1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti juu ya idadi ya watu duniani

Maja Dreyer14 Machi 2007

Idadi ya watu duniani inazidi kuongezeka kwa haraka – haya ni kulingana na ripoti mpya iliyotolewa na Umoja wa Mataifa. Ripoti hii inasema kuwa ifikapo mwaka 2050 kutakuwepo watu Billioni 9,2 duniani, yaani Billioni 2,5 zaidi kuliko leo.

https://p.dw.com/p/CHlT
Barani Afrika ongezeko la watu ni kubwa zaidi
Barani Afrika ongezeko la watu ni kubwa zaidiPicha: dpa

Kila mwaka idadi ya watu duniani inazidi kwa Millioni 78. Lakini katika siku za usoni ukuaji wa idadi ya watu utatokea hasa katika nchi zinazoendelea, wakati idadi ya wananchi wa mataifa ya kiviwanda itabaki vile vile.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya wakazi inatarajia idadi ya watu duniani kukuwa zaidi kuliko miaka miwili iliyopita. Wakati nchi fulani zinazoendelea zilikuwa na ongezeko dogo la wananchi, idadi ya watoto waliozaliwa katika nchi nyingine ilikuwa kubwa sana.

Bi Catherina Hinz wa wakfu wa Ujerumani wa masuala ya makazi duniani amesema: “Hasa katika nchi maskini ambapo mahitaji ya msingi ya watu hayapatikani, ndiko watoto wengi wanapozaliwa. Katika nchi 50 maskini zaidi duniani, idadi ya wananchi itakuwa mara mbili ifikapo kati kati ya karne hii, yaani kutoka watu millioni 800 hadi watu Billioni 1,7. Kwa hivyo katika nchi nyingi zinazoendelea mzigo katika mfumo wa afya na elimu na pia kuhusiana na hali ya chakula utakuwa mzito sana.”

Kuna nchi kadhaa zinazoendelea ambako idadi ya watoto wanaozaliwa inapungua kama Costa Rica, Thailand na Tunesia. Katika nchi nyingine idadi ya watoto ambao huzaliwa na mwanamke mmoja haijaongezeka mfano Ghana, Kenia na Indonsia. Halafu kuna kundi la tatu na mataifa ambapo idadi ya watoto wanaozaliwa haijapungua kama Niger, Nigeria na Uganda. Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya wakazi inatarajia lakini kuwa idadi ya watoto wanaozaliwa na mke mmoja katika nchi zinazoendelea itapungua kuwa wawili kwa wastani ifikapo mwaka 2050.

Lakini kwa kuwa hasa ni idadi ya vijana ndiyo inayokua kwa haraka, nchi kadhaa zitakuwa na ongezeko la mara tatu zaidi kuliko leo kama kwa mfano nchini Uganda na katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Ndiyo sababu, wakfu wa wakazi inasisitiza umuhimu wa kuwepo mkakati wa kuongeza ujuzi juu ya uzazi wa mpangilio. Ni Catherine Hinz: “Wafadhili wengi wanatambua kuwa ni tatizo kubwa kweli kwa nchi kama Uganda na wameanzisha miradi inayolenga kuchelewesha kuongezeka idadi ya wananchi, yaani kwa mfano uzazi wa mpangilio, elimu na hudumu za afya, yaani siyo tu kupanga familia bali pia huduma kwa waja wazito na wakati wa kujifungua. Lengo ni kuunganisha masuala haya katika mkakati wa kuezindeleza nchi hizi.”

Kulingana na Bibi Hinz, barani Afrika kila mwaka Dola Millioni 70 zinahitajika kwa mkakati huo wa uzazi wa mpangilio kwa sababu kuna uhaba mkubwa wa mbizu za kujikinga kushika mimba.

Ulaya ni eneo la pekee duniani ambako idadi ya wananchi itapungua. Kwa mujibu wa ripoti hii ya Umoja wa Mataifa, idadi ya wananchi itapungua kwa millioni 67 hadi mwaka 2050 kwa sababu wanawake wa Ulaya wanazaa watoto wachache sana.