1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Bush ajiandaa kuondoka madarakani

Josephat Nyiro Charo13 Januari 2009

Wachambuzi wanamueleza kuwa rais mbaya wa Marekani

https://p.dw.com/p/GXlP

Ingawa rais George W Bush wa Marekani amesema anaamini utawala wake wa miaka minane utaonekana kuwa na maana na historia, ishara si nzuri. Huku kukiwa na malalamiko kwamba sera za kigeni za rais Bush hazikuwa nzuri, kiongozi huyo amesema historia itauhukumu utawala wake. Kiongozi huyo aliyasema hayo wakati wa mkutano wake wa mwisho na waandishi wa habari siku ya Jumatatu wiki hii katika ikulu ya mjini Washington.

Msimu wa mapukutiko uliopita takriban thuluthi mbili kati ya wanahistoria 109 walimueleza rais Geoge W Bush kuwa rais mbaya zaidi katika historia ya Marekani. Wanahistoria wengine 35 walisema rais Bush ni miongoni mwa marais wabaya 10 kati ya marais 42 waliomtangulia. Ilikuwa ni miezi sita tu kabla mzozo mkubwa wa kiuchumi ambao wanauchumi wengi wanaamini utakuwa mbaya kuwahi kutokea tangu kuzorota kwa uchumi katika miaka ya 1930.

Rais Bush anaondoka madarakani Jumanne wiki ijayo umaarufu wake ukiwa umeshuka kufikia kiwango cha chini kabisa kufikiwa na rais katika historia ya hivi karibuni. Mbali na awamu yake ya kwanza kupongezwa, wachambuzi wanasema rais Bush ambaye atakumbukuwa kwa vita vyake dhidi ya ugaidi, ameiharibu haiba ya Marekani ulimwenguni. Hili pengine si tatizo la kuwaumiza vichwa watu kama makamu wa rais Dick Cheney na mahafidhina mambo leo ambao wamejitenga mbali na diplomasia na aina nyengine ya utawala usiotumia nguvu.

Lakini matatizo yanayokabiliwa na jeshi la Marekani nchini Afghanistan na Irak, pamoja na kuonekana kushindwa kwake kupata matokeo yaliyonuiwa katika maeneo mengine ya vita kama vile nchini Somalia na Pakistan au Lebanon, kwa swala la Israel, umedhihirisha mipaka ya ushawishi wa Marekani ulimwenguni na uwezo wa jeshi la Marekani kukamilisha malengo hayo peke yake.

Kitu kikubwa kilichoiharibia sifa Marekani ni uvamizi dhidi ya Irak mnamo mwaka 2003 na matumizi ya mifumo ya kuwahoji washukiwa katika jela za Marekani huko Guantanamo nchini Cuba, Abu Ghraibi nchini Irak na jela za siri zinazosimamiwa na Marekani katika nchi mbalimbali duniani, ambayo watetezi wengi wa haki za binadamu wanaileza kuwa mateso.

Kuiunga mkono Israel waziwazi hata inapofanya harakati ya kijeshi ambazo zinaonekana kutojali masilahi ya raia, kama inavyofanyika hivi sasa katika Ukanda wa Gaza, pia kuliivuruga haiba ya Marekani. Katika hotuba yake wiki iliyopita, mwanamfalme Turki al-Faisal balozi wa zamani wa Saudi Arabia, rafiki wa Marekani na aliyekuwa kiongozi wa ujasusi, alisema utawala wa rais Bush umeichia Marekani sifa mbaya na katika hali ya kutojali kutokana na mauaji ya kiholela na umwagaji damu ya watu wasio na hatia huko Gaza.

Matamamshi hayo yamezusha hisia mbalimbali miongoni mwa wachambuzi wa Marekani. Anthony Cordesman, mtaalam wa maswala ya Mashariki ya Kati katika taasisi ya masomo ya kimkakati na kimataifa, amesema si Israel wala Marekani inayoweza kunufaika kutokana na vita vinavyozusha hisia za namna hii kutoka kwa mojawapo ya watu wenye busara na wasio na msimamo mkali wa kidini katika ulimwengu wa kiarabu.

Awamu ya pili ya rais Bush ilishuhudia msimamo wa serikali yake ukibadilika kutokana na kupingwa kwa vita nchini Irak na kuingia madarakani kwa viongozi walioona ukweli wa mambo wakiongozwa na waziri wa mashauri ya kigeni Condolezza Rice na waziri wa ulinzi Robert Gates, baada ya Donald Rumsfeld kujiuzulu mnamo mwezi Novemba mwaka 2006.

Huku viongozi hawa wakipinga kukabiliana na wanachama wa kundi la nchi zilioelezwa kuwa zinaendeleza uovu, zikiwemo Korea Kaskazini na Iran, viongozi hao walifaulu kumshawishi rais Bush kwamba shinikizo, kuzitenga nchi hizo na vitisho vya kijeshi kwa kweli vimedhihirisha kutozaa matunda yoyote. Walimshawishi pia kwamba kutumia diplomasia kutakuwa na faida ya kuuonyesha ulimwengu kwamba Marekani iko tayari kutumia suluhisho la kidiplomasia kabla kugeukia matumizi ya vita.

Rais Bush alifanya vizuri barani Asia ambako kinyume cha walivyotaka makamu wake Dick Cheney na Donald Rumsfeld, aliendeleza uhusiano na China bila kuiweka kando mshika wake wa karibu Japan. Kufaulu kwake kuishawishi India na hatimaye kusaini mkata wa nishati ya nyuklia mwaka jana kunachukuliwa na wachambuzi wengi kuwa mojawapo ya ufanisi wake mkubwa katika sera yake ya kigeni. Mpango wake wa kupambana na janga la ukimwi wa gharama ya dola bilioni 15 umempa sifa kubwa barani Afrika. Rais Bush anasifiwa kwa kuumaliza mgogoro kati ya serikali ya Sudan mjini Khartoum na Sudan Kusini, ingawa ufanisi huo unagubikwa na mzozo wa Darfur.

Kama mpango wa kuongeza majeshi nchini Irak umefaulu, rais Bush atasifiwa kama rais Harry Truman wa karne ya 21 ambaye umaarufu wake wakati alipokuwa akiondoka ikulu ya 'white house' mnamo mwaka 1953 unakaribiana na wa rais Bush, lakini ambaye ufadhili wake kwa jumuiya ya NATO na mpango wa Marshall Plan bado inapongezwa kama ufanisi mkubwa.

Lakini ikiwa Irak itatumbukia kwenye machafuko au igeuke kuwa nchi inayoongozwa na utawala wa kiimla na kuwa karibu zaidi kwa Iran kuliko ilivyo hivi sasa, rais Bush ataelezwa kuwa rais mbaya zaidi wa Marekani. Historia itakuwa na kibarua cha kuamua.