1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Bush amuonya Maliki dhidi ya Iran

Mohamed Dahman10 Agosti 2007

Rais George W. Bush wa Marekani amesisitiza kwamba Iran inaidhoofisha Iraq licha ya madai ya serikali ya nchi hiyo kwa Waziri Mkuu wa Iraq Nuri al- Maliki kwamba nchi hiyo imekuwa ikisaidia kuleta usalama nchini humo.

https://p.dw.com/p/CH9n
Rais George W. Bush wa Marekani akiwa na Rais Hamid Karzai wa Afganistan huko Camp David Marekani ambapo pia alimuonya dhidi ya Iran.
Rais George W. Bush wa Marekani akiwa na Rais Hamid Karzai wa Afganistan huko Camp David Marekani ambapo pia alimuonya dhidi ya Iran.Picha: AP

Rais Bush ametowa tahadhari hiyo kwa Waziri Mkuu wa Iraq Nuri al Maliki wakati waziri mkuu huyo akiwa ziarani nchini Iran huku akikabiliwa na matatizo ya kisiasa yanayozidi kukuwa pamoja na shutuma za Marekani kwamba hachukuwi hatua za kutosha kupunguza pengo la utengano wa kimadhehebu.

Wakati akiwa nchini Iran al –Maliki ameahidiwa msaada wa nchi hiyo kurudisha utulivu nchini Iraq lakini ameambiwa na serikali ya Iran kwamba umwagaji damu utamalizika nchini humo baada tu ya kuondoka kwa wanajeshi wa Marekani.

Akiita Iran kuwa taifa la uchokozi sana ambalo lazima litengwe Bush ameonya wakati wa mkutano na waandishi wa habari kwa kusema kwamba ujumbe wake kwake ni kuwa wakati wakimfuma akitimiza dhima ya uharibifu nchini Iraq kutakuwa na gharama ya kulipa.

Amedokeza kwamba Maliki kupigwa picha akitabasamu na wenyeji wake wa Iran akiwemo hasimu wa Marekani Rais Mahmoud Ahmedinejad ni usahihi tu wa kidplomasia.

Akidharao ishara za kuboreka kwa uhusiano kati ya serikali ya Iraq na Iran Bush ambaye anapigania kuungwa mkono kwa Marekani kwa vita vya Iraq ambavyo vinapingwa na watu wengi ameelezea imani yake kwamba yeye na Maliki wanakubalina kwamba Iran ni tishio.

Bush amesema iwapo ishara kutoka kwa Maliki ni kwamba Iran ina tija itabidi awe mkweli kwa rafiki yake waziri mkuu kwa sababu haamini kwamba wana nia ya kutengeneza mambo.Hafikiri kwamba Maliki ndani moyoni mwake anafikiri kwamba wana nia hiyo na yumkini akawa na matumaini ya kuwafanya wawe na tija ya kutengeneza mambo kwa kuweka picha nzuri.Anasema Maliki anajuwa kwamba silaha zinazoingizwa kwa magendo nchini Iraq kutoka Iran na kukabidhiwa kwa watu wa itikadi kali ambao serikali haina udhibiti nao yote yana nia ya kuuwa watu wasiokuwa na hatia ni jambo ambalo huleta vurugu ambapo Maliki anajuwa fika hilo.

Hii ni mara ya pili wiki hii Bush imebidi atetee msimamo wake mkali dhidi ya Iran kwa maneno ya hadhari kwa rafiki yake mkuu huku kukiwepo uwezekano wa kuhitilafiana kwa kadri dhamira ya Iran inavyohusika.

Alimuonya Rais wa Afghanistan Hamid Karzai hapo Jumatatu wakati wa ziara yake huko Camp David nchini Marekani mahala pa kumzikia rais awe mwangalifu sana na Iran baada ya kiongozi huyo wa Afghanistan kutotilia maanani tuhuma za Marekani kwamba serikali ya Iran imekuwa ikiwapatia silaha kundi la Taliban.

Iran ambayo ina idadi kubwa ya Waislamu wa madhehebu ya Shia kama vile Iraq imekuwa na dhima muhimu ya kisiasa nchini Iraq tokea uvamizi uliongozwa na Marekani nchini humo hapo mwaka 2003.

Serikali ya Iran imekataa tuhuma za Marekani kwamba imekuwa ikiwapatia silaha wanamgambo kuchochea umwagaji damu nchini Iraq na badala yake imekuwa ikilaumu hali hiyo kuwa inatokana na kuwepo kwa jeshi la Marekani nchini Iraq.

Bush anatupilia mbali wazo kwamba Iran imekuwa na dhima nzuri ya kutimiza nchini Iraq ambapo umwagaji damu kati ya Mashia walio wengi na Wasunni walio wachache mara nyengine unafikia ukingoni mwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.