1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Putin akutana na Assad

Sudi Mnette
18 Mei 2018

Rais Vladimir Putin wa Urusi amekuwa na mazungumzo ambayo hayakutangazwa mapema na Rais Bashar al-Assad wa  Syria katika mji wa mapumziko wa Sochi. Ikulu ya Kremlin mjini Moscow imesema mazungumzo hayo yalifanyika jana

https://p.dw.com/p/2xw5z
Russland Wladimir Putin & Baschar al-Assad in Sotschi
Rais wa Urusi Wladimir Putin na mwenziwe wa Syria Bashar al-Assad walipokutanaPicha: picture-alliance/dpa/Sputnik/M. Klimentyev

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu ya Kremlin, akizingatia mafanikio makubwa ya Jeshi la Syria, Putin alimuarifu al-Assad  kwamba hali ni muwafaka kuweza  kuimarisha mchakato wa kisiasa na kwamba huenda majeshi ya kigeni yakaanza kuondoka nchini Syria.

Kiongozi wa Syria  aliwahi kusema hivi karibuni kwamba  mafanikio upande wa kijeshi yanamaanisha  kwamba serikali yake inafanikiwa katika kurejesha hali ya kawaida inayofungua njia kwa raia wengi wa nchi hiyo kurudi kwenye makaazi yao.

Uundwaji wa kamati ya kikatiba ya Syria

Schweiz Syrien-Friedengsgespräche in Genf
Wajumbe wa mkutano wa amani wa Syria wa 19.05.2017Picha: Getty Images/AFP/F. Coffrini

Pamoja na hayo alinukuliwa akisema  yeye na  Putin walizungumzia juu ya kamati ya kikatiba  inayokusudiwa kuundwa, ili kuzungumzia marekebisho ya  katika katiba , kufuatia mkutano wa Baraza kuu la majadiliano la  Syria uliofanyika  mjini Sochi mwezi Januari.

Wanasiasa wakuu wa upinzani waliyasusia mazungumzo hayo, lakini Assad amesema  Syria iko tayari kuanza kufanya kazi na Umoja wa Mataifa, kuandaa muswaada wa marekebisho ya katiba. Urusi ni mshirika mkubwa wa Bashar al-Assad  na msada wa kijeshi kutoka Moscow umemsaidia rais huyo wa Syria kupata mafanikio makubwa kuyakomboa maeneo yaliokuwa yakidhibitiwa na  wapinzani wake katika vita mnamo miezi ya hivi karibuni, yakiwemo yale yanayouzunguka mji mkuu Damascus.

Rais Putin asema magaidi waweka chini silaha

Katika matamshi yake yaliochapishwa  hapo kabla  katika mtandao wa Ikulu, Rais Putin alisema magaidi wameweka chini silaha katika maeneo muhimu nchini Syria, jambo ambalo limefanikisha kurirejesha miundo mbinu katika hali ya kawaida na hasa kumaliza harakati zao za kijeshi karibu na mji mkuu  Damascus. Kwa upande wake al-Assad aliwashukuru wanajeshi wa Urusi na hasa wale wa kikosi cha anga, kwa mchango wao muhimu, aliouita " wa kupambana na  magaidi."

Urusi ni miongoni mwa nchi tatu pamoja na Uturuki na Iran zinazojiona kuwa na usemi katika  mazungumzo kati ya upinzani nchini Syria na serikali, chini ya kile kinachoitwa mchakato wa Astana. Mazungumzo kati ya pande hizo  yamekuwa yakiendelea kila wakati katika mji  mkuu huo wa Kazakhstan tangu 2017, kwa lengo la kukamilisha  mchakato wa amani unaoongozwa na Umoja wa mataifa.

Mazungumzo ya Putin na Assad mjini Sochi jana yamekuja siku moja kabla ya Kansela Angela Merkel wa Ujerumani kukutana na  Rais Putin  mjini   humo, huku Syria ikiwa ni  moja wapo ya  masuala katika ajenda ya mazungumzo. Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen amesema  haamini  kuwa Urusi itamuunga mkono al-assad kwa muda mrefu zaidi. Akaongeza ," Mustakbali wa muda mrefu na  mchinjaji al-Assad, ambaye ana damu mikononi mwake si jambo litakalotokea."   Zaidi ya Wasyria 400,000 wamekufa katika mzozo huo ulioanza 2011 kwa maandamano yakudai mageuzi nchini humo. Mamilioni wengine wamekimbilia nchi za nje au kuwa wakimbizi wa ndani.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, dpa
Mhariri: Grace Patricia Kabogo