Saakashvili ashinda uchaguzi wa rais nchini Georgia | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.01.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Saakashvili ashinda uchaguzi wa rais nchini Georgia

Rais Mikheil Saakashvili wa Georgia anayeungwa mkono na mataifa ya magaribi ameshinda uchaguzi wa rais wa nchi hiyo matokeo ambayo upinzani umekataa kuyatambuwa na kudai kufanyika kwa duru ya pili ya uchaguzi huo.

default

Rais Mikhail Saakashvili wa Georgia

Mkuu wa tume kuu ya uchaguzi nchini Georgia Levan Tarkhmnischvili amesema Saakashvili ameshinda kwa asilimia 52.8 wakati mpizani wake Levan Gatshentschiladse amejipatia asilimia 27. Kura zote zilikuwa zimehesabiwa isipokuwa kwa vituo vya kupigia kura 43 vilioko nje ya nchi hiyo kati ya jumla ya vituo 3,500.

Saakashvili ambaye ameitisha uchaguzi huo wa haraka hapo Jumamosi kufuatia gasia za mwezi wa Novemba alikuwa akihitaji kuvuka kiwango cha asilimia 50 kushinda uchaguzi huo wa rais.

Upinzani ambao tayari umedai kuwepo kwa udanganyifu mkubwa katika uchaguzi huo umeelezea mashaka yao mapya baada ya kutolewa kwa matokeo hayo ya uchaguzi kwa kusema kwamba matokeo yamekuwa yakicheleweshwa kutolewa kwa makusudi kwamba kwa siku nzima wamekuwa wakijaribu kumpatia Saakashvili asilimia hiyo hamsini.Umesema hauamini matokeo hayo na wanadai marudio ya uchaguzi huo.

David Unsupascwili ni kiongozi wa upande wa upinzani amesema tume ya uchaguzi imejaa hila kwamba wanachapisha matokeo ili kuonyesha kwamba serikali inashinda uchaguzi lakini tutaendelea na mapambano yetu na kutoka hapa tutaelekea mahkamani.

Tangazo la tume ya uchaguzi limeonekana kuwa la kushangaza sana kutokana na kuonyesha nusu ya matokeo yake yakiwasili katika kipindi kisichozidi saa moja baada ya matokeo kuzorota kuingia kwa masaa 24 baada ya kufungwa kwa vituo vya kupigia kura.

Na licha ya tangazo hilo tovuti rasmi ya uchaguzi ambayo ilikuwa na matokeo ya uchaguzi kila inapojulishwa iliendelea kuonyesha matokeo kwa kuzingatia vituo vya kupigia kura visivyozidi asilimia 50.

Hata hivyo Alcee Hastings mkuu wa uangalizi wa uchaguzi wa Shirika la Usalama na Ushirikiano Barani Ulayas OSCE maoni yake tafauti kabisa na mashaka ya upinzani ambapo anasema uchaguzi huu ni wa kwanza kuwa na ushindani wa dhati uchaguzi wa rais ambao umewawezesha watu wa Georgia kuelezea chaguo lao la kisiasa.

Wizara ya mambo ya nje ya Urusi imepinga kauli hiyo ya Hastings ambaye ni Mmarekani kwamba haina uhalisi.

Urusi inapinga vikali harakati za Saakashvili kuitowa Georgia kwenye ushawishi wa Urusi na kuijumuisha nchi hiyo kwenye Jumuiya ya Kujihami ya Mataifa ya Magaribi NATO na taasisi nyengine za mataifa ya magharibi.

Upizani kugoma kutambuwa matokeo hayo kunatishia ukosefu mpya wa utulivu kwa nchi ambayo inajitahidi kuondokana na udhibiti wa Urusi wa karne chungu nzima na kuingiza mageuzi ya mtindo wa mataifa ya magharibi.

Nina Budshanadse ni msemaji wa bunge la Georgia anasema wamefanya mageuzi mengi yalio makini na yenye machungu nchini na ni jambo la wazi kabisa na la kawaida kwamba kiwango cha kuungwa mkono ni kidogo kuliko ilivyokuwa miaka minne iliopita.Licha ya ukweli huu anafikiri ni jambo muhimu sana kwamba zaidi ya nusu ya watu wameonyesha kumuunga mkono Saakashvili na timu yao na kwa mageuzi yao ambayo ni muhimu kwa nchi hiyo.

Urusi imekuwa ikipinga mkondo wa Georgia wa kufuata mataifa ya magharibi kwa kuiwekea nchi hiyo vikwazo kadhaa vya kiuchumi na kuunga mkono waasi wanaodhibiti mikoa miwili inayotaka kujitenga ya Abkhazia na Ossetia ya Kusini.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com