1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Schalke yawika mbele ya Dortmund

Bruce Amani
16 Aprili 2018

Ulikuwa mtanange uliosubiriwa na wengi mwishoni mwa wiki na sio tu kwa sababu ya utani wa tangu jadi wa timu hizo mbili, bali pia katika harakati za kutafuta nafasi ya Champions League. Schalke ikaizaba BVB 2-0

https://p.dw.com/p/2w80L
1. Bundesliga 30. Spieltag | FC Schalke 04 - Borussia Dortmund | Jubel Schalke
Picha: Getty Images/Bongarts/A. Grimm

Schalke waliwazaba Borussia Dortmund mabao mawili na kujiimarisha katika nafasi ya pili ya msimamo wa Bundesliga. Hiyo bila shaka na hatua kubwa katika matumaini ya kupata tikiti ya moja kwa moja ya kucheza Champions League. Ushindi huo uliwapa nafasi ya kupumua kidogo maana sasa wana pengo la pointi nane kati yao na nambari tano RB Leipzig huku zikisalia mechi nne msimu kukamilika

kichapo hicho cha kwanza cha derby kwa Dprtmund tangu Septemba 2014 kimeiteremsha timu hiyo katika nafasi ya nne, nyuma ya Bayer Leverkusen na tofauti ya mabao. BVB iko nyuma ya Schalke na pengo la pointi nne na nne mbele ya Leipzig ambao walitoka sare ya bao moja kwa moja na Werder Bremen katika mechi nyingine ya jana.

Bundesliga / 30. Spieltag/ Tedesco in einer Traube aus Fans
Tedesco alisherehekea ushindi na mashabiki wa SchalkePicha: picture-alliance/AP Photo/M. Meissner

Katika mechi za Jumamosi, mabingwa wa Bundesliga Bayern Munich ambayo inawinda mataji matatu msimu huu waliwacharaza Borussia Moenchengadbach mabao 5 – 1.

Baada ya kutwaa ubingwa wa ligi wikendi iliyopita na kujikatia tikiti ya nusu fainali ya Champions League, huu ulikuwa mchezo mwignine wa hali ya juu kutoka kwa Bayern, ambao watacheza nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Ujerumani – DFB Pokal dhidi ya Leverkusen kesho Jumanne. Uli Hoeness ni Rais wa Bayern "Isipokuwa tu dakika za kwanza kumi, lilikuwa ni burudani tosha maana walicheza vizuri sana. Kwetu sisi hasa ni vizuri kuwa tuna mechi kadhaa bila kujisihisi kuwa na shinikizo, kwa sababu shinikizo lenyewe litakuwa Jumanne"

Nico Kovac alisisitiza kuwa Eintracht Frankfurt haitatumia uteuzi wake wa kuwa kocha wa Bayern msimu ujao kama sababu ya kichapo chao cha 4-1 mikononi mwa Bayer Leverkusen. "Amini usiamini, hilo ni kawaida. Tulikuja Leverkusen leo ili kuondoka na kitu, lakini Leverkusen ni timu kubwa, na Leipzig walishuhudia hilo siku chache zilizopita. Tulijitahidi sana. Siwezi kuwalaumu vijana wangu leo. Leo, timu bora ilishinda. Nafsi yangu iko sawa tu kama tu ilivyokuwa kabla ya mechi hii na itakuwa sawa hata kesho".

Niko Kovac
Kocha wa Frankfurt Niko Kovac anaelekea BayernPicha: picture-alliance/dpa/P. Steffen

Kevin Volland aliimarisha nafasi yake ya kujumuishwa katika timu ya Joachim Loew itakayokwenda Urusi kwa ajili ya kutetea Kombe la Dunia, baada ya kuifungia Leverkusen hattrick.

Kichapo hicho kimewaweka Frankfurt katika nafasi ya sita, pointi tano nyuma ya nambari nne Leverkusen. Hanover 96 ilipata pointi dhidi ya Stuttagart baada ya kutoka sare ya 1-1.

Kwingineko, vilabu viwili vya mkiani Hamburg na Cologne vilipata kipigo na hivyo kusogea karibu na shoka la kushushwa ngazi. Cologne walifungwa 2-1 na Hertha Berlin wakati Hamburg ilizabwa 2-0 na Hoffenheim. Christian Titz ni kocha wa Hamburg "Hata kama kuna hatari kuwa Mainz wanaweza kupanda juu kwa kupata ushindi, bado tuna mechi nne zilizobaki. Na hizo ni pointi 12 na kwa kuwa hilo linawezekana, hatuwezi kukata tamaa".

Hatima ya Hamburg na Cologne huenda ikajulikana leo usiku. Kama Mainz, ya tatu kutoka mkiani, itaizaba nambari nne kutoka mkiani Freiburg leo, (wao pamoja na Freiburg na Wolfsburg) watakuwa na pengo la pointi nane mbele ya Hamburg na tisa mbele ya Cologne.

Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Josephat Charo