1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Obama aionya Syria

27 Aprili 2013

Rais wa Marekani Barrack Obama, ametoa onyo jipya kwa Syria kwamba matumizi ya silaha za maangamizi makubwa dhidi ya raia nchini humo huenda likapelekea kubadilisha msimamo wa Marekani juu ya kuingilia kijeshi Syria.

https://p.dw.com/p/18O96
Rais wa Marekani BarrackObama
Rais wa Marekani BarrackObamaPicha: picture-alliance/dpa

Obama ametoa onyo hilo wakati akiwa anakabiliwa na shinikizo kutoka nchini mwake na bara la ulaya kwa ujumla kuingilia mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.

Hata hivyo siku moja baada ya Marekani kusema kwamba kemikali hizo zenye sumu huenda zimetumika kwa kiwango kidogo, Obama anasema nchi yake lazima iwe na uhakika wa matumizi ya silaha za kemikali, na ushahidi unaoonyesha silaha hizo zimetumika kivipi na wapi.

" Tumeshawahi kuona picha mbaya sana zamani, baada ya maafisa wa ulinzi wanaoonekana kufanya maamuzi kutokana na maswala ya sera, na baadaye inakuja kubainika kuwa ushahidi iliopelekea maamuzi hayo kufanywa si wa ukweli ," alisema afisa mmoja wa ulinzi nchini Marekani ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Raia wa Syria akivalia kifaa cha kumkinga na kemikali ya sumu
Raia wa Syria akivalia kifaa cha kumkinga na kemikali ya sumuPicha: JM LOPEZ/AFP/Getty Images

Afisaa huyo alikuwa akitoa mfano wa namna Marekani ilivyoiingilia kijeshi nchini Iraq baada ya kugundua kuwa silaha za maangamizi yenye nguvu zinatumika katika ghasia za nchi hiyo madai ambayo baadaye yalisemekana sio ya kweli. Katika ghasia hizo za mwaka 2003, wanajeshi 4,500 wa Marekani waliuwawa huku raia wengi wa Iraq pia wakipoteza maisha yao.

Syria yakana madai ya kutumia silaha za kemikali

Huku hayo yakiarifiwa, serikali ya Syria imetupilia mbali madai kwamba ilitumia silaha za kemikali dhidi ya waasi nchini humo ikisema kwamba habari hizo ni za uwongo na za kupangwa.

Kulingana na shirika la habari la Syria Sanaa, waziri wa habari wa Syria Omran al-Zoabi amesema madai yanayotolewa na nchi hizo za Magharibi hayana msingi wowote.

Rais wa Syria Bashar al-Assad.
Rais wa Syria Bashar al-Assad.Picha: DSK/AFP/GettyImages

Awali, Rais Obama alimwambia rais wa Syria Bashar Al Assad kwamba utumiaji wa silaha hizo ni kuvuka mipaka ya sheria za kimataifa, na hilo ndilo litakalobadilisha msimamo Wa Marekani juu ya kuiingilia kijeshi nchi ya Syria. Mwezi uliopita serikali ya Bashar Al Assad pamoja na waasi walianza kushutumiana juu ya matumizi ya silaha za kemikali katika eneo la Khan al Assal kaskazini mwa mji wa Allepo.

Umoja wa Mataifa waanza uchunguzi

Kwa sasa Umoja wa Mataifa umeandaa kundi la wajumbe wake kuchunguza madai hayo lakini utawala wa Syria umekataa kutoa nafasi kwa wajumbe hao kuingia nchini humo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon, ameandika barua kwa Rais Assad ili aridhie wajumbe wake kuingia na kuanzisha uchunguzi.

Kwa upande wake Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa wachunguzi wa umoja huo wameshaanza kukusanya ushahidi nje ya Syria, juu ya madai ya kutumika silaha za kemikali. Kulingana na Umoja wa Mataifa, tangu kuanza kwa mapigano nchini Syria miaka miwli iliopita takriban watu 70,000 wameuwawa huku wengine wengi wakikimbilia nchi jirani.

Mwandishi:Amina Abubakar/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga