1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Abbas ziarani Ufaransa

21 Aprili 2011

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy hii leo amemkaribisha Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas mjini Paris, huku Ulaya ikizidi kueleza wazi wazi uwezekano wa kutambua taifa huru la Palestina.

https://p.dw.com/p/RJgE
Palestinian President Mahmoud Abbas attends a Fatah Central Committee and Palestine Liberation Organization (PLO) meeting in the West Bank city of Ramallah, Friday, Feb 18, 2011. (AP Photo/Majdi Mohammed)
Rais wa Wapalestina, Mahmoud AbbasPicha: AP

Hatua yo yote ya Ufaransa kukaribisha taifa la Palestina katika jumuiya ya kimataifa ni ile itakayochukuliwa pamoja na Umoja wa Ulaya. Hatua hiyo itachukuliwa kama ni jitahada ya kuufufua mchakato wa amani wa Mashariki ya Kati uliokwama, kati ya Wapalestina na Waisraeli. Hapo awali, Rais Mahmoud Abbas alisema kuwa anatafuta ushauri wa rais mwenzake Sarkozy, kuhusu jitahada za Utawala wa Wapalestina kuishawishi jumuiya ya kimataifa kutambua taifa huru la Palestina hata kabla ya kupatikana makubaliano ya amani yenye utata.

Mataifa mengi makuu yamekuwa yakisita kutambua taifa la Palestina kabla ya kuundwa rasmi, ikiwa na mipaka iliyokubaliwa. Lakini sasa, baadhi ya nchi hizo, zinaamini kuwa kutambua taifa la Palestina, huenda kukasaidia kuufufua mchakato wa amani wa Mashariki ya Kati uliokwama. Hivi juzi, mjini Paris, waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Alain Juppe aliwaambia maripota kuwa hilo, ni suala linalohitaji kuzingatiwa na linazingatiwa. Akaongezea kuwa Ufaransa inashirikiana na nchi wanachama wenzake katika Umoja wa Ulaya, kujaribu kuwarejesha Waisraeli na Wapalestina katika meza ya majadiliano na hiyo huenda ikafuatwa na hatua ya kutambuliwa taifa la Palestina baadae mwaka huu.

Ufaransa yataka kujiimarisha katika jukwaa la kimataifa

Lakini ziara ya Rais Mahmoud Abbas mjini Paris, inafanywa wakati ambapo Ufaransa inashika wadhifa wa urais katika kundi la nchi tajiri duniani G8 na lile la nchi zilizoendelea kiuchumi G20. Hivi sasa, Ufaransa inafuata siasa kali ya nje yenye lengo la kufufua dhima yake katika jukwaa la kimataifa na hasa msimamo wake katika ulimwengu wa Kiarabu. Itakumbukwa kuwa Ufaransa iliongoza mito ya kimataifa kuchukua hatua dhidi ya serikali ya kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi na ikaongoza mashambulio ya anga ya nchi shirika, dhidi ya vikosi vya Gaddafi. Vile vile Ufaransa ni taifa la kwanza kuanzisha uhusiano na serikali ya waasi wa Libya mjini Benghazi.

Lakini, Ufaransa haimo katika makundi ya mataifa yanayopaza sauti kutambua taifa la Palestina, kama zilivyofanya nchi kadhaa za Latin Amerika. Hata hivyo, Ufaransa inaunga mkono lengo la kunda taifa la Palestina, hadi utakapofanywa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mnamo mwezi wa Septemba. Wiki iliyopita, Utawala wa Wapalestina uliihimiza Marekani kuchukua msimamo dhahiri kuunga mkono taifa huru la Palestina lenye mipaka ya mwaka 1967 - yaani ile iliyokuwepo kabla ya vita vya siku sita na Israel. Vile vile mji wa Jerusalem ya Mashariki ndio uwe mji wao mkuu.

Mwandishi: Martin,Prema/AFPE

Mhariri: Josephat Charo