1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ramaphosa ataka kampuni ya marafiki wa Zuma ichunguzwe

19 Januari 2018

Cyril Ramaphosa amewataka waendesha mashitaka kuchukua hatua za haraka kuifuatilia kampuni inayomilikiwa na marafiki wa rais Jacob Zuma

https://p.dw.com/p/2r8qe
Südafrika Cyril Ramaphosa in Johannesburg
Picha: picture-alliance/Photoshot

Makamu wa rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amewataka waendesha mashitaka kuchukua hatua za haraka kuifuatilia kampuni inayomilikiwa na marafiki wa rais Jacob Zuma anayekabiliwa na kashfa kadhaa, wakati ambapo kunaongezeka na shinikizo dhidi ya kiongozi huyo la kumtaka aachie madaraka.

Ramaphosa alichukua nafasi ya Zuma kama kiongozi wa chama tawala nchini humo cha African National Congress, ANC mwezi uliopita, na sasa anapewa nafasi kubwa zaidi ya kuwa rais ajaye katika uchaguzi utakaofanyika mwaka 2019, ama hata kabla ya hapo, iwapo Zuma ataamua kujiuzulu.

Katika siku za hivi karibuni, ameanza kutoa matamshi  dhidi ya makampuni yaliyo chini ya familia ya kitajiri ya Gupta na wafanyabiashara ambao ni marafiki wa karibu wa Zuma ambao kwa pamoja wanatuhumiwa kutumia uhusiano wa kisiasa ili kushinda zabuni za serikali.

Sarafu ya Randi ya Afrika Kusini imepanda kwa haraka kwa takriban asilimia 16 tangu Ramaphosa aliposhinda kinyangayiro cha kuiongoza ANC, kutokana na ahadi yake kwa wawekezaji kwamba atachukua hatua kali dhidi ya ufisadi na kutekeleza mageuzi ya kisera.

Familia tajiri ya Gupta imedaiwa kuwa na ushawishi katika serikali ya Zuma kufuatia urafiki wao na rais
Familia tajiri ya Gupta imedaiwa kuwa na ushawishi katika serikali ya Zuma kufuatia urafiki wao na raisPicha: Imago

Zuma na Gupta huyakana madai dhidi yao

Familia ya Gupta na Zuma hata hivyo, wamekanusha kwamba wana makosa yoyote na kusema wao ni wahanga wanaolengwa katika kampeni zinazochochewa kisiasa. Msemaji wa Zuma na mwanasheria wa familia ya Gupta hawakuzungumzia chochote, walipotakiwa kufanya hivyo jana Alhamisi. 

Zuma mwenyewe amekuwa akikana madai ya rushwa yanayomkabili tangu alipoingia madarakanii mwaka 2009, na wiki iliyopita alisema ataunda tume ya uchunguzi, dhidi ya madai hayo ya kutumia ushawishi kuingilia masuala ya serikali.

Pamoja na hayo  katibu mkuu wa ANC Ace Magashule amesema Kuondolewa kwa Zuma kama kiongozi wa taifa hilo, sio miongoni mwa ajenda za mkutano wa siku nne wa kamati kuu mpya ya chama cha ANC ulioanza hapo jana.

Uvumi wa shinikizo la ANC kumtaka Zuma aondoke madarakani

Zuma amekabiliwa na madai ya kashfa mbalimbali
Zuma amekabiliwa na madai ya kashfa mbalimbaliPicha: Getty Images/AFP/M. Safodien

Kumesambaa uvumi kwamba wapinzani wa Zuma ambao ni miongoni mwa wajumbe wapya 80 waliochaguliwa katika kamati kuu ya chama wataibua upya shinikizo la kutaka Zuma kuondoka madarakani katika mkutano huo wa siku nne, ambao pamoja na mambo mengine, Ramaphosa atachukua rasmi uongozi wa chama.

Katika uchaguzi wa Kiongozi wa chama tawala cha African National Congress uliofanyika mwezi uliopita, Ramaphosa alimpiku mke wa zamani wa Zuma na ambaye alikuwa chaguo la Zuma, Nkosazana Dlamini-Zuma. Wachambuzi wanasema Ramaphosa anatarajiwa kurudisha  imani ya wanachama wengi wa ANC, waliovunjwa moyo na Uongozi wa Zuma  kutokana na kashfa chungu nzima za rushwa zinazomkabili pamoja na serikali yake kushindwa kutimiza ahadi zake, ikiwa ni pamoja na kuunda nafasi za ajira, kuhakikisha elimu  na afya bora pamoja na makaazi.

Mwandishi: Lilian Mtono.

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman