni kama inavyoshuhudiwa kila mara afrika kusini ambapo raia wa mataifa mengine ya afrika wameshambuliwa na wenyeji wanaodai kwamba wamewapokonya fursa za ajira na mapato ni kielelezo tosha kwamba bado kuna safari ndefu kufikia ndoto hiyo.

Kulingana na takwimu za mashirika ya kuhamisha pesa, raia kutoka nje Afrika hutuma kiasi kikubwa cha pesa nchini kwao. Pesa hizo ni mara tatu ya zile za misaada ya dola biloni 35 inayotolewa kwa Afrika kila mwaka. Mapendekezo ya kongamano hilo yatawasilishwa kwa viongozi wa umoja wa afrika ili wabuni sera ya pamoja kuhusu uhamiaji.

Mwandishi: Lubega Emmanuel, DW - Kampala

Mhariri: Iddi Ssessanga