Rais wa Ujerumani Horst Köhler aendelea na ziara yake ya Amerika Kusini | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.03.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Rais wa Ujerumani Horst Köhler aendelea na ziara yake ya Amerika Kusini

Rais wa Ujerumani Horst Köhler anazuru Brazil katika ziara yake ya siku kumi na mbili ya mataifa ya Amerika Kusini.

Rais wa Ujerumani Horst Köhler

Rais wa Ujerumani Horst Köhler

Rais wa Ujerumani, Horst Köhler, yumo nchini Brazil ikiwa ni kituo chake cha pili katika ziara yake ya siku 12 ya Amerika Kusini. Jana alikitembelea kituo cha umeme cha Itaipu katika eneo la mpakani kati ya Brazil na Paraguay. Kituo hicho kinaelezwa kuwa kikubwa zaidi duniani cha kutengeneza umeme kutokana na maji. Rais Köhler alikutana pia na jaji wa mahakama kuu ya serikali ya Brazil katika mji mkuu Brasilia na baadaye kukutana na viongozi wa wakfu za kisiasa za Ujerumani mjini humo.

Shughuli nyengine muhimu aliyoifanya rais Köhler mjini Brasilia ni kulifungua jengo jipya la ubalozi wa Ujerumani. Rais wa Brazil, Ignacio Lula da Silva, alihudhuria sherehe hiyo ya ufunguzi wa jengo hilo.

Rais Koehler aliwasili Brazil akitokea nchini Paraguay kituo chake cha kwanza cha ziara yake ya Amerika Kusini. Alipokuwa nchini humo rais Köhler alikutana na rais wa Paraguay, Nicanor Duarte Frutos, katika mji mkuu Asuncion. Baadaye alikutana pia na kundi la wakristo wanaozungumza lugha ya kijerumani mjini humo.

Ziara ya rais Horst Köhler wa Ujerumani nchini Paraguay ilikuwa ya kwanza rasmi katika kipindi cha miaka 146 ya uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo mbili. Kiongozi huyo anataka kuwepo vita vya kupambana na umaskini na usawa wa kijamii.

´Mpaka sasa kuna tofauti kubwa za mishahara miongoni wa raia wa Amerika Kusini. Idadi ndogo yenye mishahara mikubwa na idadi kubwa inayopata mishahara midogo isiyoweza kukidhi mahitaji yao kimaisha. Hilo linasabisha wasiwasi wa kisiasa ambao kwa mda mrefu si mzuri. Lakini kama kuna waajiri hapa ambao wanajua majukumu yao ya kijamii, yaani kuoanisha uchumi na jukumu la kijamii, basi nafikiri hiyo ni sehemu muhimu zaidi ya kuboresha hali tayari ambayo tayari imetimizwa.´

Wajerumani 10,000 na raia 120,000 wa asili ya kijerumani wanaishi nchini Paraguay. Ziara ya rais Köhler nchini humo ilikuwa pia ya kutathmini maendeleo yaliyopatikana tangu kuanza kutekelezwa katiba ya kidemokrasia kufuatia kuangushwa madarakani kiongozi wa kiimla, Alfredo Stroessner, mnamo mwaka wa 1989. Kabla kuelekea Brazil rais Köhler alionya juu ya tofauti kubwa ya mishahara akisema utamaduni wa aina hiyo hauna maisha marefu.

´Nchini Brazil watu wanakwenda ofisini kutumia helikopta na magari yasiyoweza kutobolewa kwa risasi. Maendeleo haya hayatadumu na ndio maana ni muhimu kwa masilahi ya wafanyabiashara na watu wa tabaka la juu maishani kuwajali maskini na waelewe kwamba utamaduni wa tofauti kubwa za mishahara na mahitaji mengine ya kimaisha hautadumu.´

Katika ziara yake ya Amerika Kusini rais Horst Köhler, aliyekuwa zamani kiongozi wa fuko la fedha la kimataifa, IMF, ameandamana na viongozi wa kibiashara wa Ujerumani, majaji wa mahakama ya katiba, wajumbe wa kanisa Katoliki wa Ujerumani na mkewe Eva. Kituo cha mwisho cha ziara ya rais Köhler ni nchini Colombia.

 • Tarehe 07.03.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHIi
 • Tarehe 07.03.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHIi

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com