1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saudia na Misri katika vita dhidi ya IS

11 Aprili 2016

Mfalme wa Saudi Arabia, Salman Bin Abdulaziz al-Saud, leo amehitimisha ziara yake nchini Misri, ambapo amesaini mikataba ya mabilioni ya Dola, kama ishara inayoonyesha Saudia kumuunga mkono Rais Abdel Fattah al-Sisi.

https://p.dw.com/p/1ITLn
Abdel Fattah al-Sisi King Salman Saudi Arabien Kairo Ägypten
Picha: picture-alliance/dpa/Egyptian Presidency

Ziara hiyo ya siku tano ya Mfalme Salman imefanyika wakati ambapo Saudi Arabia inalenga kuiweka Misri chini ya uangalizi wake, na wakati bado ikiendelea kushughulikia migogoro kadhaa katika Mashariki ya Kati na kushindana na Iran kwa ajili ya ukuu wa kikanda.

Ziara hiyo pia inaangazia hatua ya Saudia kuiunga mkono Misri katika mapambano dhidi ya kundi la wapiganaji wa jihadi la Dola la Kiislamu-IS, ambalo limeendesha uasi wa kikatili katika Rasi ya Sinai, tangu alipoondolewa madarakani Mohammed Morsi mwaka 2013. Saudi Arabia ilikuwa inakitilia mashaka chama cha udugu wa Kiislamu cha Morsi.

Akilihutubia bunge la Misri, Mfalme Salman amesema watashirikiana kwa pamoja na Misri katika mapambano dhidi ya itikadi kali pamoja na vita dhidi ya ugaidi, ambapo ulimwengu wa mataifa ya Kiarabu umekuwa ukiathirika zaidi pamoja na kuteseka kutokana na wapiganaji wa jihadi.

Saudia yagundua umuhimu wa msimamo wa pamoja

''Saudi Arabia imegundua umuhimu wa kuwa na mawazo na msimamo wa pamoja mmoja wa kupata ufumbuzi wa vitendo kwenye tatizo hili. Muungano wa kijeshi wa nchi za kiarabu, umeanzishwa ili kupambana na ugaidi kwa kutoa elimu na kwa kutumia vyombo vya habari, vya kifedha na kwa kutumia vikosi vya kijeshi,'' alisema Mfalme Salman.

Mfalme Salman
Mfalme SalmanPicha: picture-alliance/dpa/Saudi Press Agency

Mfalme Salman na Rais Al-Sisi, wamesaini mikataba ya uwekezaji yenye thamani ya mabilioni ya Dola, ukiwemo wa kujenga daraja katika Bahari ya Shamu ambalo litaziunganisha Saudi Arabia na Misri. Aidha, Misri pia imekubali kutenga mipaka yake ya bahari na Saudi Arabia kwa kuvikabidhi rasmi visiwa viwili vya Tiran na Sanafir kwa Saudi Arabia. Visiwa hivyo vipo katika mlango wa Ghuba ya Aqaba.

Makubaliano hayo yalizusha hasira kutoka kwa wananchi wa Misri, huku maelfu wakiandika katika mtandao wa mawasiliano ya kijamii wa Twitter, wakimshutumu Al-Sisi kwa kuviuza visiwa hivyo. Kihistoria visiwa hivyo vilikuwa mali ya Saudi Arabia na vilikodishwa nchini Misri mwaka 1950.

Ama kwa upande mwingine, Misri imetangaza kuwa itaisaidia Saudia na wanajeshi wa nchi kavu iwapo itahitaji. Hata hivyo, wachambuzi wa kisiasa wanasema kutokana na ziara ya Salman, Misri sasa inatarajiwa kuiunga mkono zaidi Saudia, hasa linapokuja suala la Iran na Yemen.

Wakati huo huo, Mfalme Salman ametunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari na Chuo Kikuu cha Cairo, kutokana na shughuli zake za kipekee kwa Waarabu na Waislamu. Kwa mujibu wa chuo kikuu hicho, Mfalme Salman ni kiongozi wa dunia na nguzo ya msingi katika ushawishi mkubwa kwenye medani ya ulimwengu wa Kiarabu na kimataifa.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, AP
Mhariri: Iddi Ssessanga