1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Musharraf ateua Waziri Mkuu mpya

Tuma Provian Dandi16 Novemba 2007

Rais Perves Musharraf amefanya uteuzi mpya wa Waziri Mkuu ili kujaribu kurejesha utawala bora unaoliliwa na raia wengi wa Pakistan

https://p.dw.com/p/CIme
Rais Perves Musharraf wa Pakistani na maswahiba wake
Rais Perves Musharraf wa Pakistani na maswahiba wakePicha: AP

Rais Perves Musharraf amemteua Bwana Mohamedmian Soomro kuwa Waziri Mkuu mpya wa Pakistan, yakiwa yamepita majuma mawili tangu alipotangaza hali ya hatari.

Kabla ya uteuzi huo Bwana Soomro alikuwa ofisa mstaafu wa Benki moja ya kimataifa, ambaye baada ya kustaafu alishika wadhifa wa uenyekiti wa Bunge la Pakistani miaka minne iliyopita.

Kazi ya kwanza ya Waziri Mkuu huyo mpya aliyechukua nafasi ya Bwana Shaukat Aziz, itakuwa kurejesha nchi katika hali ya usalama baada ya kipindi cha hali ya hatari, mpaka utakapofanyika uchaguzi wa Bunge hapo mwezi Januari mwakani.

Hata hivyo mmoja wa wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini humo Bwana Hassan Askari amesema uteuzi huo wa Waziri Mkuu mpya ni sawa na kiinimacho na kwamba anayeweza kurejesha amani na utulivu ni Rais Musharraf mwenyewe kwa kuwa ana kila dhamana mkononi mwake.

Mchambuzi huyo ameongeza kwa kusema kwamba hata kama Rais Musharraf atamteua mtu wa namna wa gani kuwa Waziri Mkuu, asipoamua kufanya mabadiliko yeye mwenyewe akiwa ni rais, hakuna kitakachowezekana.

Bwana Soomro mwenye umri wa miaka 57 ni miongoni mwa wanachama maarufu na mwenye msimamo katika chama tawala cha Pakistan Muslimu Leaque Party, na anasemekana kuwa mshirika wa karibu na Rais Perves Musharraf.

Waziri Mkuu huyo mpya pia ni kiongozi mkuu wa kabila la Soomro lililoko katika jimbo la Sindh huko kusini mwa Pakistani, na anatoka kwenye familia maarufu katika masuala ya kisiasa.

Anasemekana kuwa na uzoefu mkubwa katika masuala ya uhusiano, utetezi wa jamii na ana sifa ya kuwa mzungumzaji mzuri anayeweza kutatua matitizo makubwa ya kijamii kwa njia ya majadiliano.

Wakati Rais Perves Musharraf akifanya uteuzi huo wa Waziri Mkuu mpya, pia ameondoa amri ya kumzuia nyumbani kwake Waziri Mkuu wa zamani Bibi Benazir Bhutto.

Bibi Bhutto alizuiwa nyumbani kwake mjini Lahore wiki iliyopita baada ya kuendesha maandamano na mikutano mikubwa iliyokuwa na lengo la kumshinikiza Rais Musharraf kuondoa hali ya hatari, na kurejesha amani na demokrasia.

Kamanda wa Polisi mjini Lahore Aftab Cheema, amesema Bibi Bhutto yuko huru kwenda kokote baada kuzuiwa nyumbani kwake kwa juma zima, lakini hadi sasa maofisa kadhaa wa usalama wameendelea kuonekena nje ya nyumba yake.

Wakati Rais Musharraf akimwachia huru Bibi Benazir Bhutto, maofisa wengine wa serikali wakiwemo wanasheria, mahakimu na majaji bado wanashikiliwa na vyombo vya usalama.

Wakati hayo yakiendelea, ujumbe wa serikali ya Marekani ukiongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya nje John Negroponte umewasili nchini Pakistani kwa ajili ya kutuliza mambo.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya kisiasa, Marekani imeshindwa kumwajibisha Rais Perves Musharraf kwa kuwa ni mshirika wake wa karibu katika masuala ya kupambana na ugaidi lakini Rais George Bush anamtaka Jenerali Musharraf kuachia cheo cha ukuu wa majeshi ili abakie kuwa Rais wa kiraia.