1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Obama aanza ziara yake ya mashariki ya kati nchini Saudi Arabia.

Sekione Kitojo3 Juni 2009

Rais wa Marekani Barack Obama anaanza ziara yake ya kwanza katika eneo la mashariki ya kati tangu kushika madaraka leo Jumatano kwa kwenda nchini Saudi Arabia.

https://p.dw.com/p/I2gc
Rais Barack Obama akielekea katika ndege ya Air Force One katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dulles akielekea Saudi Arabia kuanza ziara yake ya mashariki ya kati.Picha: AP

Rais wa Marekani Barack Obama anaanza ziara yake ya kwanza katika eneo la mashariki ya kati leo Jumatano, akitafuta kuungwa mkono kwa juhudi zake za kufufua hatua za kuleta amani , na wakati huo huo mvutano ukijengeka taratibu kati ya nchi hiyo na mshirika wake mkubwa Israel.

Kilele cha ziara hii kitakuwa hotuba inayosubiriwa kwa shauku kubwa , na mataifa ya Kiislamu na Waislamu kutoka mjini Cairo, lakini Obama pia atajaribu kutafuta njia za kufufua utaratibu wa amani ya kimkoa uliokwama.

Anatarajiwa kutua kwanza nchini Saudi Arabia kwa mazungumzo na Mfalme Abdullah ambaye amekuwa akijaribu kuanzisha upya juhudi zinazoungwa mkono na mataifa ya Kiarabu za kuleta amani, na baadaye kuelekea Misr hapo kesho ambako atakutana na rais Hosni Mubarak.

Obama amesema kuwa atagusia hatua za kuleta amani katika mashariki ya kati katika hotuba yake atakayoitoa katika chuo kikuu mjini Cairo, ikiwa ni juhudi za jumla kujenga daraja kati ya mataifa ya magharibi na Waislamu, lakini hatatoa mpango kamili.

Kwa mataifa ya Kiislamu , tunatafuta njia mpya ambayo itakuwa na maslahi kwetu sote , na kuheshimiana.


Ikulu ya Marekani imeahidi kufanya kila linalowezekana , kwa kutumia uwezo uliopo wa teknolojia na mawasiliano kuhakikisha kuwa watu wengi zaidi wanaona na kusikia hotuba hii ya kihistoria.

Katika mkesha wa ziara yake hiyo hata hivyo kiongozi wa pili katika kundi la kigaidi la al-Qaeda Ayman al-zawahiri amewaambia Wamisr kujitenga na Obama, akisema kuwa ziara yake imetokana na wale wanaowatesa Wamisr pamoja na watumwa wa Marekani.

Ujumbe wake wa kipuuzi unapokelewa na bado unaendelea kupokewa na Waislamu, na hautafichwa na kampeni za uhusiano mwema ama ziara za mzaha ama maneno matamu, amesema Zawahiri.

Hata hivyo Obama anaonekana kuwa ana nafasi ya kipekee miongoni mwa viongozi wa Marekani kuweza kujipenyeza katika mataifa ya Kiislamu.

Obama amesema kuwa ana matumaini ya kufufua mazungumzo kati ya Israel na Palestina, lakini Ikulu ya Marekani imekuwa ikisita sita kuhusiana na mkakati wake huo , kutokana na mikutano kadha na viongozi wa kimkoa katika wiki za karibuni.


Kitu ambacho ni kigumu sana kila siku kukihimiza ni uvumilivu. Na diplomasia kila mara huchukua muda mrefu na sio suala la kupata matokeo ya haraka.


Israel kwa upande wake inamatumaini kuwa hotuba ya rais Obama ya mapatano na mataifa ya Kiislamu haitahatarisha taifa hilo la Kiyahudi. Rais wa Marekani ana haki ya kutaka mapatano na mataifa ya Kiislamu na kushindana na al-Qaeda ama Iran katika juhudi za kukubalika, amesema waziri wa usafirishaji wa Israel Yisrael Katz, mshirika wa karibu wa waziri mkuu Benjamin Netanyahu.

Marekani ikijaribu kupambana na kuenea kwa wapiganaji wa Taliban katika mipaka ya Afghanistan na Pakistan inaigeukia Saudi Arabia kupata msaada. Lakini hadi sasa ufalme huo unaonekana kuchukua tahadhari ya kutumbukia katika mzozo huo.

Kwa mujibu wa Mark Lippert, naibu mshauri wa masuala ya usalama wa taifa nchini Marekani , Pakistan itakuwa katika ajenda wakati rais Obama atakapokutana na mfalme wa Saudia , Abdullah mjini Riadh leo Jumatano.

►◄