1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rice tena Mashariki ya Kati

Jane Nýingi4 Oktoba 2007

Waziri wa mambo ya nje wa marekani bi Condoleza Rice anatarajiwa kusafiri mashariki ya kati wiki ijayo kwa matayarisho ya mkutano mkubwa wa kimataifa unaolenga kujadili mikakati ya kutatua mzozo kati ya israel na palestina. Kabla ya kuwasili mashariki ya kati bi Rice kwanza atapitia Urussi.

https://p.dw.com/p/C7ie
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi.Condoleza Rice akishauriana na Rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi.Condoleza Rice akishauriana na Rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud AbbasPicha: AP

Tangazo hilo la safari ya Rice katika eneo la mashariki ya kati linawadia baada ya viongozi wa Palestina na Israel kufanya mashauri mapya mjini Jerusaleum, mashauri ambayo kwa mara kwanza yalinuia kutatua tofauti zao kabla ya mkutano huo mkuu unaodhaminiwa na marekani. Hii itakuwa ziara ya saba ya Bi Rice katika eneo hilo mwaka huu.

Msemaji wa ikulu ya marekani Sean Mccormack amewaambia wanahabari kuwa, Rice kwanza atapitia mjini Moscow, Urussi, ambapo ataungana na waziri mwenzake wa ulinzi Robert Gates kwa mashauri ya ana kwa ana na mawaziri wenzao wa urussi.

Mkutano huo wa tarehe 12 wiki ijayo unawadia wakati ambapo mvutano umeshika kasi kuhusu hatua ya marekani kuweka mtambo wa kudengua makombora katika europa ya kati.

Mccormack amesema Bi Rice punde baada ya kuondoka Moscow atatembelea miji kadhaa katika eneo la mashariki ya kati ili kutengeza mazingira mazuri tayari kwa mkutano huo wa mkuu wa kimataifa wa amani.

Huu ni mkutano wa nne chini ya miezi miwili kati ya Waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert na rais wa Palestina Mahmoud Abbas.Wakati wa mkutano huo waliandaa taarifa ya pamoja itakayowezesha kupatikana kwa mwafaka kati ya mataifa hayo hasimu.

Mpatanishi wa mgogoro huo ,upande wa palestina Saeb Erakat amesema kuwa kufuatia mkutano huo wa Jerusaleum waziri mkuu Ehud olmert na Rais wa mamlaka ya Palestina.

Mahmound Abbas wamewataka kuanza kuandaa taarifa ya pamoja kwa kuzingatia maswala muhimu kwa lengo la kuyawasilisha katika mkutano wa Washington mwezi ujao.Hata hivyo afisa mkuu wa Israel katika mkutano na wanahabari alisema kuwa taarifa hiyo ya pamoja itakuwa si kamili kutokana na muda mfupi waliopewa wakuiandaa.

Pande zote mbili zina maoni tofauti kuhusu maswala yanayopasa kuafikia kabla ya mkutano huo wa Novermber. Mamlaka ya palestina imekuwa ikisisitiza kuzingatiwa kwa baadhi ya mambo kwanza,kuachiliwa huru kwa wafungwa,swala la wakimbizi, mipaka na kuhusu mji wa Jerusaleum.

Taarifa nyingine ni kuwa waliokuwa maafisa katika wizara ya ulinzi nchini marekani wamependekeza mji mkuu wa palestina na israel uwe jerusaleum. Hata hivyo wametaka kutoruhusiwa kwa wakimbizi wa kiarabu kurejea Israel miongoni mwa mapendekezo yaliyoko taarifa inayonuia kusuluhisha mgogoro wa miaka mingi kati ya waisrael na wapalestina.

Katika taarifa yao ya kurasa sita waliyomkabidhi waziri wa mambo ya nje wa marekani bi Condoleza Rice walipendekeza kufanywa kwa misururu ya mikutano ya amani baaada ya mkutatano huo mkubwa wa kimataifa wa amani katika mashariki ya kati mwezi ujao.

Kundi la wapiganaji la hamas ambalo linasimamia eneo la gaza na karibu thuluthi moja ya mamlaka ya Palestina halijatimiza masharti yaliyotolewa ma marekani ya kuhudhuria mkutano huo.Baadi ya masharti hayo ni kulitambua taifa la Israel na kukomesha mashambulizi dhidi yao.

Hata hivyo maafisa hao wa zamani wa ulinzi wa Marekani wamesema jukumu la kundi la hamas katika kutafuta amani ya kudumu mashariki ya kati ni muhimu.Mji wa Jerusalem na swala wa wakimbizi limetatiza juhudi za hapo awali za Marekani za kusaka amani mashariki ya kati.