1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais George W. Bush ziarani Mashariki ya kati

Philipp, Peter (DW)13 Mei 2008

Ziara ya sasa ya rais wa Marekani itasaidia kweli ?

https://p.dw.com/p/DyxE
Rais Bush akilahikiwa na waziri mkuu Olmert na rais PerezPicha: AP


Rais George W. Bush wa Marekani anaanza  ziara ya Mashariki ya kati hii leo.Anataka kushiriki katika sherehe za miaka 60 tangu dola la Israel lilipoundwa na anakusudia pia kuupa msukumo utaratibu wa amani kati ya Israel na Palastina.


Ni jaribio la tatu hili la rais Bush katika kipindi cha miezi sita iliyopita,katika juhudi zake za kuufufua utaratibu wa amani ya mashariki ya kati.November mwaka jana aliitisha mkutano wa mashariki ya kati huko Annapolis,msimu wa kiangazi akazitembelea nchi za mashariki ya kati,na leo anaelekea katika eneo hilo hilo katika jaribio lake la pili.


Katika hali ya kawaida tungesema ni ishara ya kutia moyo,kama pirika pirika kama hizo hazitokei mwishoni mwa wadhifa wake kama rais na kama hali ya mambo haikua kama hivi ilivyo katika eneo hilo.


Badala ya kuhitimisha enzi zake kwa fahari  akifanikiwa kutia njiani utaratibu wa amani uliosalia jina tuu,rais huyo wa Marekani anaonyesha kucheza na moto:Sio tuu anayatia hatarini matumaini japo haba yaliyopatikana miezi ya hivi karibuni, bali pia imani ndogo ya walimwengu kuelekea uwezo na nguvu za Marekani za kuweza hatimae kuupatia ufumbuzi mzozo wa mashariki ya kati.


Madhumuni rasmi ya ziara yake nchini Israel ,ni sherehe za miaka 60 ya kuundwa dola ya Israel,nchini Saud Arabia ,rais George w. Bush atasherehekea miaka 75 ya uhusiano wa pande mbili na nchini Misri anamtembelea rais Husni Mubarak aliyesherehekea hivi karibuni miaka 80 tangu alipozaliwa.Washirika  watatu wa Marekani katika eneo la mashariki ya kati na ambao bila yao hakuna  maendeleo yoyote yanayoweza kupatikana kati ya Israel na Palastina.


Ili kuwapa moyo wawajibike zaidi,analazimika rais George Bush kufanya mengi zaidi badala ya kuonyesha mafungamano ya kirafiki tuu.


Na shaka shaka zilizoko si za bure watu wakijiuliza kama kweli rais wa Marekani yuko tayari au anaweza kufanya kitu:


Katika kipindi kizima cha utawala wake ameshindwa rais Bush kuilazimisha Israel ifuate msimamo wa wastani kuelekea wapalastina.Amewaachia kwanza Ariel Sharon na baadae Ehud Olmert watekeleze sera zao bila ya hofu zozote,bila ya hata kujali mashaka katika daraja ya kimataifa seuze ya Marekani.Sera hizo hizo Israel inaziiendeleza mpaka leo.


Ingawa mjini Annapolis imetajwa kwamba Olmert na rais wa Palastina Mahmud Abbas wanabidi wafikie makubaliano kabla ya mwaka huu kumalizika-lakini Israel haikufanya chochote kurahisisha hali hiyo,hali ya maisha ya wapalastina katika maeneo ya ukingo wa magharibi inazidi kua duni , Israel inaendelea kujenga makaazi ya wahamiaji katika eneo hilo na Washington haisemi chochote.


Ukorofi umezidi pia tangu Hamas kunyakua  uongozi Gaza na kuripuka  vita bayana kati ya wafuasi hao wa itikadi kali na Israel.Na huko pia Washington imenyamaza kimya.Yote hayo ni kwasababu George Bush na serikali ya Olmert wanaamini mtutu wa bunduki ndio njia pekee ya kukabiliana na makundi ya itikadi kali mfano wa hili la Hamas.Mbinu za matumizi ya nguvu zimedhihirika lakini hazifai,badala yake zinazidi kuwapa nguvu wafuasi wa itikadi kali na kuwadhoofisha wale wanaopendelea amani-tunaona mfano wa Mahmoud Abbas.


Washington haifanyi chochote dhidi ya yote hayo.Badala yake imepelekea kudhoofika matumaini yaliyokuwepo-badala ya ufumbuzi wa amani,angalao basi ifafanuliwe mipaka ya dola la siku za mbele za Palastina.Kimsingi  si kazi kubwa hiyo kwasababu jumuia ya kimataifa inakubaliana mipaka ni ile ya kabla ya vita vya mwaka 1967.Lakini kama Israel itajifungamanisha na muongozo huo,kuna wanaoshuku,seuze tena waziri mkuu Ehud Olmert amezongwa vibaya sana na kashfa za kila aina.


Na hata kama muongozo huo utafuatwa bado linasalia suala lini Israel itarejea nyuma ili eneo hilo la kabla ya mwaka 1967 lirejee kua milki ya wapalastina.Hilo ni suala ambalo George w. Bush hana jibu.