1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Uturuki amtaka Khaftar aache matumizi ya nguvu Libya

Saumu Mwasimba
19 Januari 2020

Mkutano wa kimataifa kuhusu amani ya Libya waanza kwa rais wa Uturuki kumtaka kamanda wa kijeshi Halifa Khaftar kuacha kutumia nguvu ili kufungua njia ya mchakato wa kisiasa

https://p.dw.com/p/3WR11
Deutschland | Sicherheitsvorkehrungen zur Libyen-Konferenz | Berlin | General Haftar
Picha: Getty Images/AFP/C. Spicker

Rais wa Uturuki Reccep Tayyip Erdogan amesema Khalifa Khaftar lazima akomeshe msimamo wa kutumia nguvu ili kufungua njia ya kufanyika mchakato wa kisiasa. Erdogan ameuambia mkutano wa Berlin kwamba utekelezaji wa hatua nyingine za mchakato wa kisiasa pamoja na suluhisho vinahitaji Haftar kuondoa msimamo wake wa kutumia nguvu.

Muda mfupi kabla ya mkutano kuanza Kansela Angela Merkel na waziri wa mambo ya nje Heiko Maas walifanya mazungumzo na waziri mkuu Fayez al Serraj na hasimu wake Kamanda Khalifa Haftar katika ofisi ya Kansela. Mazungumzo na viongozi hao wa Libya yamefanyika mbali mbali.

Kiongozi wa serikali ya Libya inayotambuliwa Kimataifa Fayez al-Serraj ameonesha wasiwasi kuhusu agenda ya hasimu wake Khalifa Khaftar kabla ya mkutano mkuu kuanza. Mkutano huo ulioandaliwa na Kansela wa Ujerumani unawakutanisha viongozi wakuu kutoka nchi 12 pamoja na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya nchi za Kiarabu.

Libyen-Konferenz in Berlin l Kanzlerin Angela Merkel und UN-Generalsekretär Antonio Guterres
Picha: picture alliance/dpa/K. Nietfeld

Kamanda Khalifa Khaftar anayelidhibiti eneo la Mashariki mwa Libya yupo Berlin alikowasili toka Jumamosi usiku kwa ajili ya kushiriki kwenye mkutano huo. Mwito uliotolewa na mkutano wa Berlin unazitaka pande hizo kujizuia kuvilenga vituo vya mafuta hii ikiwa ni kulingana na rasimu ya taarifa ya mwisho ya pamoja iliyoonekana Jumapili kabla ya viongozi kuanza mkutano wao.

Rasimu hiyo pia imeitambua kampuni ya mafuta yenye makao yake mjini Tripoli ya NOC kama chombo pekee chenye haki ya kuuza mafuta ya Libya. Rasimu hiyo itajadiliwa kwenye mkutano huo wa kilele unaofanyika Jumapili. 

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis katika misa ya Jumapili amezungumzia suala la Libya na kusema anataraji kwamba mkutano wa Berlin huenda ukasababisha uthabiti wa nchi hiyo. Rais Vladmir Putin anayeshiriki mkutano huo nae amesema matarajio yake ni kwamba mkutano huu utakuwa njia ya mwanzo kuelekea kumalizika vita nchini Libya na kufikiwa suluhisho litakaloleta amani na uthabiti.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Lilian Mtono