1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais mpya ashika madaraka nchini Libanon

P.Philipp/P.Martin26 Mei 2008

Baada ya bunge kushindwa mara 19 kumchagua rais mpya bila shaka kuna sababu ya kuwa na furaha ya kiwango fulani na sio miongoni mwa Walibanon tu.

https://p.dw.com/p/E68c
Michel Suleiman is sworn in as the new president at the Parliament in Beirut, Lebanon, Sunday, May 25, 2008. Suleiman was sworn as Lebanon's president Sunday after parliament elected him in long-delayed vote that was a key step toward restoring political stability. (AP Photo/Nabil Mounzer, Pool)
Michel Suleiman akiapishwa kama rais mpya wa Libanon katika bunge mjini Beirut,Jumapili 25 Mei 2008.Picha: DW

Miezi minane iliyopita haijakwamisha tu utaratibu wa kikatiba nchini Libanon bali ulionyesha pia jinsi mzozo wa kisiasa wa nchi hiyo,ulivyohatarisha kuitumbukiza nchi katika vita vipya vya wenyewe kwa wenyewe kama ilivyoshuhudiwa mwaka 1975 hadi 1990.Hatari hiyo hasa ilidhihirika hivi karibuni yalipozuka mapigano mapya.

Kuchaguliwa kwa Michel Suleiman aliekuwa mkuu wa majeshi mpaka hivi sasa, kumemaliza mgogoro wa kisiasa.Lakini hiyo ni hatua muhimu ya kwanza tu kujitoa kwenye janga la migogoro kama ilivyokubaliwa na makundi hasimu chini ya uongozi wa Umoja wa nchi za Kiarabu na hasa Qatar.Makubaliano hayo yalitiwa saini Doha nchini Qatar juma lililopita.

sasa ndio makubaliano mengine yaliyopatikana yanahitaji kutekelezwa pia au sivyo yale yaliyozuka hivi karibuni nchini humo huenda yakashuhudiwa upya.Na njia ya kujitoa kutoka janga la migogoro haimtegemei rais binafsi au vile atakavyoongoza majadiliano,bali vipi makundi yote husika yatakavyokuwa tayari kutumia busara.

Kwanza kabisa kuundwe serikali mpya itakayowakilishwa na wajumbe wa serikali ya zamani ya waziri mkuu Fouad Siniora, iliyoelemea kambi ya magharibi na pia wafuasi wa upinzani wanaoungwa mkono na Syria na Iran.Wajumbe hao hawana budi kuketi pamoja katika baraza la mawaziri.Bila shaka hilo si jambo rahisi baada ya kundi la Hezbollah na upinzani wa Wakristo walioongozwa na jemadari wa zamani Michel Aoun kuilaani serikali ya mseto kati ya Wakristo,Wasunni na Wadruze na kushikilia kuwa ijiuzulu.

Makundi yaliyohitilafiana kutaka kuunda serikali kwa pamoja ni "demokrasia mfumo wa Kilibanoni."Si hilo tu bali kundi lililokuwa upande wa upinzani,ingawa ni dogo sasa litakuwa na kura turufu na hivyo litaweza kuzuia maamuzi muhimu kupitishwa ingawa ni wingi wa theluthi-mbili unaohitajiwa.Kwa mara nyingine tena,Libanon imezindua mfumo wa bandia wa kuwiana,kwa maslahi ya amani lakini wakati huo huo kuna hatari ya mizozo kuripuka wakati wo wote ule.

Serikali ya Libanon inapaswa kupitisha maamuzi muhimu yatakayosaidia kuleta maendeleo nchini humo.Kwa mfano,vipi serikali kuu itakavyodhibiti nchi nzima - kwa maneno mengine,vipi Hezbollah inyanganywe silaha zake.Hadi hii leo hilo ni kundi pekee la wanamgambo ambalo rasmi hudhibiti silaha,kwani serikali haikutaka mapambano na hata jeshi lililokuwa chini ya uongozi wa Jemadari Suleiman halikutaka kuingilia kati.Sababu si kama ilivyoelezwa mara kwa mara kuwa jeshi halielemei upande wo wote,bali lilitambua hatari ya jeshi kusambaratika iwapo lingeingilia kati mgogoro wa ndani wa nchi hiyo.Kwa hivyo, kuchaguliwa kwa rais mpya kunatoa matumaini lakini hakuna sababu ya kuwa na furaha kubwa hivyo.