1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Assad ajinata watashinda vita

29 Agosti 2012

Mapigano yanapamba moto na damu inazidi kumwagika huku walimwengu wakipaza sauti kudai yatengwe maeneo maalum ndani nchini Syria kuwashughulikia wakimbizi .

https://p.dw.com/p/15zAZ
Rais B ashar al AssadPicha: picture alliance/dpa

Rais Bashar al Assad wa Syria anahoji wanajeshi wake wanaweza kushinda vita vinavyoiteketeza nchi hiyo, akisema lakini muda zaidi utahitajika katika wakati ambapo waasi wanapania kuuteka uwanja wa ndege wa kijeshi kaskazini mwa nchi hiyo. Nayo Uturuki pamoja na nchi za magharibi zimetoa mwito patengwe maeneo maalum kuwahudumia wakimbizi nchini Syria kwenyewe.

Hoja za rais Assad, amezitoa katika mahojiano pamoja na kituo cha matangazo kinachoelemea upande wa serikali-Addounia. Hoja hizo ziimetangazwa siku moja tu baada ya gari moja kuripuka wakati wa maziko mjini Damascus na kuangamiza maisha ya watu 27, huku shirika linalopigania haki za binaadam la Syria kuripoti watu zaidi ya 189 wameuliwa katika mapigano ya jana kote nchini Syria.

"Nnaweza kusema kwa ufupi,tunasonga mbele,hali imeanza kuwa nzuri lakini bado hatukushinda vita-hilo litahitaji muda zaidi"-Amesema rais Assad katika mahojiano hayo na kituo cha televisheni cha kibinafsi-Addounia.

Syrien - Kämpfe in der Nähe von Damaskus
Mapigano karibu na DamascusPicha: picture-alliance/dpa

Rais Assad amezungumzia pia pendekezo la Uturuki kuutaka Umoja wa mataifa utenge eneo maalum ndani nchini Syria.

" Halijazuka bado kwanza suala kuhusu eneo maalum na pili fikra hiyo haitekelezeki si kwa mahasimu wala si kwa maadui wa Syria" amesema rais Assad .

Hata waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Laurent Fabius amekiri hii leo mipango kama hiyo itakuwa "shida sana" kuitekeleza.

Baraza la usalama la Umoja wa mataifa litakutana kesho kuzungumzia suala hilo.

Idadi ya wakimbizi wanaoingia Uturuki inazidi kuongezeka.Na wengi wengine wamekwama katika eneo la mpakani,kama anavyosema bwana mmoja aliyefanikiwa kuvuka mpaka na kuingia Uturuki.

"Kuna wakimbizi wasiopungua 2000 wanaosubiri-tumewaona.Hali yao ni mbaya sana.Wanaketi na kulala chini.Hakuna vyoo,hakuna maji wala chakula."-anaasema bwana huyo.

Syrien Flüchtlingslager
Watoto ni miongoni mwa wasyria wanaokimbia mapiganoPicha: picture-alliance/dpa

Wakati huo huo mapigano yanaendelea katika maeneo mbali mbali ikiwa ni pamoja na Aleppo na Damascus.

Shirika linalopigania haki za binaadam nchini Syria,lenye makao yake makuu mjini London linaripoti kuhusu mapigano makali yaliyoripuka karibu na uwanja wa ndege wa kijeshi wa Taftanaz-eneo la kaskazini linalokutikana kati ya miji ya Aleppo na Idlib ngome za waasi na kitovu cha mashambulio ya vikosi vya serikali kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters

Mhariri:Josephat Charo