1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saudia Arabia yaishambulia Yemen

Sylvia Mwehozi
17 Mei 2019

Iran imelaani mashambulizi ya angani yaliyofanywa na Saudi Arabia dhidi ya ngome zinazomilikiwa na waasi wa Kihouthi nchini Yemen kuwa ni uhalifu. 

https://p.dw.com/p/3IeUV
Jemen Sanaa Luftangriffe der Saudis
Picha: Reuters/M. al-Sayaghi

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran, Seyed Abbas Mousavi, ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa na makundi ya kutetea haki za binadamu kuchukuwa hatua kuzuia uhalifu huo kutotekelezwa tena kwa njia yoyote ile.

Kupitia ujumbe alioutuma kwa njia ya Telegramu, msemaji huyo alisema kuwa mataifa yanayoyasaidia makundi hayo pinzani nchini Yemen kwa kuyapa silaha na mabomu, yanapaswa kulaumiwa pia kwa uhalifu huo na kuchukuliwa hatua.

Hata hivyo, Mousavi hakujibu kuhusu madai kwamba Iran ilihusika katika mashambulizi ya waasi siku ya Jumanne dhidi ya maboma ya mafuta ya Saudia.

Mashambulizi hayo yalifuatia shambulizi la roketi lililofanywa na Wahouthi dhidi ya bomba la mafuta la Saudi Arabia na kusababisha kufungwa kwa mabomba makuu ya mafuta nchini Saudia. Saudi Arabia ilisema kuwa mashambulizi hayo yalifanywa kufuatia maagizo ya Iran.

Ramadan Islam Religion
Msichana aliyetoroka mapigano Taiz akimbilia SanaaPicha: Reuters/K. Abdullah

Shirika la madaktari wasiokuwa na mipaka lilisema kuwa takriban watu wanne waliuawa na wengine 48 kujeruhiwa katika mashambulizi yaliyofanywa na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia Arabia kwenye mji mkuu wa Yemen, Sanaa.

Afisi ya Umoja wa mataifa inayoshughulikia maswala ya kibinadamu OCHA ilisema  kuwa watoto watano waliuawa na watu 16 kujeruhiwa katika mashambulizi hayo.

Muungano huo uliingilia kati hali ya Yemen mnamo mwezi Machi 2015 wakati rais Abedrabbo Mansour Hadi alipokimbilia mafichoni nchini Saudia Arabia  baada ya waasi kutishia kuteka ngome yake ya mwisho Aden baada ya kuteka maeneo mengi ya nchi hiyo.

Kampeni ya mashambulizi ya angani dhidi ya ngome zinazoshikiliwa na waasi zimekuwa zikilaaniwa mara kwa mara na Umoja wa Mataifa na makundi ya kutetea haki za binadamu kwa sababu ya  idadi kubwa ya vifo vya raia.

VYANYZO: AFP/AP/ TATU KAREMA