1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya mwaka ya halmashauri kuu ya Umoja wa mataifa inayowahudhumia wakimbizi

Oumilkher Hamidou15 Juni 2010

Ukosefu wa usalama unafanya iwe shida kwa wakimbizi kurejea nyumbani-anasema mkuu wa halmashauri kuu ya Umoja wa mataifa inayowahudumia wakimbizi-UNHCR

https://p.dw.com/p/NrZB
Wakimbizi mashariki ya jamhuri ya kidemokrasi ya KongoPicha: Ute Schaeffer

Idadi ya wakimbizi walioshindwa kurejea makwao kwa sababu za usalama imeongezeka mwaka 2009. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya mwaka ya halmashauri kuu ya Umoja wa mataifa inayowashughulikia wakimbizi-UNHCR- iliyotangazwa hii leo mjini Geneva.

Wakimbizi laki mbili na 51 elfu tuu kati ya milioni 15 walioko katika kila pembe ya dunia ndiyo walioweza kurejea nyumbani mwaka jana. Hiyo ni idadi ndogo kabisa kuwahi kushuhudiwa tangu miaka 20 iliyopita.

Mizozo nchini Afghanistan, Somalia na katika Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo imepelekea wakimbizi kadhaa wa nchi hizo washindwe kurejea mwakao-amesema mkuu wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Mataifa inayowashughulikia waakimbizi, Antonio Guterres.

Mizozo mengine iliyodhihirika kana kwamba imeanza kupungua makali, mfano nchini Iraq na kusini mwa Sudan haikumalizika kama ilivyokua ikitarajiwa, na watu walioyapa kisogo maskani yao wameshindwa kurejea nyumbani-amesema bwana Guterres katika taarifa yake iliyochapishwa wakati mmoja na ripoti ya mwaka ya Halmashauri kuu ya Umoja wa Mataifa inayowashughulikia wakimbizi-UNHCR.

"Wakimbizi wanaoishi uhamishoni tangu miaka mitano iliyopita ndio kundi kubwa la wakimbizi ulimwenguni. Idadi hiyo itaongezeka tuu ikiwa idadi ya wanaorejea makwao itaendelea kupungua"-amesisitiza waziri mkuu huyo wa zamani wa Ureno.

Kwa jumla, wakimbizi milioni moja hurejea nyumbani kwa hiari kila mwaka-ripoti ya UNHCR imesema.

Taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa inatofautisha wakimbizi ambao hawaishi tena katika nchi zao za jadi, na wale waliolazimika kuyapa kisogo maskani yao na kubakia wakiranda randa ndani nchini mwao.

Idadi ya wakimbizi haijaongezeka mwaka jana,wamesalia kuwa watu milioni 15 na laki mbili.Kwa mujibu wa ripoti ya halmashauri kuu ya Umoja wa mataifa inayowahudumia wakimbizi, takriban asili mia 80 ya wakimbizi hao wanaishi katika nchi zinazoinukia. Pakistan inasemekana imewapokea wakimbizi milioni moja na laki sabaa na kufuatiwa na Iran na Syria ambazo kila moja imewakaribisha wakimbizi milioni moja na elfu tano.

Idadi ya wanaoomba kinga ya ukimbizi pia imeongezeka mwaka jana. Afrika kusini imepokea maombi mengi zaidi ya aina hiyo, ikifuatiwa na Marekani na Ufaransa.

Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, wakimbizi wasiopungua milioni moja na laki tatu wamepatiwa uraia wa kigeni, na zaidi ya nusu ya wakimbizi hao wamepatiwa uraia wa Marekani.

Mwandishi: Ummil Hamidou/Reuters/AFP/DPA

Imepitiwa na: Miraji Othman