1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Abbas adhamiria kuwasilisha ombi la Wapalestina

22 Septemba 2011

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Mahmoud Abbas anaazimia kuwasilisha ombi la kutaka taifa la Palestina kutambuliwa katika Umoja wa Mataifa, licha ya Rais wa Marekani Barack Obama kuonya kuwa hakuna njia ya mkato.

https://p.dw.com/p/Rn7f
Palestinian President Mahmoud Abbas attends the 66th session of the United Nations General Assembly, Wednesday, Sept. 21, 2011. (Foto:Richard Drew/AP/dapd)
Rais wa Wapalestina Mahmoud AbbasPicha: dapd

Hotuba ya Rais Obama katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na hata mkutano wake pamoja na Rais Abbas haukusaidia kubadili dhamira ya kiongozi huyo wa Wapalestina kuwasilisha ombi la kutaka uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa. Marekani imeapa kutumia kura yake ya turufu katika Baraza la Usalama kulipinga ombi hilo la Wapalestina, huku ikihofiwa kuwa hatua kama hiyo huenda ikazusha mzozo mpya katika Mashariki ya Kati.

Lakini Israel na Marekani zinashikilia kuwa majadiliano ya ana kwa ana kati ya Waisraeli na Wapalestina ndiyo yatakayoweza kuleta makubaliano ya amani yatakayosaidia kuunda taifa jipya la Palestina. Rais Obama alipohutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hapo jana alisema:"Ninaamini kuwa hakuna njia ya mkato ya kumaliza mzozo uliodumu miongo kadhaa."

President Barack Obama talks with Palestinian President Mahmoud Abbas during a meeting in New York, Wednesday, Sept., 21, 2011. (Foto:Pablo Martinez Monsivais/AP/dapd)
Rais Barack Obama (kulia) na Rais Mahmoud AbbasPicha: dapd

Katika hotuba yake, hakutaja kitisho cha Marekani kutumia kura yake ya turufu kwenye Baraza la Usalama, lakini alisema, amani haitopatikana kwa kutoa taarifa na kupitisha maazimio katika Umoja wa Mataifa. Ingekuwa rahisi hivyo, basi hivi sasa amani ingeshapatikana. Kwa kweli, Obama anajikuta katika hali ya kufedhehesha, kwani alipolihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa miezi 12 iliyopita, alitoa mwito wa kuwapatia Wapalestina uanachama kamili katika kipindi cha mwaka mmoja. Hapo jana, alisema kuwa wakati huo na hivi sasa pia anaamini, Wapalestina wanastahili kuwa na taifa lao wenyewe. Lakini Israel pia, ihakikishiwe usalama wake kwa sababu ya vitisho vya majirani waliopigana nao vita mara kwa mara.

French President Nicolas Sarkozy, addresses the 66th session of the United Nations General Assembly at U.N. headquarters Wednesday, Sept. 21, 2011. (AP Photo/Jason DeCrow)
Rais wa Ufaransa, Nicolas SarkozyPicha: dapd

Nae, Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy ameonya kuhusu hatari ya wimbi la machafuko kutokea katika Mashariki ya Kati ikiwa Marekani itatumia kura ya turufu. Yeye amependekeza kuwapatia Wapalestina hadhi ya kuwa mwanachama mwaangalizi katika Umoja wa Mataifa kama hatua ya kuelekea kwenye uanachama kamili. Akaongezea kuwa, itayarishwe ratiba ya kuanzisha majadiliano mapya kati ya Waisraeli na Wapalestina katika kipindi cha mwezi mmoja na makubaliano ya dhati yapatikane katika muda wa mwaka mmoja. Akazungumzia juu ya jukumu la kisiasa na kuonya kwamba nchi moja pekee haiwezi kuutatua mzozo huo, bali mchango wa jumuiya nzima ya kimataifa.

Mpatanishi mkuu wa Wapalestina, Nabil Shaath amesema, kabla ya kwenda kwenye Baraza Kuu, Rais Abbas atalipa Baraza la Usalama muda wa kuzingatia ombi la uanachama kamili. Marekani ikitumia kura yake ya turufu katika Baraza la Usalama, basi Wapalestina watakwenda katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwasilisha ombi la kupewa hadhi ya kuwa mwanachama mwangalizi kama vile Vatican.

Katika Baraza Kuu, wingi wa kura tu unatosha na kura ya turufu haiwezi kutumiwa huko. Wasiwasi wa Israel ni kuwa hata hadhi ya mwanachama mwaangalizi huenda ikawapa Wapalestina haki ya kuwa mwanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu na kufikisha malalamiko yake kuhusu Israel. Katika mapendekezo ya Sarkozy, rais huyo wa Ufaransa ametoa mwito kwa Wapalestina kutokwenda katika mahakama hiyo wakati wa kufanya majadiliano.

Mwandishi: Martin,Prema/afpe

Mhariri:Josephat Charo