1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Bush ana matumaini makubaliano ya amani Mashariki ya Kati kufikiwa mwaka huu.

Mohamed Dahman19 Mei 2008

Rais George W. Bush wa Marekani afufuwa matumaini ya mchakato wa amani Mashariki ya Kati wakati wa ufunguzi wa kikao cha uchumi duniani kuwa makubaliano ya amani ya Israel na Wapalestina yanaweza kufikiwa mwaka wa 2008.

https://p.dw.com/p/E2RP
Rais George W. Bush wa Marekani akihutubia Kikao cha Uchumi Duniani mjini Sharm El -Sheikh Misri Jumapili ya tarehe 18.05.2008.Picha: AP

Wakati mchakato huo mgumu wa amani kati ya Israel na Wapalestina ukiendelea kutowa matunda machache Bush amekuwa akihimizwa na viongozi wa Kiarabu kuyapa mazungumzo hayo msukumo mkubwa zaidi.

Akihutubia kikao hicho Bush amesema anaunga mkono kwa nguvu kuwepo kwa taifa la Wapalestina la kidemokrasia pembezoni mwa taifa la kidemokrasia la Israel na kwamba iwapo uongozi ukishajiishwa makubaliano hayo ya amani yanaweza kufikiwa mwaka huu.

Bush amesema makubaliano ya amani ni kwa maslahi ya Wapalestina.Ni kwa maslahi ya Israel, ni kwa maslahi ya mataifa ya Kiarabu na ni kwa maslahi ya dunia.Na naamini kwa dhati kwamba kutokana na uongozi na ushujaa tunaweza kufikia makubaliano hayo ya amani mwaka huu.

Rais Bush ameupa mawaidha ulimwengu wa Kiarabu juu ya kila kitu kuanzia ukandamizaji wa kisiasa hadi kunyimwa kwa haki za wanawake lakini yamekuja kugota kwenye malalamiko kwamba anaipendelea Israel katika mazungumzo ya amani yanayozorota.

Hotuba ya Bush katika bunge la Israel Knesset wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya kuundwa kwa taifa la Israel haikupokewa vizuri katika ulimwengu wa Kiarabu.Kule Bush kumwaga sifa kem kem kwa demokrasia ya Israel kumeonekana na Waarabu wengi kuwa ni ushahidi zaidi wa uungaji mkono usioyumba wa serikali ya Marekani kwa sera za dhuluma za taifa hilo la Kiyahudi dhidi ya Wapalestina.

Mfalme Abdullah wa Jordan hakuhitaji kuwa muangalifu katika kuiambia Israel na Marekani kwamba sherehe za uhuru zinakuwa hazina maana wakati watu wengine wanaendelea kubakia bila ya kuwa na taifa.

Amesema siku hasa ya kusheherekea itakuwepo hapo pale tu Wapalestina na Waisrael wote watakapoweza kusema wako huru,wako salama na yaliopita si ndwele tugange yajayo.

Maneno ya mwanzo kabisa ya Mfalme huyo katika hotuba yake kwa ufunguzi wa kikao cha uchumi duniani yameelezea shauku ya kushuhudia kuzaliwa kwa taifa la Palestina mwaka huu wa 2008.

Amesema ni muhimu kwamba mwaka 2008 haumaliziki kama ilivyokuwa mwaka 2000.

Mfalme Abdullah amesema Mashariki ya Kati leo ingelikuwa vengine iwapo kungelikuwapo na amani na utulivu kwamba taifa huru la Wapalestina lingelikuwepo na faida mbali mbali ikiwa ni pamoja na amani yenyewe,kupunguwa kwa itikadi kali, ustawi wa uchumi na kujumuishwa eneo hilo katika ulimwengu wa dunia.

Maoni kama hayo yametolewa na Rais Hosni Mubarak wa Misri akihutubua kikao hicho.

Mubarak ameseama suala la Wapalestina ni kiini cha mzozo katika eneo hilo la Mashariki ya Kati na ni muhimu katika kukabiliana na makali yake.Amesema tatizo kuu Mashariki ya Kati sio vita dhidi ya ugaidi wala demokrasia.

Zaidi ya washiriki 1,500 wakiwemo wakuu wa nchi na wafanyabiashara mashuhuri wanahudhuria mkutano huo wa Kikao cha Uchumi Duniani huku Misri nchi mwenyeji wa mkutano ikiahidi kuendelea na mageuzi ya kiuchumi licha ya kukabiliwa na changamoto kubwa zikiwemo mzozo wa chakula duniani.