1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Jacob Zuma aendelea kushinikizwa ajiuzulu

Amina Mjahid
12 Februari 2018

Raia wa Afrika Kusini wanataka kumalizika mkwamo wa kisiasa baada ya Rais Jacob Zuma kuendelea kubakia madarakani licha ya shinikizo za kitaifa kumtaka rais huyo mkongwe ajiuzulu kutokana na madai ya rushwa yanayomkabili

https://p.dw.com/p/2sXu8
Südafrika Präsdient  Jacob Zuma
Picha: Reuters/S. Sibeko

Kusubiri habari za hatima ya kiongozi wa moja ya mataifa yaliyoimarika kiuchumi barani Afrika, ambaye kisiasa anaonekana kuchafuka kupita kiasi kutokana na kashfa za rushwa zinazomkabili, kumezua ati ati kwamba  makamu wake, Cyril Ramaphosa, anayetarajiwa kuchukua nafasi ya Urais itakayoachwa wazi iwapo Zuma atajiuzulu, bado anajadiliana na Rais Zuma juu ya mpango watakaouchukua ili aachie ngazi.

Südafrika ANC Parteitag Zuma und Ramaphosa
Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma na Makamu wake Cyril RamaphosaPicha: Getty Images/AFP/M. Safodien

Awali Ramaphosa alisema kamati kuu ya chama tawala cha ANC inapanga kukamilisha kipindi cha kubadilishana madaraka katika mkutano wa leo Jumatatu mchana.

Hata hivyo, upande wa upinzani umetupilia mbali taarifa ambazo hazijathibitishwa kwamba Rais Zuma ameomba makubaliano ya kulindwa dhidi ya kushtakiwa, wakisema kwamba Zuma anapaswa kushitakiwa iwapo kesi ya madai ya rushwa itafunguliwa dhidi yake na kufungwa jela iwapo atapatikana na hatia

Hadhi ya Zuma, ambaye amekana kufanya makosa yoyote, imeharibika kufuatia mfululizo wa kashfa zinazomkabili. Mahakama ya Juu ya Afrika Kusini ilitoa hukumu kwamba alikiuka katiba kufuatia uchunguzi wa mamilioni ya dola yanayodaiwa kutumika kuikarabati nyumba yake binafsi, fedha zilizolipwa na serikali.

Aidha Kamisheni ya Mahakama iko karibu kuanzisha uchunguzi wa kuibwa kwa fedha za serikali na washirika wa Zuma, huku waendesha mashtaka wakitarajiwa kutangaza iwapo watayahusisha pia madai ya rushwa juu ya fedha zilizotumika katika mpango wa silaha miongo miwili iliyopita.

Misstrauensvotum Südafrika
Baadhi ya waandamanaji Afrika Kusini wanaotaka Zuma ajiuzuluPicha: Reuters/M. Hutchings

Katika mkutano huu wa leo, kamati hiyo ya kitaifa ya chama cha ANC inaweza kumtaka rais ajiuzulu kama ilivyomlazimisha Thabo Mbeki kujiuzulu wadhifa wake wa urais takribani muongo mmoja uliopita, hatua iliyotoa nafasi kwa Zuma kuingia madarakani mwaka 2009.

Lakini Zuma akigoma kujiuzulu na kukataa ombi hilo, suala hilo huenda likafikishwa bungeni, kwa hoja ya kutokuwa na imani naye. Hoja ya upinzani kama hiyo inatarajiwa kufikishwa bungeni mnamo Februari ya tarehe 22. Iwapo hoja hiyo itafanyika na wabunge wengi wakapiga kura dhidi ya Zuma, basi itabidi baraza la mawaziri lijiuzulu na kuondoa matumaini ya Ramaphosa ya kuwa na urahisi wa kukabidhiana madaraka.

Ramaphosa anatarajiwa kuwa kaimu rais wakati Rais Zuma atakapoondoka madarakani na huenda akachaguliwa na bunge kuwa rais katika uchaguzi unaopaswa kufanyika siku 30 baada ya Zuma kujiuzulu. Kuanzia wakati huo mpaka siku ya uchaguzi mkuu baadaye mwaka ujao, hautahesabiwa kama kipindi cha kwanza cha urais. Afrika Kusini inakubali mihula miwli tu ya urais.

Mwandishi: Amina Abubakar/AP/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef