1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ramallah: Marekani yaahidi itatoa dola milioni 80 kusaidia usalama wa Palestina.

2 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBcl

Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas na Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi Condoleezza Rice wametia saini mwafaka wa dola milioni themanini kuvisaidia vikosi vya usalama vya Wapalestina.

Bi Condoleezza Rice pia amesema Israil iko tayari kujadili maswala makuu yanayohusu kuundwa taifa huru la Wapalestina.

Bi Condoleezza Rice amesema:

"Nimekuja mara hii kuifuatilia mikakati aliyoitangaza Rais Bush tarehe kumi na sita mwezi uliopita kuhusu suala la kuanzishwa mataifa mwili huru yanayoishi kwa amani. Sote tunaridhishwa na uongozi wa Rais Mahmoud Abbas na pia serikali yake inayoongozwa na Salaam Fayadd. Bila shaka tuna nia ya dhati kusaidia kutekelezwa mpango huo"

Waziri huyo wa Marekani wa mambo ya nje alitangaza hayo baada ya kushauriana na Rais Mahmoud Abbas na waziri wa mambo ya nje wa Israil Tzipi Livni.

Katika ziara yake ya siku nne katika eneo hilo la Mashariki ya Kati, Bi Condoleezza Rice amekuwa akizungumzia na kutetea kikao cha kimataifa cha amani kilichopangwa kuandaliwa katika eneo hilo kabla ya mwisho wa mwaka.

Saudi Arabia imesema iko tayari kuhudhuria kikao hicho.