1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Musharraf acheza kamari ya kisiasa.

Mohamed Dahman24 Juni 2007

Kwa mtu ambaye aliwahi kusema kwamba mkakati wake wa kamari ni kuweka dau mara tatu au kun’gatuka Rais Pervez Musharraf anakabiliwa na kamari kubwa kabisa ya maisha yake ya kisiasa katika utaratibu wa uchaguzi uliopangwa kufanyika nchini Pakistan baadae mwaka huu.

https://p.dw.com/p/CHCJ
Rais wa Pakistan Generali Pervez Musharraf.
Rais wa Pakistan Generali Pervez Musharraf.Picha: AP

Kabla ya kuingia kwenye malumbano na hakimu mkuu wa Pakistan hapo mwezi wa Machi ilionekana mshirika huyo wa Marekani Musharraf angelishinda kipindi kengine cha miaka mitano kwa ulaini kuwa rais wa taifa hilo tete lenye nguvu za nuklea.

Musharraf alikuwa na mpango wa kuchaguliwa tena unaojulikana kama Mpango A kwa kudhani kwamba vurugu zilizozuka kutokana na kusimamishwa kazi kwa Hakimu Mkuu Iftikhar Chaudhry zitamalizika.

Lakini kutokana na kushindwa kudhibitti vurugu hizo generali huyo ambaye ameingia madarakani katika mapinduzi ya mwaka 1999 anatafakari kwa haraka maamuzi ya kuchukuwa ikiwa ni pamoja na Mpango B wa kuitisha uchaguzi na mapema ikiwezekana hata mwezi wa Septemba.

Ni wachambuzi wachache wa mambo wanaona Musharraf anaweza kuanguka madarakani lakini wote wanamuona kwamba ni mtu aliejeruhiwa kutokana na hatua mbali mbali za makosa alizochukuwa.

Mpango A unahusu kuyahusisha mabaraza ya bunge ya taifa na majimbo kumpa mamlaka mpya wakati bado akiwa ni mkuu wa majeshi hapo mwezi wa Septemba au Oktoba.Baadae mabaraza hayo yatavunjwa kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaotazamiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Wachambuzi wa mambo wanatuhumu kwamba dhamira ya kumn’gowa Chaudhry ilikuwa ni hofu kwamba angeliruhusu changamoto za kupinga mkakati wa Musharraf wa kutaka kuchaguliwa tena.

Mpango B ambao hivi sasa unazingatiwa inamaanisha kwamba kuitisha uchaguzi na mapema ambapo baadae ataweza kuomba kupatiwa mamlaka ya kuongoza nchi wakati bado akiwa ni mkuu wa majeshi kutoka mabaraza ya bunge.

Ayaz Amir mchambuzi wa kisiasa anaeheshimika ameandika kwenye gazeti la Dawn hivi karibuni kwamba uamuzi huo utahitaji moyo na dira akitabiri kwamba utasafisha hali ya hewa ya kisiasa, kutuliza mvutano na kuondowa nadhari kutoka kwa Musharraf kwa kuwa vyama vyote vitakuwa vimehusika.

Tatizo ni kwamba Musharraf anahofu kwamba chama tawala nchini Pakistan cha Pakistan Muslim League chama ambacho kimeunganishwa pamoja kufuatia mapinduzi yake kitashindwa vibaya katika uchaguzi mkuu.

Kuna tetesi nzito kwamba Musharraf atajaribu kuondokana na kutengwa kisiasa na kujipatia awamu ya pili ya urais kwa kufikia maelewano na hasimu wake wa zamani Benazir Bhutto kwa kumruhusu mwanamke huyo aliewahi kuwa waziri mkuu mara mbili kurudi nchini Pakistan baada ya kuishi uhamishoni kwa hiari kwa takriban muongo mmoja.

Vipi Pakistan itaibuka kutoka mikingamo hiyo ni suala lenye utashi mkubwa kwa Marekani,serikali za mataifa ya magharibi na hasimu yake India ambaye ni mshirika wa Pakistan katika mchakato wa amani wa miaka mitatu.

Kile kitakachotokea katika wiki chache zijazo kwenye Mahkama Kuu ambayo inategemewa kumaliza kusikiliza ombi la hakimu mkuu kupinga uadilifu wa kesi dhidi yake kutayakinisha Musharraf atachukuwa maamuzi gani.