1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa China bungeni Marekani

20 Januari 2011

Rais wa China Hu Jintao akiendelea na ziara yake rasmi ya siku nne nchini Marekani, hii leo anatembelea bunge la Marekani linalokosoa vikali sera za China kuhusu sarafu yake ya Yuan.

https://p.dw.com/p/QtlV
Der chinesische Präsident Hu Jintao mit US-Präsident Barack Obama vor dem staatsbankett im Weißen Haus am 19.01.2011. (AP Photo/Carolyn Kaster)
Rais Hu Jintao(kushoto) akikaribishwa Ikulu na Rais Barack ObamaPicha: AP

Mbali na suala hilo, mada nyingine iliyozushwa katika mkutano wake pamoja na Rais Barack Obama hiyo jana ni suala tete kuhusu haki za binadamu nchini China. Marais hao wawili walitofautiana katika maoni yao kuhusu mada hiyo, lakini waliahidi kushirikiana zaidi ili kujenga uaminifu. Lakini hii leo, Rais Hu atakapokutana na wabunge wa Marekani, mazingira yatakuwa tofauti kabisa, kwani tangu mwaka 2005 wabunge wa Marekani wametishia kupitisha sheria ya kutoza ushuru maalum kwa bidhaa za China, katika jitahada ya kukabiliana na sera za China kuhusu sarafu yake Yuan, ikituhumiwa kuwa inazuia thamani ya sarafu hiyo kuongezeka, ili bidhaa zake ziwe rahisi katika masoko ya dunia. Hadi sasa China imekataa kuitikia mito ya kupandisha thamani ya Yuan.

Hata kwenye mkutano wa waandishi wa habari hiyo jana, mjini Washington, ilidhihirika kuwa Rais Barack Obama na mwenzake Hu Jintao hawakuweza kuondosha tofauti zao kuhusu thamani ya Yuan, licha ya hapo awali kutangazwa makubaliano ya biashara yenye thamani ya mabilioni ya dola. Juu ya hivyo, pande zote mbili zimeahidi kuendelea kushirikiana katika masuala muhimu ya kimataifa. Hata hivyo Obama hakusita kulizusha suala la haki za binadamu. Alisema:

"Nimesisitiza kuwa Marekani inawajibika kuheshimu haki za kimataifa. Hizo ni haki za binaadamu, uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kueleza maoni, kukutana, na uhuru wa kuabudu. Haki hizo zinatambuliwa katika katiba ya China vile vile."

Aufgenommen vor dem Weissen Haus, am 19.01.2011, von You Ran, freier Mitarbeiterin der DW Menschenrechtsgruppen demonstrieren während des Besuchs von Hu Jintao bei Obama,
Wanaharakati wa haki za binadamu wakiandamana nje ya Ikulu ya WashingtonPicha: DW

Rais Hu aliepuuza suala la ripota mmoja kuhusu haki za binaadamu, baadae hakuwa na budi kuzungumzia mada hiyo na kueleza hivi:

"China daima imewajibika kuhifadhi na kuheshimu haki za binadamu na imepiga hatua kubwa katika suala hilo"

Akaongezea kuwa China ni taifa kubwa lenye matatizo mengi kuhusu maendeleo ya kijamii na kiuchumi.Hata hivyo, amekiri kuwa bado kuna mengi yanayohitaji kutekelezwa kuhusu haki za binaadamu nchini China. Kwa jumla, wadadisi wa Marekani wanasema kuwa mkutano wa kilele kati ya Hu na Obama, umesaidia kuipatia Marekani mikataba ya kibiashara na vile vile viongozi hao wamekubaliana kuwa na ushirikiano zaidi katika masuala ya kijeshi na kukabili hatari ya kusambazwa kwa silaha za kinyuklia kutoka Korea ya Kaskazini na Iran.

Mwandishi:Martin,P/RTRE
Mpitiaji:Mohammed Abdul-Rahman