1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SAN DIEGO :Miale ya moto yaelekea eneo la kusini mwa California

25 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7Cl

Miale ya moto inaripotiwa kufika karibu na maelfu ya nyumba za wakazi wa eneo la kusini mwa California hata baada ya pepo kupungua kasi na viwango vya joto kushuka.Pepo hizo zilitarajiwa kupotea kabisa hii leo ili kuimarisha juhudi za wazima moto.

Mkasa wa moto katika jimbo la California nchini Marekani umeingia siku yake ya tano huku nyumba 1300 zikiteketea na watu yapata nusu milioni kulazimika kuyahama makazi yao.

Rais George Bush wa Marekani aliyetangaza mkasa huo kuwa janga anatarajiwa kuzuru eneo hilo hii leo akiandamana na gavana wa jimbo la California Arnold Schwarzenegger.

Shirika la kitaifa la kupambana na mikasa FEMA limepeleka maafisa wake alfu moja hususan kwenye maeneo yaliyoathirika zaidi katika wilaya ya San Diego.Kwa upande mwingine wataalam wa kuzima moto wanaeleza kuwa kupungua kasi kwa pepo za Santa Ana kumeleta faraja ila pepo za bahari huenda zikasababisha hatari.Moto huo ulianza mwishoni mwa juma lililopita na mpaka sasa kuteketeza eneo lililo na ukubwa wa takriban kilomita alfu mbili na sabini na mbili.Watu sita wanaripotiwa kupoteza maisha yao na wengine zaidi ya sabini kujeruhiwa wengi wao wazima moto.