1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya umoja wa mataifa kuhusu biashara na teknolojia

19 Julai 2007

Ripoti ya mwaka kuhusu umasikini, biashara na maendeleo katika nchi masikini imetolewa baada ya kumalizika mkutano wa shirika la UNCTAD la umoja wa mataifa. Mkutano huo ulituwama zaidi katika maswala ya maendeleo na teknolojia katika nchi masikini.

https://p.dw.com/p/CHk8
Baraza kuu la Umoja wa Mataifa
Baraza kuu la Umoja wa MataifaPicha: AP

Ripoti hiyo ya umoja wa mataifa ya mwaka huu imelenga zaidi maendeleo ya kiteknolojia katika nchi masikini.

Nchi masikini zaidi duniani zinahitaji ufahamu wa teknolojia ili kupata maendeleo hivyo basi ripoti hiyo imependekeza kwamba wafadhili wahamishe misaada yao na kuielekeza katika maswala ya sayansi na utafiti.

Mkutano wa shirika la umoja wa mataifa UNCTAD uliomalizika mjini Geneva, Uswisi na kutoa ripoti hiyo umependekeza zaidi kuwa wafadhili wa kimataifa waongeze misaada yao ili kuboresha sekta za teknolojia na mafunzo hasa kwa nchi ambazo uchumi wake ni hafifu ili nchi hizo zijikwamue kutoka kwenye tatizo la malimbikizo ya malighafi na wafanyakazi wasio na ujuzi wa kutosha katika uzalishaji.

Ripoti hiyo ya umoja wa mataifa ya mwaka 2007 imezilenga nchi ambazo hazijaendelea, imesema kwamba mbinu mpya za kilimo zitakazo ongeza mazao na ubora zinahitajika zaidi katika nchi masikini za barani Afrika, Latin Amerika na Asia ambako idadi kubwa ya wakulima kila kukicha wanahama sehemu za mashambani na kuelekea mijini.

Kwa mujibu wa shirika la UNCTAD kiwango cha chini ya asilimia nne tu cha mikopo ya benki ya dunia ndio kimetumiwa katika sekta za miradi ya sayansi na teknolojia katika kipindi cha miaka 25.

Katibu mkuu wa UNCTAD Supachai Panitchpakdi amesema hakuna uwiyano katika maswala ya utawala, maswala ya kijamii na yale ya kiteknolojia.

Ametoa mfano kwamba nchi masikini katika bara Asia kama vile Bangladesh, Laos, Nepal na Cambodia ikiwa ndio kwanza zinaanza kupiga hatua katika maswala ya kiteknolojia nchi nyingi za Afrika nazo zinazidi kudidimia.

Nchi masikini zaidi barani Afrika zinakwama kutokana na kuwekeza zaidi katika viwanda vya uzalishaji mali asili.

Bwana Panitchpakdi amesema kuwa nchi hizo zinahitaji kuanzisha mbinu zitakazo imarisha sekta za madini na nishati ili kukuza uchumi wao.

Rais wa baraza kuu la umoja wa mataifa Sheikha Haya Rashed Al Khalifa amesema kuwa nchi masikini zaidi duniani hazijafaidika vilivyo kutokana na utandawazi isipokuwa nchi hizo zimepata mateso mengi kufuatia maamuzi ya utandawazi.

Bibi Khalifa aliutaja msemo wa kiongozi maarufu wa zamani wa India Mahatma Ghandi kwamba katika maeneo yanayokabiliwa na umasikini mkubwa watu wanamuona Mwenyezi Mungu katika kipande cha mkate, na usemi huo bado unadhihirika hata baada ya miongo kadhaa.

Makamu waziri mkuu wa Uturuki ambae pia ni waziri wa mambo ya nje Abdullah Gul ametangza kuanzishwa mfuko maalum wa dola milioni 20 za kusaidia miradi ya ya maendeleo katika nchi masikini zisizokuwa na bandari na pia nchi ambazo ni visiwa vidogo.