1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rajoy hatarini kuondolewa madarakani Uhispania

Caro Robi
31 Mei 2018

Waziri mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy anakabiliwa na kura ya kutokuwa na imani naye bungeni baada ya wanasiasa wa upinzani wa chama cha kisoshalisti kuwasilisha hoja ya kufanyika kura hiyo.

https://p.dw.com/p/2yixv
Spanien | Parlamentsdebatte zum Misstrauensvotum gegen Ministerpraäsident Rajoy | Mariano Rajoy
Picha: Reuters/S. Perez

 Huku wabunge wakianza mjadala mkali bungeni kumhusu waziri mkuu Mariano Rajoy kuelekea kura hiyo ya kutokuwa na imani naye hapo kesho, kiongozi wa Kisoshalisti Pedro Sanchez amesema Rajoy amepoteza hadhi yake baada ya wiki iliyopita kufichuliwa kashfa ya mfumo mpana wa viongozi wa chama chake cha  PP kupokea rushwa ili watoe kandarasi kubwa za umma.

Sanchez amemueleza Rajoy kuwa kuendelea kusalia kwake madarakani kama waziri mkuu kuna madhara na ni mzigo sio kwa Uhispania tu, bali pia kwa chama chake akiongeza hawezi kulilazimisha taifa kuchagua kati ya ufisadi na uthabiti kwasababu hakuna msukosuko mkubwa kama ule unaosababishwa na ufisadi.

Je, Wasosholisti wataweza kumuondoa Rajoy?

Sanchez anaonekana kuwa karibu kupata uungwaji mkono mkubwa bungeni ili kura hiyo ya kutokuwa na imani na Rajoy iweze kupita bungeni. Wabunge 176 wanahitaji kuunga mkono Rajoy kuondolewa madarakani.

Spanien | Parlamentsdebatte zum Misstrauensvotum gegen Ministerpraäsident Rajoy | Pablo Sanchez
Kiongozi wa chama cha Kisosholisti Pedro SanchezPicha: Getty Images/P. Blazques Dominguez

Waziri huyo mkuu wa Uhispania anayeongoza serikali ya walio wachache alichaguliwa tena mwaka 2016. Sanchez ameahidi kuitisha uchaguzi mpya katika kipindi cha miezi michache ijayo iwapo hoja yake itafanikiwa bungeni.

Chama cha Kisoshalisti kina viti 84 katika bunge la Uhispania lenye idadi jumla ya viti 350. Tayari kimepata uungwaji mkono kutoka chama cha mrengo wa kushoto kinachopinga kubana matumizi cha Podemos ambacho kina wabunge 67.

Na kwa uungwaji mkono kutoka kwa vyama vidogo vya majimboni vikiwemo viwili vya jimbo la Catalonia linalotaka kujitenga na kujitawala, huenda hoja ya chama cha Kisosholisti ikaungwa mkono na wabunge 175, ikipungukiwa na kura moja tu kupata idadi inayohitajikwa kwa kura hiyo kupitishwa bungeni.

Chama cha Basque Nationalist Party PNV kilicho na wabunge watano ambacho kinatawala katika jimbo la Basque kwa ushirikiano na chama cha  Kisoshalisti lakini kilimuunga mkono Rajoy kupitisha bajeti ya mwaka 2018, kimesema kitampinga Rajoy katika kura hiyo ya kutokuwa na imani naye, na hivyo kumaanisha uwezekano wa Rajoy kuondolewa madarakani sasa ni mkubwa mno.

Wiki iliyopita, mahakama kuu inayoshughulikia kesi kubwa za kihalifu iliyoko mjini Madrid, ilisema imegundua mfumo mpana wa rushwa zilizotolewa kwa maafisa wa zamani wa chama cha PP ili watoe kandarasi kati ya mwaka 1999 na 2005.

Maafisa wa PP washitakiwa kwa ufisadi

Mahakama hiyo iliwahukumu kifungo cha gerezani, watu 29 walio na mafungamano na chama hicho tawala akiwemo mweka hazina wa zamani na kukiagiza chama cha PP kurejesha euro 245,000 ambazo kilipokea kutoka kwa mfumo huo kukisaidia katika kampeini za uchaguzi.

Spanien |  Debatte über Abwahl von Rajoy
Wabunge wa Uhispania wakiwa bungeni kujadili kura dhidi ya RajoyPicha: imago/Agencia EFE/J. C. Hidalgo

Mariano Rajoy aliye madarakani tangu 2011, anakuwa waziri mkuu wa kwanza wa Uhispani aliye madarakani kutoa ushahidi katika kesi hiyo ambapo aliitwa kama shahidi na hivyo kuchochea wito wa kumtaka ajiuzulu.

Katika hukumu iliyotoa, mahakama hiyo ya Madrid ilisema ushahidi alioutoa kiongozi huyo ni wa kutiliwa mashaka. Rajoy amekanusha kuwa na ufahamu wa chama chake cha Popular Party PP kupokea ufadhili wa kifedha kwa njia zisizo sahihi.

Katika kikao cha bunge leo, Rajoy amesema kesi hiyo haiwahusishi maafisa wa serikali akisisitiza ni wanasiasa wachache tu waliotuhumiwa kwa madai hayo ya ufisadi, na kuongeza chama cha PP kina watu wafisadi lakini chenyewe sicho na kumshutumu mpinzani wake Sanchez kwa kutaka kutumia kashfa hiyo kujinufaisha kisiasa.

Wachambuzi wanasema Rajoy, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2011, atadhoofishwa kisiasa iwapo kura hiyo itafeli bungeni , huku vyama vya upinzani vikitarajiwa kuendelea na azma yao ya kumuondoa madarakani.

Mwandishi: Caro Robi/afp/ap

Mhariri:Yusuf Saumu