1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Steinmeier akosoa Brexit na wazalendo

Iddi Ssessanga
4 Aprili 2017

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ameonya kuwa wafuasi wa siasa kali wanatumia kisingizio cha uzalendo kutoa nadhari kwenye masuala muhimu. Steinmeier pia amekosoa uamuzi wa Brexit kuwa ni kutokuwa na dhamana.

https://p.dw.com/p/2agBm
Frankreich Bundespräsident Steinmeier besucht EU-Parlament
Picha: picture alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Katika moja ya hotuba zake kubwa tangu alipoapishwa kuwa mkuu wa nchi ya Ujerumani mwezi uliopita, mwanadiplomasia huyo wa zamani ameitaja hatua ya Uingereza kuondoka ndani ya Umoja wa Ulaya kuwa mbaya na kuonya kuwa nchi hiyo itateseka bila tajiriba ya kiuchumi na kisiasa ya Umoja wa Ulaya.

Steinmeier amesema ni ukosefu wa dhamana kusema kwamba katika dunia hii, nchi ya Ulaya inaweza kufanya sauti yake na maslahi yake ya kiuchumi kusikika bila Umoja wa Ulaya. Akizungumzia matamshi ya kizalendo na ya kupinga uhamiaji yaliohanikiza katika kampeni za Uingereza kuondoka katika Umoja wa Ulaya, na pia kampeni za uchaguzi barani Ulaya, na hususani nchini Ufaransa, Steinmeier amewataka raia wa Ulaya kuyapuuza mavuguvugu hayo.

"Rejesha udhibiti, hiyo ni kaulimbiu nzito tunayoisikia kila mahala, lakini nataka niseme hivi, wazalendo hawataweza kuitimiza, na kama inaweza kutimizwa, basi ni jambo ambalo tunaweza kulifanikisha kwa pamoja ikiwa hatutayafanya mambo kuonekana mepesi isivyo, kama hatutoiachia majukumu Brussels, lakini tukashughulikia mambo pamoja, ikiwa tutaimarisha soko la ndani na wakati huo huo tukawalinda wale ambao wameathirika na utandawazi.

Frankreich Bundespräsident Steinmeier besucht EU-Parlament
Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akilihutubia bunge la Ulaya mjini Strasbourg 04.04.2017.Picha: picture alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Ikiwa uwezo wetu wa ubunifu unaweza kuimarishwa ili Ulaya iweze kubadilika na ikiwa hatukubali tu mabadiliko, hapo ndipo tunaweza kuwanyima nafasi wafuasi wa siasa kali na kuwaambia hatupotezi uhuru barani Ulaya, na kinyume chake, kwa mara ya kwanza tunapata nguvu, uzito duniani kupitia umoja huo," alisema Steinmeier mbele ya bunge la Ulaya mjini Strasbourg.

Steinmeier pia amekosoa uzalendo wa kutathimini watu wengine kwa misingi ya utamaduni wao kuwa ni uwezo mdogo wa kufikiri na kusema wale wanaounga mkono uzalendo wa namna hiyo walikuwa wanachimba mahandaki, na kuongeza kuwa wakiwa na Ulaya iliyo imara, watatafuta njia za kujenga mdaraja juu ya mahandaki hayo.

Matamshi ya rais Steinmeier yamekuja kabla ya moja ya ziara zake rasmi katika wadhifa wake mpya katika nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya Ugiriki. Ziara hiyo inatazamiwa kuwa ngumu, kwa sababu Ujerumani kwa sasa inajiona kama mdhamini mkubwa wa mshikamano wa Ulaya.

Hata hivyo mvutano bado uko juu kati ya mataifa hayo mawili kuhusiana na mgogoro wa madeni wa Ugiriki, na jukumu la serikali mjini Berlin, kama mmoja ya wakopeshaji wakuu wa hatua za kubana matumizi zinazochukiwa sana na raia wa Ugiriki.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae,DW

Mhariri: Saumu Yusuf