1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya UNICEF kuhusu haki za watoto

Oumilkher Hamidou6 Oktoba 2009

Shirika la Umoja wa mataifa la UNICEF linahimiza haki za watoto zilindwe

https://p.dw.com/p/Jyyy
Kitambulisho cha shirika la Umoja wa mataifa linalowahudumia watotoPicha: AP

 Shirika la Umoja wa mataifa linalowahudumia watoto-UNICEF limechapisha ripoti inayozungumzia  maafa yanayowaathiri watoto kote ulimwenguni.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya shirika la Umoja wa mataifa linalowahudumia watoto UNICEF,mamilioni ya watoto-wasichana kwa wavulana wanageuka wahanga wa matumizi ya nguvu, uonevu na kugeuzwa wajakazi.Kwa namna hiyo watoto milioni 150 wenye umri wa chini ya miaka 15 wanalazimishwa kufanya kazi za sulubu kwa namna ambayo wanashindwa hata kupata wasaa wa kwenda shule.Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya shirika la Umoja wa mataifa la UNICEF iliyochapishwa hii leo.Kwa mujibu wa tarakimu,mnamo mwaka 2007 watoto milioni 51 walizaliwa kote ulimwenguni,bila ya kuandikishwa.Na kwa kuwa hawana vyeti vya kuzaliwa,watoto hao wanakosa kinga na kwa namna hiyo inakuwa rahisi kwao kuangukia mhanga wa makundi ya wanyonyaji.Kila msichana mmoja kati ya watatu katika nchi zinazoinukia anaolewa akiwa bado mtoto.

Shirika la Umoja wa mataifa linalowahudumia watoto linalalamika katika ripoti yake hiyo ya kwanza ya kina kuhusu kuvunjwa haki za watoto kote ulimwenguni,kwamba watoto wasiopungua milioni moja wamefungwa jela,zaidi ya nusu ya watoto hao bila ya kufikishwa mahakamani.Zaidi ya watoto wadogo milioni 18 wanaishi katika familia ambazo kutokana na sababu za vita au maafa ya kimaumbile,zimeyapa kisogo maskani yao.

Ripoti ya UNICEF inahisi wasichana ndio wanaodhulumiwa zaidi.Katika nchi zisizopungua 29 za dunia hii,wasichana wanalazimika kutahiriwa kwa sababu za kimila.Idadi ya wasichana wanaoolewa wakiwa bado wadogo inapindukia asili mia 70 katika nchi kama vile Niger,Tchad,na Mali na katika nchi mfano wa Bangladesch,Guinea na Jamhuri ya Afrika ya Kati,idadi ya wasichana wanaoolewa wakiwa bado wadogo inapindukia asili mia 60-kwa mujibu wa ripoti hiyo ya UNICEF.Hata hivyo ripoti hiyo inazungumzia dalili za matumaini mema:Katika nchi nyingi za Afrika idadi ya wasichana wanaotahiriwa inapungua.Katika nchi mfano wa Bangladesh, ambako mitindo ya watoto wadogo kulazimishwa kuolewa imeenea,umri wa msichana kuolewa umerefushwa kidogo.

"Jamii haiwezi kujiendeleza,ikiwa vijana wake wanalazimishwa kuolewa wakiwa bado wadogo,wakidhalilishwa kimwili na kupokonywa haki zao za kimsingi" amesema hayo mkurugenzi wa shirika la UNICEF Ann Veneman.Shirika la Umoja wa mataifa linalowahudumia watoto limetaja hatua tano muhimu ili kuweza kuwahifadhi kwa uzuri zaidi watoto,miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kinga maafa yanapotokea,ushirikiano imara kati ya serikali na kuhifadhiwa data.Kwa mujibu wa UNICEF ripoti kuhusu kinga ya watoto ina maelezo kutoka takriban nchi zote za dunia.

Mwandishi:Oummilkheir Hamidou/AFP/AP

Mhariri:Abdul-Rahman