1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa zamani wa Israel apatikana na hatia

Sekione Kitojo30 Desemba 2010

Rais wa zamani wa Israel Moshe Katsav amepatikana na hatia ya makosa mawili ya ubakaji.

https://p.dw.com/p/zrhD
Rais wa zamani wa Israel Moshe Katsav.Picha: AP

Rais wa zamani wa Israel Moshe Katsav amepatikana leo na hatia ya makosa mawili ya ubakaji, ikiwa ni kilele cha kashfa iliyojitokeza miaka minne iliyopita ambayo ililishangaza taifa hilo la Kiyahudi. Rais huyo wa zamani anakabiliwa sasa na hukumu ya kwenda jela miaka minane.

Wakati mahakama hiyo mjini Tel Aviv ikitoa hukumu hiyo, ambapo pia imemhukumu Katsav kwa madai ya bughdha za kingono, vitendo vinavyovuka mipaka na kuzuwia sheria kuchukua mkondo wake, rais huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 65 ambaye alionekana dhahiri kufadhaika, alikuwa akinong'ona tu, "hapana , hapana".

Hukumu hiyo inakuja baada ya kuendeshwa kesi hiyo ambayo imechukua mwaka mmoja na nusu na kujumuisha madai ambayo ni ya kuhuzunisha, yakimuonesha Katsav kuwa ni mbakaji ambaye mara kwa mara huwasumbua wafanyakazi wanawake katika ofisi yake.

Kiongozi huyo wa zamani wa nchi anashutumiwa kwa kumbaka mara mbili mwanamke mmoja ambaye ametambuliwa kwa jina la "Aleph" wakati akiwa waziri wa utalii, na kuwafanyia usumbufu kingono na kuwabughudhi wanawake wengine wawili wakati akiwa rais. Katsav amesema kuwa hana hatia wakati wote wa uchunguzi wa kesi hiyo ya ubakaji na usumbufu wa kingono.

Awali alikubali makubaliano ya kutoa maelezo yake mahakamani ambayo yangemfanya kukubali madai madogo madogo na kulipa faini ili waendesha mashtaka watupilie mbali madai ya ubakaji, lakini baadaye alibadili msimamo wake, na kufanya makubaliano hayo kuwa batili na kusema anataka kusafisha jina lake mahakamani.

Alilazimika kujiuzulu kama rais , akakabidhi ofisi kwa hasimu wake Shimon Peres. Katsav amewashutumu wahanga wake kwamba wanajaribu kumwendea kinyume na kudai kuwa alikuwa mhanga wa juhudi za kumchafulia jina zinazofanywa na kundi la waendesha mashtaka na vyombo vya habari bila ya yeye kuweza kujitetea. Mwanawe wa kiume Boaz Katsav, baada ya kutolewa hukumu hiyo amesema kuwa baba yake hana hatia.

Tunataka kukata rifaa. Na kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, kila mmoja atatambua kuwa baba yangu , rais wa nane wa taifa la Israel hana hatia.

Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema kuwa ni siku ya masikitiko kwa taifa la Israel na raia wake, lakini ameisifu kesi hiyo kuwa ni ishara ya nguvu za mfumo wa sheria wa nchi hiyo.

Mwandishi : Sekione Kitojo / AFPE

Mhariri : Josephat Charo