1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Xi Jinping wa China afanya ziara Ufaransa

Abdu Said Mtullya26 Machi 2014

China na Ufaransa zinatarajiwa kufikia mapatano kadhaa ya biashara katika siku ya kwanza ya ziara ya kiserikali ya Rais Xi Jinping nchini Ufaransa.Jee ziara ya Rais wa China inafanyika wakati mwafaka kwa Ufaransa?

https://p.dw.com/p/1BVqY
Rais Xi Jinping wa China afanya ziara Ufaransa
Rais Xi Jinping wa China afanya ziara UfaransaPicha: Reuters

Ufaransa ipo nyuma ya jirani zake wa Ulaya , na hasa Ujerumani katika biashara na vitega uchumi inapohusu uhusiano wake na China.

Hata hivyo Ufaransa imefanya bidii katika kuziba pengo katika sekta za usafirishaji wa angani, nyuklia, kilimo na maendeleo ya miji.

China kununua ndege aina ya Airbus

Mapatano baina yake na China pia yanatarijiwa kutiwa saini katika sekta hizo wakati wa ziara ya siku tatu ya kiserikali ya Rais Xi Jinping nchini Ufaransa. Ufaransa inatarajiwa kunufaika hasa kutokana na makubaliano itakayoyafikia juu ya kuiuzia China ndege.

Wakati wa ziara yake ya China mwaka uliopita Rais Francois Hollande wa Ufaransa alipewa ahadi na mwenyeji wake Rais Xi Jinping kwamba China inadhamiria kununua ndege 60 aina ya Airbus. Rais Xi Jinping amesema ziara yake nchini Ufaransa itampa fursa ya kushirikiana na mwenyeji wake Rais Hollande katika kutathmini kwa pamoja hatua iliyopigwa katika uhusiano wa miaka 50 baina ya China na Ufaransa.

Akizungumza kwenye dhifa ya kiserikali ya kuadhimisha mwanzo wa ziara yake nchini Ufaransa Rais Xi Jinping alisema katika mji wa Lyon kwamba mazungumzo yake na Rais Hollande yatahusu kuupanga mustkabali wa pamoja baina ya nchi zao.

Mustakabal wa pamoja

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius amemwambia Rais Xi kuwa Ufaransa inakaribisha vitega uchumi. Meneja wa kiwanda kikubwa cha nyuklia cha Ufaransa, Areva, bwana Luc Oursel amesema anatumai mikataba kadhaa itatiwa saini katika sekta ya nyuklia wakati mazungumzo yanaendelea China ina mpango wa kujenga kiwanda cha kuyachujia mabaki ya nyuklia. Rais Hollande atamlaki mgeni wake Rais Xi kwenye Ikulu mjini Paris ambako pia watatiliana saini mkataba wa biashara ya magari ya kiwanda cha Peugeot.

Katika kuadhimisha miaka 50 ya uhusiano wa kibalozi baina ya China na Ufaransa Rais Xi atahudhuria dhifa maalumu kwenye Ikulu ya Versailles. Katika ziara yake ya nchini Ufaransa Rais Xi pia anatarajiwa kuujadili mgogoro wa Ukraine na masuala mengine ya kimataifa na mwenyeji wake Rais Hollande.

Mwandishi:Mtullya Abdu.afpe/

Mhariri:Gakuba Daniel