1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Rais Köhler ataka sera za kimataifa za maendeleo

Ilikuwa miaka kumi iliyopita pale rais wa zamani wa Ujerumani, Bw. Roman Herzog, alipotoa hotuba maarufu ya Berlin na kudai Ujerumani iendelee mbele haraka. Tangu wakati huo imegeuka mila kwa rais wa nchi hii kutoa hotuba kubwa kila mwaka. Leo hii, ilikuwa zamu ya rais Horst Köhler naye alitumia vizuri nafasi yake pale alipolaumu juu ya ukosefu wa usawa si Ujerumani wala duniani katika enzi hii ya utandawazi.

Rais Horst Köhler

Rais Horst Köhler

“Kupanda kwa watu fulani kusiwasababishe wengine kushuka chini katika maisha yao.” Haya aliyasema rais Horst Köhler wa Ujerumani katika hotuba aliyoitoa adhuhubri ya leo mjini Berlin. Köhler alitoa mwito kugawa faida na hasara kwa usawa akionya kwamba licha ya kuwa na watu wengi kwenye tabaka la kati na kati wanaonufaika kutokana na kupanda kwa uchumi wengine wenye mishahara ya chini au hawana ajira kabisa watategemea misaada. Wakati huo huo, Rais Köhler alijaribu kuwapa moyo Wajerumani wasiogope utandawazi bali wajiingize katika mwenendo huu. Köhler alisema enzi hiyo ya utandawazi tayari imewasaidia watu wengi kuondokana na umaskini kama kwa mfano huko China ambapo tangu mwaka wa 1980 watu millioni 500 waliweza kutokana na umaskini.

Köhler amesema: “Hata ikiwa bado kuna kazi nyingi za kufanya, kimsingi utandawazi ulileta maendeleo mazuri katika nchi maskini. Kwa hivyo ni baraka kubwa kwa watu wengi.”

Hata hivyo, Rais Köhler alilaumu kuwa utandawazi pamoja na faida yake, una sura mbaya, yaani kutojali wale wasio na nguvu. Kama mfano, Köhler alisema nchi za Magharibi zinalipa Dola Billioni moja kama ruzuku kwa bidhaa za kilimo wakati zinalipia Dola Billioni moja kwa mwaka tu kama msaada kwa sekta ya kilimo barani Afrika.

Nchi za Ulaya pia hazitoi mfano mzuri alisema Köhler akitoa mfano mwingine: “Nchi za Ulaya zinavua samaki wengi mno karibu na pwani za Afrika lakini zikikosolewa zinaonyesha tu mikataba zilizoifunga na nchi husika za Kiafrika. Wakati huo huo, Ulaya inaonekana kama inastushwa, kusikia hasira juu ya idadi kubwa ya Waafrika wanaopanda boti zao ndogo na kuelekea Ulaya wakijaribu kukimbia umasikini wao.”

Rais Köhler alitoa mwito kuwa na sera mpya kama sera za ndani za dunia. Kwa ajili hiyo inabidi kuwa na mahusiano ya karibu kati ya Shirka la Fedha Duniani IMF, shirika la biashara duniani WTO, benki ya Dunia na Umoja wa Mataifa, alisema Köhler. Raisi huyu alitaka pia nchi zinazoendelea zipewe usemi zaidi katika mashirika makubwa ya kifedha.

Rais Köhler mwenyewe aliwahi kuwa mkurugenzi wa shirika la fedha ulimwenguni IMF ana anajitolea hasa kwa nchi za bara la Afrika. Katika hotuba yake alidai Ulaya ibadilishe kabisa uhusiano wake na nchi maskini kwa manufaa ya pande zote mbili, kwa sababu: “Changamoto ya kuleta maendeleo itakua huku idadi ya watu duniani inazidi kuongezeka. Watu wote hao wana haki ya kupata chakula, maji safi, elimu na maisha ya kibinadamu. Pia wana haki ya kuheshimika kama sisi tunavyotaka kuheshimika. Basi hakuna tena taifa ambalo linaweza kuhakikisha ustawi kwa wanachi wake bila ya kujali mataifa mengine.”

 • Tarehe 01.10.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CH7P
 • Tarehe 01.10.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CH7P

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com