Rais Obama apata muwafaka wa kupunguza madeni ya serekali ya Marekani | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.08.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Rais Obama apata muwafaka wa kupunguza madeni ya serekali ya Marekani

Rais Barack Obama wa Marekani na viongozi wa vyama vya Democratic na Republican wamekubaliana juu ya suluhu ya kuyatanzua mabishano kuhusu madeni ya serekali.

default

Rais Barack Obama wa Marekani baada ya kupata muwafaka wa kuzidisha kiwango cha juu cha serekali kuweza kukopa

Rais Barack Obama wa Marekani na viongozi wanaoongoza kutoka vyama vya Republican na Democratic vya nchi hiyo wamekubaliana juu ya suluhu ya kuyatanzua mabishano kuhusu madeni ya serekali. Makubaliano hayo lazima sasa yatamaliza ile sarakasi ya kisiasa iliokuwa inaendelea huko Washington.

Maafikiano hayo yaliokuwa yanatakiwa sana kwa muda mrefu yako machoni mwa watu, lakini sio kwamba ni ya uhakika moja kwa moja. Pale rais Obama alipotangaza jana usiku kwamba suluhisho limefikiwa katika mashauriano ya kupandisha juu kiwango ambacho serekali ya Marekani inaweza kukopa, masoko ya fedha barani Asia yalikuwa yanaanza shughuli za kila siku; pia ilionekana waziwazi kwamba, angalau, dunia imepumua. Hata hivyo, suluhisho hilo ambalo Rais Obama aliweza kuafikiana na wabunge wa vyama vya Democratic na Republican lazimakwanza liuzike kwa wabunge wa baraza la wawakilishi. Ni pale baraza la Senate na la wawakilishi yatakapotoa vibali vyao ndipo muwafaka huo utakuwa umepita. Na jambo hilo litabidi lifanyike leo, lakini sio kwamba jambo hilo litakuwa rahisi.

Bado kutakuwa na wabunge ambao hawataliunga mkono suluhisho hili. Kwa upande wa Chama cha Republican kuna wabunge ambao wameshaamua vichwani mwao kwamba, kimsingi, kiwango cha serekali kuweza kukopa kisizidishwe, au wabunge hao wanahisi kwamba kupunguzwa matumizi katika sekta za huduma za kijamii hakujaenda mbali vya kutosha. Na kwa upande wa wabunge wa Chama cha Democratic, kuna wale wanaopinga, kimsingi, kupunguzwa matumizi katika bima ya kijamii. Hadi sasa haijafahamika kwanini pande hizo mbili zilishindwa kukubaliana kabla, lakini sasa pande hizo hazitaweza kuonekana kuwa hazina dhamana.

Hakuna wakati zaidi wa kuuboresha muwafaka huu. Wakati unayoyoma, na ifikapo kesho, serekali ya Marekani itakuwa haina uwezo wa kukopa. Hali hiyo itakuwa na matokeo mabaya kwa watu, na wale wabunge wenye vichwa vikaidi watashindwa kujitetea. Watu wenye mahitaji ya huduma za kijamii hawataweza kulipiwa na serekali pale serekali itakapokuwa imefilisika, na hamna mfanya biahara ambaye ataweza kuchukuwa mkopo pale riba za mikopo zitakapopanda. Kwa hivyo, hakutakuweko na suala kama kuliunga mkono suluhusu hilo na suala la kupandisha kiwango cha fedha ambacho serekali inaweza kukopa.

Suluhisho linaunganisha kupandisha kiwango cha serekali kuweza kukopa na ulazima wa kupunguzwa matumizi ya serekali. Wabunge wa vyama vyote viwili wanakubaliana kwamba deni la dola bilioni 14.3 ni jambo lisilokubalika. Lakini kile kitisho kwamba mashauriano hayo yaliokuwa magumu yangelipeleka taifa liangukie kwenye mzozo wa kifedha na kiuchumi- jambo ambalo litakuwa na athari kwa dunia- liliwafanya wabunge wa Chama cha Republican wasiweze kujitenge na njia iliopendekezwa. Mwanzoni ilikuwa sio wazi kwao juu ya matokeo yatakavokuwa.

Rais Obama naye ameregeza kamba. Muwafaka huo sasa unaonekana vingine kuliko vile alivotaka yeye mwenyewe; kwa sasa kodi hazitapandishwa, lakini jambo hilo linaweza kufanyiwa mashauriano na tume isioelemea chama chote cha kisiasa. Muhimu ni kwamba serekali imeweza kuepushwa isishindwe kukopa, na mwishowe yaweza kusiweko ile haja ya serekali kupunguziwa uwezo wake wa kuchukuwa madeni. Hiyo inatokana na kwamba Rais Obama amefaulu kukipandisha sana kiwango cha juu kabisa cha kuweza kukopa, hivyo sarakasi kama hii ya kisiasa haitoweza kabisa kurejewa mnamo mwaka mmoja na nusu ujao. Mara nyingine dunia haitoshuhudia sarakasi kama hii bila ya kuweko athari nyingine.

Jambo lolote lingine ambalo halitakuwa la kulikubali suluhisho hili itamaanisha maafa. Hiyo itakuwa kufikisika kwa viongozi wa vyama vya kisiasa, hasa yule wa chama cha Republican, John Boehner, ambaye katika wiki zilizopita hasa hajapendeza mbele ya watu. Tutaraji kwamba mzozo huu wa wiki zilizopita ambao viongozi wa Marekani wamejitakia wenyewe utamalizika na kwamba serekali na bunge zitauondosha mkwamo ulioko: nao ni ukosefu wa kazi, madeni makubwa yanayodaiwa serekali na uchumi ulio dhaifu. Ni wakati umefika sasa.

Mwandishi: Bergmann, Christina/ Othman, Miraji/ZR

Mhariri: Miraji Othman

 • Tarehe 01.08.2011
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/128Ok
 • Tarehe 01.08.2011
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/128Ok

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com