Rais wa zamani wa Maldives kukamatwa? | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.02.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Rais wa zamani wa Maldives kukamatwa?

Mahakama ya Maldives imetoa waranti wa kuwezesha kukamatwa kwa aliyekuwa rais wa visiwa hivyo, Mohammed Nasheed, pamoja na aliyekuwa waziri wake wa ulinzi huku jeshi likitumwa katika mji wenye machafuko wa Addu.

Rais wa Maldives aliyeondoka madarakani, Mohammed Nasheed.

Rais wa Maldives aliyeondoka madarakani, Mohammed Nasheed.

Wakati huo huo Meya wa mji wa Addu ambao ni wa pili kwa ukubwa kisiwani Maldives, amesema utaratibu wa sheria umesambaratika katika mji huo.

Shirika la habari la AFP limearifu kwamba Mahakama ya Maldives imetoa hati ya kisheria ya kuwezesha kukamatwa kwa aliekuwa Rais wa Maldives Mohammed Nasheed pamoja na aliekuwa Waziri wake wa ulinzi Adam Gafoor.

Hata hivyo taarifa hiyo imekanushwa na Mkuu mpya wa Polisi wa Maldives Abdullah Riyas. Lakini duru nyingine imezithibitisha habari hizo. Polisi imesema maandamano aliyoyaongoza baada ya kujiuzulu kilikuwa kitendo cha ugaidi.

Maandamano ya Maldives.

Maandamano ya Maldives.

Kwa mujibu wa taarifa zaidi, polisi sasa wapo njiani kuenda kumkamata rais huyo wa zamani. Lakini hajulikani alipo. Nasheed alijeruhiwa baada ya polisi kuyavunja maandamano anayoyaongoza.

Rais huyo alijiuzulu jumanne iliyopita baada ya maandamano ya kumshinikiza afanye hivyo. Lakini wafuasi wake sasa wanadai kwamba Mohamed Nasheen alipinduliwa. Wafuasi hao wanadai kwamba Rais huyo wa zamani alishikiwa silaha na kulazimishwa kujiuzulu.

Wakati huo huo Meya wa mji wa Addu Abdulla Sodig ameliambia shirika la habari la AFP kwa njia ya simu kwamba utaratibu wa kisheria umesambaratika katika mji huo ambao ni wa pili kwa ukubwa katika kisiwa cha Maldives.

Kwa mujibu wa taarifa, wanajeshi wamepelekwa wakati viongozi wa mji huo wanajaribu kukabiliana na ghasia. Baada ya Meya wa mji huo kusema kwamba utaratibu wa kisheria umesambaratika, wanajeshi 3000 wamepelekwa pamoja na polisi wenye silaha.

Rais mpya wa Maldives, Waheed Hassan.

Rais mpya wa Maldives, Waheed Hassan.

Meya huyo Bwana Sodig alieumizwa mkononi baada ya kushambuliwa na kundi la watu, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba, majeshi hayo ya usalama sasa yanawakamata wanaofanya fujo mitaani.

Hatua ya kuwapeleka wanajeshi na polisi inafuatia ghasia zilizotokea jana usiku katika mji huo wa Addu ambapo vituo viwili vya polisi, mahakama na nyumba za watu binafsi zilishambuliwa na kuchomwa moto. Ghasia zilisambaa na kufika katika mji Mkuu, Male hapo jana ambapo polisi walipambana na wafuasi wa Rais aliejizulu Bwana Mohamed Nasheed.

Meya wa mji wa Addu Bwana Sodig ambae ni mwanachama wa chama cha Democratic cha Rais wa zamani,amesema kuwa hapo awali maandamano yalianza kwa utulivu. Lakini baadae makundi fulani yalijiingiza katika maandamano hayo na kusababisha ghasia.

Habari kutoka mji Mkuu, Male zinasema msemaji wa jeshi Abdul Raheem amethibitisha kwamba majeshi yamepelekwa katika mji wa Addu. Ameeleza kuwa wanajeshi hao hawakuingia katika mji huo ili kuuteka, lakini ametamka kwamba wapo katika mji huo wenye wakaazi 32,000.

Mwandishi: Mtullya Abdu/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef

DW inapendekeza

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com