1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Mugabe amtaka Tsvangirai akubali kuapishwa kuwa waziri mkuu

Saumu Mwasimba19 Desemba 2008

Jumuiya ya kimataifa inazidi kumshinikiza ajiuzulu madarakani

https://p.dw.com/p/GJrJ
"Asema hatishwi na nchi za magharibi na wala hang'atuki madarakani''Picha: picture-alliance/ dpa

Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe Morgan Tsvangirai ametishia kujiondoa kwenye mazungumzo ya kugawana madaraka na rais Mugabe ikiwa serikali haitokoma kuwahangaisha na kuwakamata wapinzani wake wa kisiasa.

Wakati huohuo Umoja wa mataifa unasema kwamba idadi ya watu waliokufa kutokana na maradhi ya kipindi pindu nchini humo imeongezeka na kufikia watu 1,123 na wengine zaidi ya elfu 20 wakiwa tayari wameambukizwa maradhi hayo.

Rais Robert Mugabe amesema hakuna hata nchi moja ya kiafrika inayoweza kumuondoa madarakani.Gazeti linalomilikiwa na serikali la Herald limenukuu kiongozi huyo akiwaambia viongozi wa chama chake kwamba mwito wa Botswana wa kutaka aondolewe madarakani sio chochote bali ni maneno matupu.Aidha amesema wakati mzuri utafika kwa wazimbabwe licha ya kwamba wananchi wanakabiliwa na njaa,gharama za maisha,utekaji nyara wa wapinzani na janga la maradhi ya kipindupindu.

Gazeti hilo ambalo ni mdomo wa serikali limenukuu kiongozi huyo akiomba msahama wananchi kwa ukosefu wa chakula unaoshuhudiwa katika taifa hilo akisema serikali imeagizi unga wa mahindi na kwamba utaanza kugawanywa kwa wale walioathirika zaidi.Huku hayo yakijiri benki kuu ya taifa hilo imetoa noti mpya ya dolla billioni 10 katika juhudi za kukabiliana na mfumko mkubwa kabisa wa bei kuwahi kushuhudiwa katika taifa hilo.

Jumuiya ya kimataifa nayo inazidi kumshinikiza rais Mugabe angatuke madarakani,waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown amewataka viongozi wa nchi za kusini mwa Afrika kujitenga na Muagabe huku akisema kwamba hali ya zimbabwe ni msiba mkubwa kabisa.Akizungumza katika mkutano wa kila mwezi na vyombo vya habari Brown amesema nchi hizo jirani ya Zimbabwe zinapasa kujitokeza wazi kuunga mkono upande wa upinzani ambao ulishinda uchaguzi wa urais wa duru ya kwanza mapema mwaka huu.

Katika kipindi cha wiki za hivi karibuni viongozi mbali mbali wa dunia wamekuwa wakimshinikiza rais Mugabe ang'atuke uongozini huku baadhi ya viongozi wa kisiasa katika baadhi ya nchi za kiafrika wakitoa mwito wa kupelekwa wanajeshi kuutatua mzozo wa Zimbabwe.

Miongoni mwa viongozi waliotoa mwito huo ni pamoja na waziri wa mambo ya nje wa Bostwana na waziri mkuu wa Kenya.Lakini viongozi wengi wa Afrika wanaonekana kutokubaliana na mwito huo,majirani wa Zimbabwe haungi mkono pendekezo hilo ikiwemo Afrika Kusini kama alivyoweka wazi Jacob Zuma kiongozi wa chama tawala cha ANC.

Kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai ametishia kujiondoa katika mazungumzo ya kugawana madaraka ikiwa serikali itaendelea kuwateka nyara wafuasi wake.Kitisho hicho kimekuja huku jumuiya ya kimataifa ikizidi kuingiwa na wasiwasi juu ya kusambaa kwa maradhi ya kipindu pindu pamoja na miito ya kumtaka Mugabe ajiuzulu.

Pamoja na hayo lakini rais Mugabe amewambia wanachama wake kwamba Zimbabwe ni nchi yake na kamwe hatosalimu amri na kwamba hatishwi na miito hiyo ya kumtaka ajiuzulu.Na tukimnukulu rais Mugabe alisema'' Sitishiki,na hata kama nikitishwa kwamba nitakatwa kichwa naamini kwamba sitotishika na hakuna kitu kitakachonifanya niondoke madarakani,Zimbabwe ni nchi yetu sio ya waingereza''Mwisho wa kumnukulu rais Mugabe.

Nchi za ulaya ya kaskazini kama vile Denmark,Iceland,Norway na Sweden pia zimemtaka Mugabe ajiuzulu wakimtwika lawama kuhusiana na hali ya mambo katika taifa lake.