1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Molina akana kuhusika na mashitaka ya rushwa

4 Septemba 2015

Aliekuwa Rais wa Guatemala Otto Perez Molina yuko jela hivi sasa akisubiri kujibu mashitaka mahakamani kufuatia tuhuma za kujihusisha na rushwa zinazo mkabili mnamo wakati makamu wa Rais akiapishwa kukaimu nafasi yake.

https://p.dw.com/p/1GR4G
Alie kuwa Rais wa Guatemala Otto Perez Molina
Alie kuwa Rais wa Guatemala Otto Perez MolinaPicha: Reuters

Jaji wa Guatemala aliamuru rais huyo wa zamani kwenda jela mnamo wakati mchakato wa usikilizaji wa kesi hiyo ukiendelea.

Hadi sasa hakuna mashitaka yaliyokwishafunguliwa dhidi yake na amekuwa pia akikana kuhusika na kashfa yoyote katika sakata hilo huku wachunguzi wakidai kuwa Molina, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 64, alipokea dola milioni 3.7 ikiwa ni rushwa kwa ajili ya kutoa punguzo la kodi kwa wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa nchini humo.

Wabunge wa bunge la nchi hiyo wapatao 116 huku 41 waki kosekana walikutana siku ya alhamisi kupiga kura ya pamoja ya kuamua iwapo wakubali kupokea hatua hiyo ya kujiuzulu kwa Rais Perez Molina ambaye hata hivyo aliwashangaza baada ya kuamua kuachia ngazi.

Siku mbili kabla bunge la Congress la nchi hiyo lilimvua Perez Molina kinga ya kutoshitakiwa likitoa mwanya wa Rais huyo wa zamani kuweza kujibu tuhuma hizo za rushwa mahakakamani.

Makamu wa Rais kukaimu nafasi ya Urais

Makamu wa ais wa nchi hiyo, Alejandro Maldonado, aliapishwa mara moja kukaimu nafasi hiyo ya Urais hafla iliyoshuhudiwa na mamilioni ya wananchi wa Guatemala kupitia televisheni ya taifa hilo.

Waanadamanaji nchini Guatemala
Waandamanaji nchini GuatemalaPicha: picture-alliance/AP Photo/Luis Soto

Mwanadiplomasia huyo wazamani mwenye umri wa miaka 79 aliwataka mawaziri wote wanaounda baraza la mawaziri la nchi hiyo kujiuzulu nafasi zao na kusema ya kuwa atawashirikisha wale wote waliokuwa mstari wa mbele katika kupiga vita masuala ya rushwa kupendekeza vijana wenye taaluma inayopasa kuingia katika serikali atakakayounda.

Hatua ya kujiuzulu kwa Perez Molina inafuatia maandamano ya muda mrefu ambayo baadaye yalifuatiwa pia na vurugu.

Molina aonyesha sura ya unyonge

Molina ambaye ni jenerali wa jeshi wa zamani alionyesha sura ya unyonge mnamo wakati waendesha mashitaka walipokuwa wakisoma mashitaka yanayomkabili huku akionekana kuinamisha kichwa wakati mawasiliano yake ya simu yaliyorekodiwa yalipokuwa yakichezwa yanayomhusisha na kashifa hiyo ya rushwa.

Waendesha mashitaka nchini humo tayari wamemshitaki aliyekuwa makamu wa Rais wa Molina, Roxana Baldetti, aliyejiuzulu wadhifa wake huo mwezi Mei mwaka huu kwa kupokea dola milioni 3.8 kama rushwa mnamo mwaka 2014 huku pia wakidai Molina alikuwa miongoni mwa kundi la wahalifu tangu mwaka 2014 kwa lengo la kuibia nchi hiyo.

Hii ni mara ya kwanza kwa maandamano ya raia yaliyopelekea kujiuzulu kwa Rais nchini Guatemala.

Wakati huo huo, Marekani imekuwa msitari wa mbele kuwapongeza wananchi wa Guatemala kwa hatua yao ya muda mrefu waliochukuwa iliyopelekea kujiuzulu kwa Rais Molina.

Msemaji wa ikulu ya Marekani, Josh Ernest, alisema ya kuwa utawala wa Rais Obama uko tayari kufanya kazi na makamu wa Rais Alejandro Maldonado katika wadhifa wake huo mpya na kuongeza kuwa Marekani pia iko tayari kulisaidia taifa hilo kuweza kusonga mbele katika kipindi hiki cha machafuko nchini humo.

Mwandishi : Isaac Gamba/DWE

Mhariri: Mohammed Khelef