1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

RIPOTI YA OECD JUU YA MATUMAINI YA USTAWI WA UCHUMI:

Abdu Said Mtullya26 Mei 2010

Shirika la OECD latoa matumaini ya kustawi kwa uchumi katika nchi za Ulaya.

https://p.dw.com/p/NY0X
Kansela Merkel wa Ujerumani na katibu Mkuu wa shirika la OECD Angel Gurria pamoja na waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble.Picha: AP

Shirika la Ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo, OECD, limesema katika ripoti yake kwamba ustawi wa uchumi katika nchi za ukanda wa sarafu ya Euro utafikia asilimia 1.2 mnamo mwaka huu, tofauti na utabiri wa hapo awali.

Hata hivyo, shirika hilo limezitaka nchi za ukanda huo zikabiliane na matatizo ya bajeti yanayoweza kuzorotesha mchakato huo wa ustawi.

Katika ripoti yake iliyotoa mjini Paris leo, shirika la OECD, limeonyesha matumaini kutokana na utabiri unaoashiria kwamba pato la jumla la taifa la nchi 16 zinazotumia sarafu ya Euro litastawi kwa asilimia 1.2 mnamo mwaka huu na asilimia 1.8.mwaka ujao.

Shirika hilo limetilia maanani katika ripoti yake kwamba uchumi unaanza kustawi tena hatua kwa hatua katika nchi za ukanda wa Sarafu ya Euro kufuatia hatua za kuufufua uchumi zilizotekelezwa na nchi hizo na kutokana na kukua tena kwa biashara ya dunia.

Hali nzuri katika sekta ya fedha,pia imechangia katika ustawi huo,ingawa pamekuwapo na hali ya kuyumba yumba katika sekta ya mabenki.

Hata hivyo,shirika la OECD limetahadharisha kwamba kurejea kwa hali nzuri kunaweza kutatizwa na hatua za kujaribu kurejesha nguvu ya ushindani na kutokana na udhaifu katika nchi zisizokuwa na nguvu kubwa kiuchumi katika eneo hilo.

Katika ripoti yake ya nusu mwaka,shirika hilo limesema ingawa kustawi tena kwa uchumi wa Ujerumani,kimsingi,kumekuwa imara,ustawi huo utaanza kuwa madhubuti katika nusu ya pili, kadri mauzo ya nje yatakavyonufaika na kustawi tena kwa biashara ya dunia.

Hata hivyo,nchi za ukanda wa Euro zinatakiwa ziendelee na mageuzi.

Lakini kwa jumla,uchumi utafikia asilimia 0.1 badala ya asilimia 1.5 kama ilivyokuwa mwaka jana, na baadae utastawi kwa asilimia 0.6 katika mwaka ujao.

Na licha ya udhaifu wa muda,kimsingi ustawi ni imara, na unaashiria ukuaji madhubuti katika siku za usoni.

Ustawi nchini Ufaransa ,yaani nchi inayoshika nafasi ya pili katika nguvu za uchumi baada ya Ujerumani,barani Ulaya, uchumi utakua kwa asilimia 2 mnamo mwaka huu na katika mwa ujao.

Mwandishi: Abdu Mtullya/AFPE

Mhariri: Miraji Othman