1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Lansana Contê anataka sheria za Kijeshi ziongezewe muda

23 Februari 2007

Vyama vya upinzani nchini Guinea vimelalamikia hatua ya rais Lansana Contê kutaka kurefusha sheria za kijeshi ambazo wanasema zinalenga kuukandamiza upinzani.

https://p.dw.com/p/CHJL
Rais Lansana Contê wa Guinea
Rais Lansana Contê wa GuineaPicha: AP

Vyama vya upinzani na vile vya wafanyakazi vimetishia kuendelea na mgomo wao hadi pale rais Contê atakapomtangaza waziri mkuu mpya.

Rais Lansana Contê aliwasilisha jana bungeni ombi la kutaka muda wa hali ya hatari uongezwe katika taifa hilo la Afrika Magharibi. Bunge la Guinea linajadili pendekezo hilo la rais Contê leo hii.

Hali hiyo ya hatari ilitangazwa nchini Guinea tangu siku 10 zilizopita kukabiliana na vurugu dhidi ya utawala wake.

Jeshi lilipewa nguvu zaidi na likatangaza hali ya kutotoka nje kutwa, kucha. Amri za kijeshi hadi sasa zimefaulu kudhibiti hali ya utulivu nchini humo.

Mpatanishi wa upande wa upinzani Bobacar Biro Barry amelieleza shirika la habari la Reuters kabla ya kukutana na wapatanishi wa Afrika magharibi kwamba hatua ya rais Contê itazidisha tu ari yao ya kuendeleza muungano wao wa upinzani.

Barry na viongozi wengine wa upinzani wanatarajiwa kukutana na rais wa zamani wa Nigeria jenerali Ibrahim Babangida anaeongoza ujumbe wa wapatanishi kutoka Umoja wa nchi za Afrika Magharibi ECOWAS ili kutafuta suluhisho la mzozo huo.

Viongozi wa upinzani wanadai kwamba rais Lansana Contê ambaye yumo katika miaka ya sabini ajiuzulu kutoka madarakani baada ya kutawala kwa kipindi cha miaka 23, walianza madai yao hayo pale rais Contê alipomchagua rafiki yake wa karibu Eugene Camara kuchukuwa wadhfa wa uwaziri mkuu licha ya kuwepo makubaliano ya awali kwamba angemchagua mtu aliyekubalika na pande zote.

Takriban watu laki 120 wasio na silaha wameuwawa tangu mwanzoni mwa mwaka huu nchini Guinea kufuatia vurugu kati ya raia na walinda usalama.

Hali ya nchini Guinea imezua wasiwasi kwamba huenda machafuko hayo yakaathiri usalama wa eneo zima na hasa katika nchi jirani za Sierra Leone na Liberia ambazo ndio kwanza zinajikwamua kutoka kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Rais Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia amemshauri rais Contê ashirikiane na vyama vyote ili kuzuia mfarakano wa kisiasa utakao sababisha umwagikaji wa damu na kuzitia nchi jirani katika hali ya wasiwasi.

Bibi Sirleaf aliyasema hayo huko nchini Rwanda ambako anahudhuria mkutano wa wanawake katika mji wa Kigali.

Hivi karibuni balozi wa Guinea nchini Liberia aliwasilisha malalamiko yasiyo rasmi mjini Monrovia, kwamba kuna makundi ya wapiganaji nchini humo yanayotayarishwa kuishambulia Guinea, madai ambayo rais Ellen Johnson Sirleaf aliahidi kuyashughulikia na kuliahidi taifa jirani kuwa hatokubali umwagikaji damu utendeke.

Na wakati huohuo katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki Moon anatarajiwa kutuma ujumbe maalum nchini Guinea kutafuata njia za kutatua mzozo unaoendelea kuwa mkubwa katika taifa hilo la Afrika ya Magharibi.