1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sasa majirani hawahofii tena Muungano wa Ujerumani

30 Septemba 2010

Baada ya miaka 20 ya Muungano wa Ujerumani, hofu walizokuwa nazo mataifa jirani, ambayo yalipigana vita na nchi hii katika Vita vya Pili vya Dunia, sasa zimeondoka.

https://p.dw.com/p/PQXf
Sherehe ya Muungano wa Ujerumani mbele ya Ukuta wa Berlin.
Sherehe ya Muungano wa Ujerumani mbele ya Ukuta wa Berlin.Picha: picture alliance / dpa

Kansela wa zamani wa Ujerumani, Helmut Kohl, alikuwa na ndoto ya kuiona siku moja Ujerumani ikiungana tena. Lakini kwa majirani wa Ujerumani, kuanzia Uingereza hadi Ufaransa na Uholanzi, suali kubwa walilokuwa wakijiuliza ni ikiwa je, Ujerumani kubwa iliyoungana itakuwa ya amani na ya masikizano, itakayoweza kujiunga na Jumuiya ya Ulaya na Umoja wa Kujihami wa Nchi za Magharibi, NATO?

Kwa hakika, hilo ndilo lililokuwa lengo la Helmut Kohl, ambaye kila mara alisisitiza kwamba Ujerumani iliyoungana haitakwenda na uhasama wa zamani kwenye jamii ya watu wa Ulaya.

Kansela wa zamani wa Ujerumani, Helmut Kohl, ambaye anatajwa kuwa injini ya Muungano wa Ujerumani
Kansela wa zamani wa Ujerumani, Helmut Kohl, ambaye anatajwa kuwa injini ya Muungano wa UjerumaniPicha: dapd

"Ule uadui na Unazi kamwe hautaruhusiwa tena." Alisema kiongozi huyu anayetajwa kama injini ya Muungano wa Ujerumani.

Badala ya kuwa kichocheo cha mfarakano na machafuko, kama ambavyo majirani zake walikuwa wamekhofia, Ujerumani imekuwa kichocheo cha umoja na mshikamano wa Ulaya. Kwa muda wote, imekuwa ikipigania kumalizika kwa mgawanyiko wa jamii ya Ulaya.

Kwa mfano, katika siasa yake ya nje imejiwekea lengo la kuhakikisha kwamba, zile nchi za zamani za Kambi ya Mashariki na Balkan zinakuwa sehemu ya Umoja wa Ulaya na NATO.

Hili limewafanya majirani waliokuwa na wasiwasi, sasa wakiri kwamba Ujerumani hii ya sasa siyo kabisa ile waliyoifikiria. Alfred Grosser, mwandishi na mwanasiasa wa mjini Paris, anasema kwamba zile hisia mbaya dhidi ya Ujerumani zilizokuwepo Uingereza na Marekani sasa zimefutika. Badala yake, sasa kinachosikikana ni kauli tafauti. Wamarekani na Waingereza wanakiri kwamba Wajerumani ni marafiki wema na ambao walifanya uamuzi wa busara kuungana tena.

Lakini mashaka dhidi ya Wajerumani bado yapo miongoni mwa raia wa Poland. Mwandishi wa Poland, Andrzej Stausiuk, anasema kwamba raia wengi wa nchi hiyo wangependa kuja Ujerumani kutafuta fedha, lakini Ujerumani si mahala penye fursa hiyo.

Kansela wa zamani wa Ujerumani, Helmut Kohl, akishagiliwa na umma wa Wajerumani kwenye maadhimisho ya Muungano wa Ujerumani
Kansela wa zamani wa Ujerumani, Helmut Kohl, akishagiliwa na umma wa Wajerumani kwenye maadhimisho ya Muungano wa UjerumaniPicha: picture alliance/dpa

Jamhuri ya Chek nayo imekuwa na mashaka yake kwa Ujerumani kutokana na historia iliyopo baina ya nchi hizi mbili tangu nyakati za vita vya dunia. Asilimia 30 ya ardhi ya Chek inakaliwa na Wachek wenye asili ya Ujerumani, jambo ambalo liliwahi kuzua mtafaruku baina ya nchi mbili hizi. Hata hivyo, hivi sasa nchi zote mbili ni wanachama wa Umoja wa Ulaya na NATO.

Katika Umoja wa Ulaya, Ujerumani imekuwa ikishikilia urais wa Jumuiya hiyo unaokwenda kwa mzunguko na pia imekuwa ikichukuliwa kama kituo cha kujifunzia utamaduni, sanaa na siasa za Muungano ambazo sasa ni maarufu hapa Ujerumani.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Bernd Riegert

Mhariri: Josephat Charo