1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa China ziarani Marekani

Sekione Kitojo18 Januari 2011

Wachina wanaiangalia Marekani kama mshindani wao mkuu katika masuala ya kiuchumi na biashara, wakati rais wa nchi hiyo Hu Jintao akifanya ziara yake ya kwanza nchini humo.

https://p.dw.com/p/zz45
Rais Barack Obama na rais Hu Jintao wa China katika mkutano wa kundi la G20 Nov. 11, 2010, mjini Seoul, Korea ya kusini.Picha: AP

Rais wa China Hu Jintao amekwenda Marekani katika ziara ya siku nne ya kiserikali. Kuna mengi ya kidiplomasia yakuzungumza kati ya pande hizo mbili kuurudisha katika hali nzuri uhusiaono uliokuwa umekumbwa na misukosuko.Lakini je kwa Wachina Marekani bado ni taifa linalopendeza machoni mwao kama ilivyokuwa mwanzo?

Gazeti la China la Global Times katika toleo lake la mwishoni mwa mwaka liliandika makala iliyohoji ni vipi Wachina wanavyoutazama ulimwengu kwa uwazi zaidi. Kutokana na makala hiyo imedhihirika kwamba Wachina wengi wanaitazama Marekani kama iliyo bado katika nafasi ya juu kwa umaarufu. Hata hivyo kiwango cha wanaoishabikia Marekani kimeteremka ikilinganishwa na mwaka 2008 kutoka asilimia 20 hadi asilimia 7.5.Hali hii lakini sio jambo la kushangaza kama anavyosema Profesa Shi Yinhong wa chuo kikuu cha Beijing.Anasema kwamba wakati Wachina wakizidi kupata moyo wa kujiamini ndivyo wanavyozidi kujitenga na Marekani.

''Idadi kubwa ya Wachina wanaikosoa siasa ya nje ya Marekani. Na suala hili linakuja hasa inapohusu siasa ya China na Marekani. Mtu anavyoona hali ilivyokuwa hapo awali kati ya pande hizo mbili ni vigumu kueleza na kuelewa hasa kuhusu mtazamo huu wa sasa.''

Hatua ya Marekani ya kuuza silaha huko Taiwan, mvutano wa kibiashara kati ya China na Marekani, suala la kujiondoa kwa mtandao mkubwa wa google kutoka China hatua ya kufanya luteka ya kijeshi katika pwani ya China na hiyo ndiyo inayoonekana kuwa chachu iliyozusha mvutano katika mwaka uliopita baina ya pande hizo mbili.

Suala jingine ambalo daima huonekana kuzusha mvutano katika uhusiano baina ya China na Marekani ni suala la Biashara. Rais wa China Hu Jintao kabla ya kuanza ziara yake hii alitoa taarifa akikosoa sera za taasisi za fedha za Marekani. Zaidi ni suala linalohusu sarafu ya China.

Licha ya mafanikio ya wafanyibiashara wa China ulimwenguni sarafu ya Yuan ina nafasi ndogo katika jukwaa la kimataifa kutokana na vikwazo vilivyopo katika ubadilishanaji na sarafu nyingine.

Rais Barack Obama wa Marekani anatarajiwa kumtia kishindo rais Hu Jintao kuhusiana na suala hilo la sarafu ya Yuan.Wakosoaji wanasema kwamba Beijing inateremsha makusudi thamani ya sarafu yake ili kuimarisha biashara yake nje na wengi wanakasirishwa na hatua hiyo. Wamarekani wengi wanaamini hatua hiyo inasababisha hali mbaya katika uchumi wake pamoja na soko lake la ajira.

Rais Hu Jintao anayetarajiwa kujiuzulu kama rais na katibu mkuu wa chama cha Kikomunisti mwaka 2012 anawasili Marekani leo usiku katika ziara ambayo ni ya kwanza na ya mwisho katika jukwaa la kisiasa.

Mwandishi: Cao, Haiye/DW/Saumu Mwasimba
Mhariri: M. Abdul-Rahman