1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Kagame ziarani Ufaransa

13 Septemba 2011

Rais Paul Kagame wa Rwanda amezungumzia kuhusu kufungua ukurasa mpya katika uhusiano wa nchi yake na Ufaransa wakati wa mazungumzo na rais Nicolas Sarkozy mjini Paris.

https://p.dw.com/p/12Xq1
Rais Paul Kagame wa Rwanda ameonya dhidi ya mataifa ya kigeni kuwa na fikra za kuitawala Afrika.Picha: picture-alliance/dpa

Rais wa Rwanda Paul Kagame amezungumzia kuhusu kufungua ukurasa mpya katika uhusiano wa nchi yake na Ufaransa wakati wa mazungumzo yake na rais Nicolas Sarkozy mjini Paris jana.Kagame leo yuko katika siku yake ya pili ya ziara nchini humo.

Ziara ya kwanza ya kiongozi huyo wa Rwanda tangu kutokea mauaji ya kimbari mwaka 1994 , rais Paul Kagame amesisitiza kuwa ziara yake ilikuwa na lengo la kujenga upya mahusiano ya kiuchumi na kibiashara.

Kagame amewaambia waandishi habari kuwa kwa kufanya ziara hiyo , tunaangalia mbele badala ya kuangalia yaliyopita.

Kagame alianza ziara yake ya kwanza nchini Ufaransa siku ya Jumapili tangu pale yalipofanyika mauaji ya kimbari mwaka 1994, ambapo uchunguzi rasmi wa Rwanda mwaka 2008 uliwahusisha maafisa wa Ufaransa pamoja na majeshi ya nchi hiyo katika mauaji hayo.Lakini licha ya ziara hiyo ya kuleta uhusiano mwema kati ya Rwanda na Ufaransa, baadhi ya raia wa Rwanda wanaoishi nchini Ufaransa waliandamana kuipinga ziara hiyo , wakimshutumu rais Kagame kwa kukiuka haki za binadamu.

Waziri wa biashara na viwanda nchini Rwanda , Francois Kanimba , mmoja kati ya mawaziri kadha walioongozana na rais Kagame katika ziara hiyo , amesema kuwa Rwanda ina pendelea zaidi kufanyakazi na Ufaransa katika kuendeleza miradi ya nishati inayotokana na maji, maeneo yanayotoa nguvu za umvuke wa maji pamoja na gesi ya methane pamoja na kupanua mfumo wa ugavi wa umeme nchini humo.

Katika taarifa Sarkozy amesema ziara hiyo inaashiria hatua mpya katika hatua ya kujenga uhusiano ambao uko katika misingi ya majadiliano na kuheshimiana.

Belgien EU Gipfel Nicolas Sarkozy in Brüssel
Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy amekiri kuwa Ufaransa imeshindwa kwa nchi yake kutambua mauaji ya kimbari.Picha: dapd

Shirika la maendeleo la Ufaransa litaongeza msaada wake kwa makampuni ya ukubwa wa kati na madogo nchini Rwanda, amesema rais Sarkozy.

Kabla ya kukutana na rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy , Kagame alizungumza katika taasisi moja ya Ufaransa, ambako alionya mataifa makubwa ya nje dhidi ya kile alichokieleza kama ni kujaribu kuitawala Afrika na kushutumu fikra hizo za kila wakati kuwapima Waafrika bila ya kuheshimu matakwa ya watu wa Afrika.

Kagame amesema baada ya kula chakula cha mchana pamoja na rais Sarkozy kuwa viongozi hao wawili walijadiliana mipango ya ushirikiano wa kiuchumi kama njia ya kuimarisha uhusiano wao. Ameongeza kuwa Wafaransa wako huru kuwekeza nchini Rwanda, katika utalii, miundo mbinu, na Wanyarwanda watafurahi kufanya biashara nchini Ufaransa.

Mkutano kati ya rais Kagame na Sarkozy umewezesha kufufua uhusiano kati ya nchi hizo mbili, ambazo zimekuwa zikinyosheana vidole kuhusiana na mauaji ya kimbari katika miaka ya hivi karibuni.

Katika mwaka 2008, Rwanda iliishutumu Ufaransa kwa kuwapa mafunzo wanamgambo wa Kihutu ambao waliwauwa Watutsi 800,000 pamoja na Wahutu waliochukua msimamo wa kati, na kulishutumu jeshi la Ufaransa kuwa limehusika moja kwa moja katika mauaji hayo. Ufaransa ilikana madai hayo. Wakati wa ziara yake nchini Rwanda mwaka jana , Sarkozy amekiri kuwa Ufaransa ina kubali makosa kutokana na kutoweza kuliangalia kwa makini suala la mauaji ya kimbari. Mtazamo wa Ufaransa kwa Rwanda ulijengeka katika uchunguzi wa Aprili 6, 1994, ilipoangushwa ndege iliyokuwa imemchukua rais Juvenal Habyarimana. Mauaji hayo yalionekana kwa kiasi kikubwa kuwa ndio yaliyozusha mauaji ya kimbari nchini Rwanda.

Mwandishi : Sekione Kitojo / ape/dpae/rtre

Mhariri:Abdul-Rahman,Moahammed