1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Rouhani ashinda kwa kishindo

20 Mei 2017

Rais Hassan Rouhani wa Iran amechaguliwa tena kuwa rais wa nchi hiyo baada ya kuzowa asilimia 57 ya kura matokeo yanayoonyesha kuungwa mkono kwa juhudi zake za kujenga upya uhusiano wa kigeni wa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/2dHyP
Hassan Rouhani
Picha: Reuters/President.ir

Ushindi wake huo umetangazwa Jumamosi (20.05.2017) na waziri wa mambo ya ndani wa nchi hiyo.

Sheikh huyo mwenye umri wa miaka 68 ametumia miongo mitatu katika kitovu cha utawala wa kimapinduzi wa Iran lakini bado anakabiliwa na upinzani kutoka kwa wale wenye misimamo mikali wakati akijaribu kujenga upya uhusiano na mataifa ya magharibi.

Rouhani ambaye daima amekuwa akivaa kilemba cheupe amerudia tena ushindi wake wa kishindo alioupata mwaka 2013 kwa kuwaunganisha pamoja wafuasi wa misimamo ya wastani na wanamageuzi kwa ahadi zake za kukomesha kutengwa kwa Iran na kuboresha haki za kiraia nchini Iran.

Rouhani ambaye amezaliwa katika jimbo la Semnan tarehe pili Novemba mwaka 1948 ameowa na ana watoto wanne na anashikilia shahada ya uzamivu katika sheria kutoka Chuo Kikuu cha Caledonia cha Glasgow huko Scotland.

Amejinadi kama mgombea wa mabadiliko na uhuru wa kijamii kwa kuwashambulia wapinzani wake kuwa watu wenye misimamo mikali na "enzi yao imekwisha."

Makubaliano ya nyuklia

Iran Präsident Rohani zu U.S. Luftschlägen gegen syrischen Luftwaffenstützpunkt
Rais Hassan Rouhani.Picha: picture-alliance/AA/Iranian Presidency

Muhula wake wa kwanza umeshuhudia kufikiwa kwa makubaliano ya kihistoria na mataifa yenye nguvu duniani ambayo yamekomesha vikwazo vingi na mzozo wa miaka 13 kuhusiana na mpango wa nyuklia wa Iran.

Pia ameanzisha mtizamo wa kisomi zaidi katika kuushughulikia uchumi na kudhibiti mfumuko wa bei uliokuwa ukiongezeka.Lakini wakosoaji wake wanasema amezitelekeza kwa kiwango cha kupindukia faida za kiuchumi kutokana na makubaliano hayo ya nyuklia na kulikuwa na hofu kwamba kuendelea kwa mkwamo wa kiuchumi na ukosefu mkubwa ajira kutaathiri juhudi zake za kutaka kuchaguliwa tena.

Jambo hilo limethibitika kwa halina msingi wakati Rouhani alipomshinda mpinzani wake mwenye msimamo mkali Ebrahim Raisi kwa kujipatia asilimia 57 ya kura hapo Ijumaa kwa kuungwa mkono na idadi kubwa ya watu waliojitokeza kupiga kura.

Ushindi wa kishindo

Iran Präsidentschaftswahl | Ebrahim Raisi
Ebrahim Raisi mpinzani mkuu wa Rouhani katika uchaguzi wa rais.Picha: Reuters/Tima

Wafuasi wake walitaraji ushindi mwengine wa kishindo utampa uwezo zaidi wa kuregeza vikwazo vya kijamii na kuwaachilia huru wanaharakati na viongozi wa upinzani waliofungwa baada ya maandamano makubwa ya umma hapo mwaka 2009.

Uzoefu mkubwa wa Rouhani wa kushughulikia vitu faraghani aliopata kutoka kwa marehemu mwanamapinduzi aliekuwa na ushawishi wa maamuzi Akbar Hashemi Rafsanjani umemuweka katika nafasi madhubuti kuweza kuzungumza na makundi ya kihafidhina zaidi yalioko katika taasisi za mahakama na vikosi vya usalama nchini humo.

Akiwa kama msuluhishi wa Iran katika mpango wake wa nyulia kwa mazungumzo ya mwaka 2003 hadi mwaka 2005,Rouhani alijipatia jina la utani la "sheikh mwanadiplomasia" kutoka kwa wazungu washirika wa mazungumzo hayo lakini huo pia ukawa ndio mwanzo wa shutuma kuoka wenye msimamo mikali nyumbani ambao walimtuhumu kwa kuyapigia magoti mataifa ya magharibi.

Muumini wa utawala wa kimapinduzi

Iran Präsidentschaftswahlen 2017
Wapiga kura wakionyesha wino baada ya kupiga kura .Picha: Getty Images/M. Saeedi

Kabla ya hapo alikuwa muumini shupavu wa utawala wa kimapinduzi.Alishikilia nyadhifa muhimu za ulinzi wakati wa vita vya Iran na Iraq vya mwaka 1980 - 1988 kabla ya kutumika kwa miaka 16 akiwa katibu wa Baraza Kuu la Usalama la Taifa ambao ni wadhifa wa juu wa usalama nchini Iran.

Wakati maandamano ya wanafunzi yalipoingia mitaani hapo mwaka 1999 Rouhani aliwaita "majambazi na wahujumu" na baya zaidi ni "wachafuzi wa dunia " madai ambayo yanastahiki adhabu ya kifo nchini Iran.Msimamo wake kutokea wakati huo umekuwa ukilainika.

Rouhani daima amekuwa akitaka kujega upya uhusiano na Marekani na amekuwa kiongozi wa kwanza wa Iran kuzungumza na mwenzake wa serikali ya Marekani wakati Barack Obama alipompigia simu hapo mwezi wa Septemba mwaka 2013.

Katu hakuwahi kuwa katika njozi yoyote ile juu ya ugumu wa uhusiano huo ambapo aliwaambia waandishi wa habari wa Marekani hapo mwaka 2002: " Marekani haina shauku na nchi zilizo huru .....Marekani ina shauku na nchi ambazo zinasalimu amri kabisa na kuchukuwa hatua kwa mujibu wa madai ya Marekani."

Mwandishi : Mohamed Dahman /AFP/

Mhariri : Caro Robi