1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Tunisia ameapa kuutokomeza ugaidi

19 Machi 2015

Rais wa Tunisia ameahidi kuukabili bila huruma ugaidi nchini mwake baada ya washambuliaji kuwaua watu kumi na tisa, kumi na saba kati yao wakiwa watalii wa kigeni katika jengo la kumbukumbu za kihistoria hapo jana.

https://p.dw.com/p/1Et2A
Picha: Getty Images/AFP/F. Belaid

Rais wa Tunisia Beij Caid Essebsi ambaye amewatembelea hospitalini waliojeruhiwa katika shambulizi la kigaidi ameapa kuwa serikali yake itapambana na ugaidi hadi mwisho bila ya huruma yoyote na kuwataka raia wa nchi hiyo kufahamu kuwa wako katika mapambano dhidi ya ugaidi na watu wachache katika jamii hawatalitisha taifa zima.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amelaani shambulizi hilo alilolitaja kuwa la kusikitisha na kuongeza kuwa ameghadhabishwa mno na shambulizi hilo.

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa pia limelaani shambulizi hilo na kusisitiza kuwa hakuna shambulizi la kigaidi litakaloifanya Tunisia kuachana na azma ya kutafuta njia ya kujiimarisha kidemokrasia, kuufufua uchumi wake na kuboresha maendeleo.

Jumuiya ya kimataifa yalaani mashambulizi

Shambulizi hilo limewaghadhabisha maelfu ya watunisia ambao walikusanyika katika mji mkuu wa Tunisia, Tunis wakiimba wimbo wa taifa na kuwalaani washambuliaji waliowaita magaidi.

Watu wakitoroka mashambulizi katika makavazi ya Tunisia
Watu wakitoroka mashambulizi katika makavazi ya TunisiaPicha: picture-alliance/AP/H. Dridi

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ameyalaani pia mashambulizi hayo huku waziri mkuu wa Uingereza David Cameron akisema ameshutushwa na shambulizi hilo. Rais wa Ufaransa Francois Hollande naye amesema anaungana na Tunisia wakati huu akiongeza kuwa mashambulizi ya kigaidi yameathiri kila mmoja.

Waziri mkuu wa Tunisia Habib Essid amesema washambuliaji waliokuwa wamevalia magwanda ya kijeshi waliwafyatulia watalii risasi walipokuwa wakishuka kutoka kwenye basi moja na kuwaandama hadi ndani ya makavazi hayo na kuwashika kadhaa mateka.

Miongoni mwa raia wa kigeni waliouawa katika shambulizi hilo ni raia watatu wa Japan, wanne wa Italia, wawili wa Colombia wawili wa Poland na mmoja mmoja kutoka Australia, Ufaransa na Uhispania.

Watalii wa kigeni walengwa

Essid amesema askari waliwauawa washambuliaji wawili na wanawasaka wengine. Kiasi ya watu wengine 40 pia wamejeruhiwa katika Shambulio hilo baya zaidi tokea lile la kujitoa mhanga la wafuasi wa Al-Qaeda kwenye sinagogi moja katika kisiwa cha utalii cha Djerba 2002, ambapo watu 21 waliuwawa. Wakati wa shambulizi, takriban watalii 100 walikuwa katika jengo hilo ambalo liko karibu na bunge la Tunisia.

Waziri mkuu wa Tunisia Habib Essid
Waziri mkuu wa Tunisia Habib EssidPicha: Getty Images/AFP//F. Belaid

Hakuna kundi ambalo limedai kuhusika na shambulizi hilo la jana lakini Tunisia imekuwa ikikabiliwa na ongezeko la mashambulizi kutoka kwa makundi ya wanamgambo wenye itikadi kali.

Maafisa nchini Tunisia wamesema kiasi ya raia 3,000 wamekwenda nchini Iraq, Syria na nchi jirani ya Libya kujiunga na makundi ya kijihadi likiwemo la dola la kiislamu IS. Kiasi ya wapiganaji 500 wa Tunisia wanaaminika kurejea nyumbani.

Mwandishi:Caro Robi/Afp/dpa

Mhariri: Gakuba Daniel