1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia zaidi wauawa Afghanistan na majeshi ya NATO:

Halima Nyanza22 Februari 2010

Wakati serikali ya muungano ya Uholanzi imevunjika kutokana na suala la kuwepo wanajeshi wake Afghanistan, Afghanistan, kwenyewe kuna taarifa kwamba Wanajeshi wa Jeshi la NATO. wameua tena raia.

https://p.dw.com/p/M8ER
Waziri Mkuu wa Uholanzi Jan Peter Balkenende, ambaye serikali yake imevunjika kutokana na suala la kuwepo wanajeshi wa nchi hiyo Afghanistan, ambapo jeshi la kimataifa linaarifiwa kuua raia wasio na hatia zaidi.Picha: AP

Raia hao wasiokuwa na hatia wameuawa katika shambulio lililofanywa na ndege za Jeshi hilo la kujihami la NATO, kusini mwa Afghanistan, baada ya kuwadhani kuwa ni wapiganaji na kwamba miongoni mwa waliouawa ni wanawake na watoto.

Akizungumzia shambulio hilo, gavana wa jimbo hilo, Sultan Ali Uruzgani amesema shambulio hilo la anga dhidi ya msafara wa magari matatu yaliyowapakiza raia lililotokea katika jimbo la Dai Kundi, lililengwa na wanajeshi hao wa NATO.

Nayo taarifa iliyotolewa na Ofisi ya rais wa nchi hiyo, imesema kwamba Baraza la Mawaziri chini ya uongozi wa Rais wa Nchi hiyo, Hamid Karzai, limelaani vikali shambulio hilo.

Mawaziri hao pia wameyataka majeshi ya NATO, kuwa makini zaidi kabla ya kufanya mashambulio yao ya kijeshi.

Kwa upande wake, Kamanda wa NATO, nchini Afghanistan, Jenerali katika jeshi la Marekani Stanley McChrystal tayari binafsi ameomba radhi kwa Rais Karzai na kuahidi  kuongeza juhudi ili kuaminiwa zaidi na Waafghanistan.

Katika taarifa yake aliyoitoa leo, Jenerali McChrystal amesema wamesikitishwa na tukio hilo lililopoteza maisha ya watu wasio na hatia, na kukiri kuwa kuwalinda raia ni jambo muhumu katika mapambano hayo dhidi ya Taliban.

Aidha amelitaka jeshi hilo la NATO kuwekea mipaka matumizi ya mashambulio ya anga.

Kuuawa kwa raia wasio na hatia katika mashambulio hayo, kumekuwa chanzo kikubwa cha wasiwasi kati ya serikali ya Afghanistan na Majeshi ya Kimataifa, ambapo maafisa wa Afghanistan wanasisitiza kuwa vifo kama hivyo vinadhoofisha uungaji mkono wa umma kwa zaidi ya majeshi laki moja na elfu 13 ya kigeni na katika serikali ya nchi hiyo.

Wakati hayo yakitokea, Waziri Mkuu wa Uholanzi, nchi ambayo pia ina majeshi yake nchini Afghanistan Jan Peter Balkenende amekutana na Malkia Beatrix wa nchi hiyo, kuanza mchakato unaoonekana kupelekea kufanyika kwa uchaguzi wa mapema, katika kipindi hiki cha majira ya ya kuchipua baada ya serikali yake kuvunjika kutokana na mabishano makali juu ya majeshi ya nchi hiyo kujitoa nchini Afghanistan.

Hata hivyo Bwana Balkenende hakutoa taarifa zozote kuhusiana na mkutano wake huo na malkia.

Waziri Mkuu wa Uholanzi amekuwa akitaka Malikia kukiidhinisha chama chake cha Christian Democratic Alliance kuongoza serikali ya muda katika kipindi cha mpito mpaka pale uchaguzi utakapofanyika na serikali mpya kuundwa.

Bwana Balkenende alitangaza kujiuzulu, baada ya chama chake kushindwa kufikia makubaliano na vyama vinavyoshirikiana nacho katika serikali ya  muungano, juu ya suala la kuwepo kwa majeshi ya nchi hiyo nchini Afghanistan.

Kwa sasa Uholanzi ina kiasi cha wanajeshi elfu mbili ambao wako katika jimbo la Uruzgan kusini mwa Afghanistan.

Mwandishi: Halima Nyanza(dpa,ap)

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed