1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Ufilipino chini ya shinikizo

14 Novemba 2013

Rais Benigno Aquino wa Ufilipino yuko chini ya shinikizo linalozidi kuongezeka kuharakisha usambazaji wa chakula, maji na madawa kwa manusura walioko kwenye hali mbaya kufuatia kimbunga kikali kilichoipiga nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/1AHQU
Maelfu ya nyumba zaangamizwa katika mji wa Tacloban kufuatia kimbunga Haiyan nchini Ufilipino.
Maelfu ya nyumba zaangamizwa katika mji wa Tacloban kufuatia kimbunga Haiyan nchini Ufilipino.Picha: Reuters

Rais Benigno Aquino wa Ufilipino yuko chini ya shinikizo linalozidi kuongezeka kuharakisha usambazaji wa chakula, maji na madawa kwa manusura walioko kwenye hali mbaya kufuatia kimbunga kikali pamoja na kuanzisha tena serikali za mitaa ambazo zimeshindwa kufanya kazi kutokana na athari ya kimbunga hicho.

Wakati juhudi za kimataifa za kutowa misaada zimepamba moto wamiliki wengi wa vituo vya mafuta ambao biashara zao zimenusurika wanagoma kufunguwa upya vituo hivyo na kusababisha kuwepo kwa uhaba wa mafuta ambayo yanahitajiwa na malori ili kuweza kusafirisha mahitaji na timu za matibabu kwenye maeneo yalioathirika ikiwa takriban wiki moja baada ya kimbunga hicho cha Haiyan kuikumba Ufilipino.

Alfred Romualdez meya wa mji wa Tacloban mji wa wakaazi 220,000 uliogeuzwa kuwa vifusi katika jimbo lililoathirika zaidi la Leyta amesema hali inatisha, kunakuwepo na maombi kutoka kwa jamii ya kwenda kondowa maiti ambao wanasema ni maiti tano au kumi lakini wakati wanapofika maeneo husika hukutana na miili 40.Ameongeza kusema kwamba uhaba wa malori unafanya hali kuzidi kuwa ngumu ambapo inakuwa vigumu kuamuwa iwapo malori hayo yatumike kusambaza chakula au kukusanya maiti.

Maiti zimeanza kuzikwa

Nje ya Tacloban takriban maiti 300 zimeanza kuzikwa katika kaburi la pamoja leo hii na kaburi kubwa litachimbwa kwa ajili ya kuzika maiti 1,000. Afisa tawala wa jiji Tecson John Lim ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters amesema serikali za mitaa zinaendelea kushindwa kufanya kazi zikiwa na wafanyakazi 70 kutoka 2,500 ambapo wengi wao wameuwawa au wameemewa mno na huzuni kuweza kufanya kazi.

Manusura wa kimbunga Haiyan nchini Ufilipino.
Manusura wa kimbunga Haiyan nchini Ufilipino.Picha: Nicolas Asfouri/AFP/Getty Images

Meli ya kubeba ndege ya Marekani USS George Washington inatarajiwa kuwasili Ufilipino leo jioni ikiwa na mabahari 500 na ndege zaidi ya 80.Japani pia inapanga kutuma wanajeshi 1,000 na manowari pamoja na ndege kwa kile ambacho yumkini kikawa ni utumiaji mkubwa wa kijeshi wa nchi hiyo kuwahi kushuhudiwa tokea baada ya kipindi cha vita cha nchi hiyo.

Rais ashinikizwa

Rais wa Ufilipino Benigno Aquino amekuwa akijitetea kutokana na namna alivyoshughulikia kimbunga hicho kwa kuanzia na kutolewa kwa tahadhari juu ya nguvu yake na hatari ya kuzuka kwa dhoruba na sasa kasi ya juhudi za kutowa misaada.

Rais Benigno Aquino wa Ufilipino.
Rais Benigno Aquino wa Ufilipino.Picha: Reuters

Amesema idadi ya vifo ingelikuwa kubwa zaidi ingelikuwa watu hawakuhamishwa na kutotayarishwa kwa shughuli za misadaa lakini manusura wanasema hawakupata tahadhari ya kutosha kuhusu mawimbi makubwa kama yale ya tsunami.

Aquino pia amezusha mjadala juu ya kiwango cha maafa na kupunguza sana idadi ya vifo kutoka 10,000 iliokuwa imekadiriwa na serikali za mitaa.Serikali imethibitisha kufikia leo watu waliokufa ni 2,357 kiwango ambacho wafanyakazi wa misaada wanasema kinaweza kuongezeka.

Kwa mujibu wa Shirika la Msalaba Mwekundu idadi ya awali ya watu wasiojulikana walipo kufikia leo imeendelea kubakia 22,000 lakini imetahadharisha kwamba idadi hiyo inaweza kujumuisha wale ambao tayari wamepatikana.

Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya watu 544,600 wamepoteza makaazi yao na takriban asilimia 12 ya wananchi wa nchi hiyo wameathirika na kimbunga hicho lakini maeneo mengi bado hayakupokea misaada.

Mwandishi: Mohamed Dahman/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef